Hakuna kitu kinachowaumiza na kuwarudisha watu wengi nyuma kama dharau na matusi ya wengine.

Pale ambapo mtu unajitahidi kufanya kitu kikubwa, lakini wale wanaokuzunguka wanakudharau na hata wakati mwingine kukutukana, inakuwa vigumu sana kwako kuendelea.

Na pale unapokutana na ugumu kwenye kufanya au unaposhindwa, unakubaliana na wale waliokudharau na kukutukana.

Lakini ipo kinga moja ya dharau na matusi ya wengine, ambayo ukiwa nayo, dharau na matusi ya wengine hayatapata nafasi kabisa ya kukurudisha nyuma.

Kinga hiyo ni kujithamini wewe mwenyewe, kujua kuna kitu kikubwa na cha kipekee ambacho kipo ndani yako. Kwa kujua na kuthamini kile kilichopo ndani yako, matusi na dharau za wengine kwako zitakuwa kelele tu ambazo hazina nafasi.

Kwa chochote kikubwa unachotaka kwenye maisha yako, kwanza anzia ndani yako, anza na thamani kubwa iliyopo ndani yako. Jua hakuna anayeweza kuona au kujua kilichopo ndani yako ila wewe mwenyewe. Hivyo kuwasikiliza maneno yao na kuyaamini ni kujipoteza wewe mwenyewe.

Watu hawataacha kusema, na hutaweza kuwapangia watu waseme nini. Wewe jukumu lako ni kufanya kile ulichopanga kufanya, usipoteze muda kuwasikiliza, hakuna kipya wanachoweza kukuongezea.

Hata kama unajiambia utapata ushauri mzuri kupitia kukatisha kwao tamaa, siyo kweli, huhitaji mtu wa kukuambia kwamba safari yako itakuwa ngumu na utakutana na vikwazo, unapaswa kujua hilo tangu unaanza. Na kuwa na watu wa kukumbusha hilo mara kwa mara hakutabadili chochote kwako.

Jithamini wewe mwenyewe, jua utofauti mkubwa uliopo ndani yako na chukua hatua, usiwasikilize wanaokudharau na kukutukana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha