Siku hizi watu wamekuwa wanashindwa kutatua matatizo yao binafsi kwa sababu tunaelekea kusahau kwamba matatizo haya ni muhimu kwa watu gani.
Uwepo wa mitandao ya kijamii na urahisi wa mawasiliano umewafanya watu kukimbilia kutoa matatizo yao binafsi kwa wengine kuliko kukaa chini na kuyatatua.
Mtu anakuwa na tatizo, badala ya kukaa nalo na kulitatua, anakimbilia kuliweka kwenye mitandao au kuwasiliana na wengine, akiamini atapata ushauri bora wa kutatua tatizo hilo. Lakini ni mara chache mno watu wanapata ushauri mzuri kwa njia hizo. Na hata wanapoupata, bado kuufanyia kazi inakuwa vigumu kwao.
Kitu kingine kinachowafanya wengi kushindwa kutatua matatizo yao ni kufikiri matatizo hao ni muhimu kuliko kitu kingine chochote. Hivyo wanataka dunia isimame, kila mtu aache kufanya anachofanya na ashiriki kwenye kutatua matatizo yake.
Ukweli ni kwamba matatizo yako ni muhimu kwako tu, hakuna mwingine anayeumizwa na matatizo yako kama unavyoumizwa nayo wewe. Na kumbuka kila mtu anahangaika na matatizo yake, hivyo hakuna anayetumia muda mwingi kuyafikiria matatizo yako kama unavyodhani. Kila mtu anakazana na matatizo yake.
Kwa kujua haya, unapokutana na tatizo lolote kwanza unajua ni muhimu kwako na siyo wengi wanataka kulisikia au hata wakilisikia watalifikiria. Pia kama unahitaji ushauri kwenye kutatua tatizo unalokutana nalo, chagua mtu sahihi ambaye yupo tayari kukusikiliza na kukushauri kwa kina, badala ya kuweka kwenye mitandao ambapo watu hawana muda wa kufikiri kwa kina, badala yake wanakuambia kile wanachojisikia tu kusema.
Ukizingatia hayo mawili, utaweza kutatua sehemu kubwa sana ya matatizo makubwa unayokutana nayo huku ukiwa na utulivu wa maisha yako na watu wakidhani labda mambo yako yanaenda murua bila ya matatizo yoyote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kweli kocha huwezi pata msaada kwa kupost matatizo yako ktk mtandao wa kijamii hakuna anaejali tatizo la mwingine.muhimu kuwa na mtu unaemwamini na atakae kusaidia ahsante kocha kwa makala ya leo !!!!
LikeLike
Karibu sana Hendry.
LikeLike