“Erase the false impressions from your mind by constantly saying to yourself, I have it in my soul to keep out any evil, desire or any kind of disturbance—instead, seeing the true nature of things, I will give them only their due. Always remember this power that nature gave you.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.29
Siku mpya, siku bora na siku ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora sana.
Tuianze siku hii kwa shukrani za kipekee, kwa kuwa kuiona siku hii ni bahati ya kipekee sana kwetu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; NGUVU YA KAULI UNAZOJIAMBIA…
Zile kauli unazojiambia kila siku, zina nguvu kubwa sana kwenye maisha yako.
Kila unachojiambia, iwe ni kwa sauti au kimya kimya ndiyo unachokiamini na kukifanya.
Ni vigumu sana kufanya kinyume na kile unachojiambia.
Kwa kujua nguvu hii ya kauli unazojiambia, unaweza kuitumia kwa manufaa yako.
Unachofanya ni kujiambia kauli chanya na za kukupeleka mbele zaidi.
Chagua kauli chanya ambayo utajiambia kila wakati unapokwama au kukutana na changamoto.
Kuwa na kauli za kujiambia kwenye kila hali ili uweze kusonga mbele zaidi.
Kwa mfano unapokutana na ugumu na kufikiria kuacha unachofanya, jiambie “NINAWEZA KIFANYA KILA NINACHOTAKA KUFANYA NA NITAFANYA SASA” jiambie kauli hii kwa sauti na rudis mara nyingi uwezavyo. Kwa kufanya hivyo akili na mawazo yako yanabadilika, huoni tena ugumu bali njia ya kufanya.
Kadhalika unapoamka asubuhi, kuwa na kauli chanya na ya ushindi wa siku yako unayojiambia mara nyingi.
Pia unapojikuta ukifikiria mambo hasi au kufikiria ubaya juu ya wengine, kuwa na kauli chanya ya kujiambia na kukutoa hapo.
Kauli unazojiambia huku ukiziamini zina nguvu kubwa sana kwako na zinaweza kuleta mabadiliko makubwa kwako.
Fanya zoezo hili kila siku na kila mara, usiishie tu kufikiria kauli hizo chanya, bali jiambie kwa sauti na pia ziandike.
Hata kwenye malengo yako makubwa, jiambie kwa kauli ambayo umeshayakamilisha tayari, na hili litakupa nguvu zaidi ya kuyafikia.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujiambia kauli chanya zitakazokusukuma upige hatua zaidi kwenye maisha yako.
#KauliHuumba, #NguvuYaKufikiriChanya, #UnakuwaUnachojiambia
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha