“At every moment keep a sturdy mind on the task at hand, as a Roman and human being, doing it with strict and simple dignity, affection, freedom, and justice—giving yourself a break from all other considerations. You can do this if you approach each task as if it is your last, giving up every distraction, emotional subversion of reason, and all drama, vanity, and complaint over your fair share. You can see how mastery over a few things makes it possible to live an abundant and devout life—for, if you keep watch over these things, the gods won’t ask for more.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 2.5
Tumeipata nafasi nyingine nzuri sana kwetu rafiki.
Ni fursa ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari FANYA KILICHO MBELE YAKO…
Ni rahisi sana mawazo yetu kuhama hama na kufikiria vitu ambavyo havihusiani kabisa na kile tunachofanya.
Wajibu wako kama mtu, kama mwanamafanikio ni kufanya lile jukumu ambalo lipo mbele yako, na kuhakikisha mawazo yako yote yapo kwenye jukumu hilo.
Kila unachofanya, kifanye kwa ustadi wa hali ya juu, kifanue kwa mapenzi, kwa uhuru na kwa haki.
Jipe mapumziko kutoka kwenye usumbufu wa aina yoyote ile, na weka akili na nguvu zako kwenye kile unachofanya.
Wengine wanafanya nini hilo halikuhusu na wala haliko ndani ya uwezo wako.
Wengine wanasema nini juu yako ni kupoteza muda wako kufikiria au kutaka kujua.
Achana na yote hayo na fanya kazi yako, kwa umakini wa hali ya juu.
Chukulia kila jukumu unalofanya kama ndiyo jukumu la mwisho kufanya kwenye maisha yako, kama vile hutapata nafasi nyingine tena.
Sasa jiulize kama una nafasi ya mwisho kabisa ya kufanya kitu kimoja tu halafu ukikimaliza maisha yako yameisha, je utatumia muda huo kufanya vitu visivyo na umuhimu?
Je wakati unafanya ulichopanga kufanya, utaruhusu usumbufu wowote ukuingilie kwenye ufanyaji wako?
Majibu ni hapana, utafanya kilicho muhimu na utafanya kwa utulivu na kuepuka kila aina ya usumbufu.
Kubobea vitu vichache na kuvifanya kwa ufanisi mkubwa kutakupa mafanikio makubwa na maisha yenye utoshelevu wa hali ya juu.
Epuka kila aina ya kelele na achana na yasiyo muhimu.
Chagua kufanya yaliyo muhimu na ondokana na usumbufu mwingine wowote.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchagua kufanya yaliyo muhimu na kuepukana na usumbufu wa mitandaonya kijamii, habari na kufuatilia maisha ya wengine.
#KuwaNaVipaumbele, #EpukaUsumbufu, #BobeaMachacheMuhimu
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha