Watu wengi wanapokuwa wanaanza kazi au biashara mpya wanakuwa na hamasa kubwa sana mwanzoni. Japo mwanzo unakuwa mgumu, lakini watu hao wanakuwa na msukumo makubwa wa kujifunza na kuweza kufanya vizuri kile kipya wanachoanza.

Kadiri muda unavyokwenda wanajua kila wanachopaswa kujua na hapo ndipo tatizo kubwa linapoingia, wanazoea kile wanachofanya na hilo linawapeleka kuchoka kukifanya.

Kile ambacho mwanzo kiliwapa hamasa ya kujituma zaidi, sasa wakikiangalia wanakuwa hawana hata msukumo wa kukifanya. Wanaona ni kawaida na hakuna kipya, wanaona ni kurudia yale yale ambayo wamekuwa wanafanya miaka na miaka na kwa kifupi inachosha.

Tatizo kubwa sana linalopelekea watu kufika kwenye hali hii ni kuacha kukua. Pale mwanzoni mtu anapokuwa hajakizoea kitu, anakuwa anajifunza na kukua zaidi kadiri anavyokwenda. Lakini anapofika hatua ya kujua yale ya msingi, anaacha kujifunza na kujaribu mambo mpya na kufanya kwa mazoea.

Katika hatua hiyo anaacha kabisa kukua, na hapo ndipo mazoea na kuchoka kunakoleta shida.

Sisi binadamu ni viumbe hai, na sifa ya kiumbe hai yeyote ni kukua. Hili linaonekana wazi kwa kila kiumbe, angalia hata miti na wanyama, huwa wanaendelea kukua kadiri siku zinavyokwenda, hawabaki pale walipo. Hata mtu mkubwa kiasi gani, kila wakati wa msimu unatoa majani mapya, maua mapya na hata matunda mapya.

Ukuaji ni kanuni ya asili ya viumbe hai wote, kanuni ambayo hata wewe binafsi unaweza kuitumia na ukaweza kukua zaidi na kuendelea kuwa na hamasa kwenye kile unachofanya.

Kuweza kutumia vizuri kanuni hii ya ukuaji na kuondoka kwenye mazoea, mara zote jisukume kufanya ambacho hujawahi kufanya. Kila wakati jaribu kitu kipya ambacho hujawahi kufanya huko nyuma. Hata kama ni kidogo kiasi gani, hata kama kinakupa hofu kiasi gani, wewe jaribu na hilo litakuweka kwenye mchakato wa ukuaji, ambao utakuwezesha kuwa na hamasa ya kupiga hatua zaidi.

Kila unapojiambia kwamba umeshazoea au tayari unajua kila kitu, chagua kitu kipya cha kufanya, ambacho kitakusukuma zaidi ili uwe bora zaidi ya ulivyo sasa.

Hiyo ndiyo kanuni muhimu ya ukuaji na kutokuzoea chochote unachofanya sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha