Rafiki yangu mpendwa,

Miili yetu ni sawa na betri ya simu. Unapokuwa umelala ndiyo unachaji betri hii, hivyo unapoamka asubuhi nguvu unayokuwa nayo ni sawa na betri iliyojaa kwa silimia 100.

Lakini sote tunajua ya kwamba unapoanza kutumia simu yako, basi chaji iliyokuwa imejaa inaanza kupungua. Kama chaji ilikuwa asilimia 100 kila unachotumia kinapunguza chaji hiyo.

Sasa pata picha, una simu ambayo umeanza nayo asubuhi na chaji ni asilimia 100, ila hutaweza tena kuichaji kwa siku nzima mpaka usiku utakapofika. Halafu jioni, una simu muhimu sana ya kikazi au kibiashara itaingia, hivyo unahitaji kuwa na chaji ya kutosha kwenye simu yako ili kuweza kuwasiliana kwa simu hiyo. Je utatumiaje simu yako kwa siku nzima?

Je utatumia chaji hiyo kuzurura kwenye kila mtandao wa kijamii, kucheza michezo iliyopo kwenye simu au kuwasiliana na watu kwa sababu tu una dakika au meseji za bure?

discharged-battery-fully-charged

Bila shaka utachunga sana chaji yako, kila unachofanya utajiuliza kama ni muhimu na kila wakati utaangalia ni chaji kiasi gani imebaki na utajaribu kuipangilia ili iweze kukufikisha kwenye simu muhimu ya jioni.

Sasa kama unavyopata mfano huu wa betri ya simu, ndivyo mwili wako na akili yako vilivyo. Unapoamka asubuhi unakuwa na nguvu nyingi kimwili na kiakili za kukuwezesha kufanya makubwa. Lakini kila maamuzi unayofanya kwenye siku yako, yanapunguza nguvu hiyo.

Pale unapoanza kubishana na wewe mwenyewe iwapo uamke au la, unapunguza nguvu yako ya kiakili, unapoamka na kuanza kufikiria uvae nguo gani unapunguza nguvu hiyo. Unapoamka na kuanza kufuatilia habari na yanayoendelea unapunguza nguvu hiyo. Unapoamka na kuanza kugombana na watu au kukumbuka watu uliogombana nao siku za nyuma inapunguza nguvu hiyo.

SOMA; Hii Ndiyo Nguvu Kubwa Iliyopo Ndani Yako, Unayoweza Kuitumia Kupata Chochote Unachotaka.

Haishangazi kwa nini wengi mpaka unapofika kuanza majukumu yako ya siku umeshachoka na hujui hata ufanye nini. Ni kwa sababu unatumia vibaya nguvu zako unazoanza nazo kila siku. Ni sawa na mtu ambaye anaanza kutumia simu yake asubuhi kwa kucheza ‘magemu’ yaliyopo kwenye simu hiyo, au kutembelea mitandao ambayo haina maana.

Njia pekee ya kukuwezesha wewe kutumia nguvu zako vizuri na kutokuchoka haraka ni kuepuka kufanya maamuzi na kuchukua hatua ambazo hazina manufaa yoyote kwako. Epuka ana kusumbuka na mambo yasiyo muhimu kwenye mwanzo wa siku yako.

Unapofika muda wa kuamka amka bila ya kuanza kubishana na wewe mwenyewe, usikimbilie kupata habari au yanayoendelea asubuhi na mapema. Na pia unapofika wakati wa kuondoka nyumbani, usianze kubishana na wewe mwenyewe uvae nini au upite wapi.

Kazana sana kupunguza maamuzi unayofanya kwenye mwanzo wa siku yako ili utunze nguvu zako kwa yale mambo ambayo ni muhimu zaidi. Jiwekee utaratibu wa kuianza siku yako ambapo tangu unapoanza mpaka unapomaliza kila kitu kimepangiliwa. Siyo unamaliza kufanya kitu kimoja halafu unaanza kujiuliza ni kipi kingine ufanye, hapo unapoteza muda na nguvu zako nyingi.

Linda nguvu za akili na mwili wako kama unavyolinda chaji ya betri yako pale unapojua kuna simu ya muhimu baadaye na huwezi kuichaji tena kwa siku hiyo. Kwa sababu akili yako ndiyo betri kuu ya maisha yako, ukiweza kuitumia vizuri itakupa chochote unachotaka.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge