Mpendwa rafiki yangu,
Kila binadamu kadiri ya imani yake huwa anasali, na kama tunavyojua sala ina nguvu ndani yetu. kile ambacho tunakirudia kukiomba kila siku huwa kinakaa kwenye akili yetu sana mwishowe kinakuja kuwa kweli. Kumbe basi, kuna nguvu kubwa sana ya kujitamkia maneno yenye nguvu kila siku ya maisha yako.
Kuna sala ambayo inapendwa sana na karibu na waumini wa dini zote duniani. Sala ambayo inapendwa na karibu dini zote, ambayo imekuwa kama wimbo wa taifa katika zama hizi za taarifa siyo sala nyingine bali kulalamika na kunung’unika.
Tunaona kuwa binadamu ana asili ya kulalamika kwenye kila jambo. Binadamu ni kama tumbo hata ulipe chakula kizuri namna gani, bado halitoweza kuendelea kuwa na shukrani. Umfanyie kitu kizuri au kibaya hatokosa kulalamika au kunung’unika kwa kasoro yoyote ile.
Ukiwa mkusanyiko wa watu, nyumba za ibada, sherehe, kwenye mabasi ya umma , makazini na kwenye jumuiya zetu utakutana na watu wanaolalamika na kunung’unika juu ya jambo fulani.
Tukiangalia hata enzi na enzi wana wa Israeli walimlalamikia Mungu kupitia kiongozi wao Musa. Hakuna sehemu ambayo hakuna watu ambao hawalalamiki. Ukienda hospitali utakutana na wagonjwa waliokata tamaa na wanachukulia kulalamika ni kama sehemu ya kumaliza matatizo yao. Kulalamika kuwekuwa ni sumu ya maendeleo karibu sehemu nyingi ya maisha yetu.
Kwenye mahusiano yetu kama ndoa, manung’uniko yako. watu wanashindwa kuishi maisha ya furaha, hawaangalii katika uchanya bali kwenye uhasi na uhaba tu. Kama tungekuwa tunachukulia mambo katika mtazamo chanya tusingekuwa tunalalamika kila siku. Hebu niambie ni sehemu gani ambayo watu hawanung’uniki na kulalamika? Watu wanalalamika kwenye kila eneo la maisha yao.
Ukija katika maisha ya kiroho watu wanasali wakiona hawapati kile wanachotaka wanaanza kumlalamikia Mungu kuwa hawapi kile wanachotaka. Tumekuwa siyo watu wa kushukuru kwenye kila jambo bali tumekuwa ni watu wa kulalamika kwenye kila jambo.
Rafiki yangu, kulalamika ni kupoteza muda na nguvu, utamaduni wa kulalamika umezaa wavivu wengi. Mambo yanaenda ndivyo sivyo kwa sababu ya sisi wenyewe kutochukua hatua na kuamini kuwa jukumu la maisha yetu siyo letu ni la wengine. Tunatakiwa kulibeba jukumu la maisha yetu, na kuamini kuwa jukumu la maisha yako ni lako mwenyewe na hakuna anayekosa usingizi kwa sababu ya maisha yako.
Hatua ya kuchukua leo; acha kulalamika. Ukiona jambo jiulize swali hili mara moja, je liko ndani ya uwezo wangu? au liko nje ya uwezo wako? Ukiona liko ndani ya uwezo wako litatue na ukiona liko nje ya uwezo wako achana nalo lisikupotezee muda.
Kwahiyo, ni marufuku kulalamika, kulalamika ni roho ya umasikini na uhaba. Unapopenda kulalamika na mabaya mengi yanakuwa yanakuja katika maisha yako. Hata kama unapitia magumu kiasi gani kuw amtu wa shukrani.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana