Mpendwa rafiki,

Ndoa ndiyo chemchem ya miito yote hapa duniani. Hatuwezi na familia bora kama hatuna ndoa iliyo bora. Ndoa ni mama wa kila kitu, matunda tunayaona hapa duniani chanzo chake ni ndoa bora. Ndoa ni mpango wa Mungu na siyo mpango wa mwanadamu na kwa asili ndoa siyo bali mitazamo ya watu kadiri ya tafsiri zao ndiyo hupelekea maneno mengi katika jamii yetu.

Binadamu ni viumbe vya hisia hivyo kama ni viumbe vya hisia unatakiwa kama wewe ni mwanandoa ucheze na hisia za mwenzako. Uwe mtu wa kujali hisia za mwenzako na kile unachomfanyia mwenzako ujiulize mara mbili kabla hujamfanyia je ni sahihi kumfanyie hivyo? Kama siyo sahihi usifanye.

Hata maneno tunayoongea na kuwaambia wenzetu muda mwingine tunakosea, sasa kabla hujamwambie mwenzako maneno yoyote yale, chuja kwanza na chuja kwa kujiuliza je ni sahihi kumwambia? Ukiona siyo sahihi kusema hicho unachotaka kusema usiseme na kaa kimya. Maneno ni chanzo cha ugomvi katika ndoa nyingi unakuta mmoja wa wanandoa anamjibu mwenza  wake vile anavyotaka na hii baadaye huleta mpasuko.

Kuna hali ya adimu kutokea katika ndoa za siku hizi, kitu ambacho watu wanaona ni cha kawaida lakini kina thamani sana, unaweza kuona ni kitu kidogo lakini ikitokea mtu anakipata kutoka kwa watu wa nje lakini ndani hakipatikani  lazima utakuwa unajitengenezea matatizo mwenyewe.

urafiki kwenye ndoa

Hali hiyo ni kupongezana, kuna baadhi ya wanandoa hawapongezani, yaani lack of appreciation. Ukikosa kumthamini mwenzako unakuwa unampa shida, wewe ndiyo mtu wa kwanza unayetakiwa kumtia moyo mwenza wako kwa hali yoyote ile.

SOMA; Hii Ndiyo Sala Kuu Inayopendwa Na Watu Wengi Duniani

Pale mwenzako anapofanya vizuri unatakiwa umpongeze, ni wajibu wako kufanya hivyo, wako wanandoa ambao wanakiri kabisa hata wafanye kitu kizuri mke au mume wake haoni wala hapongezi hivyo hii inakuwa inakatisha hata tamaa. Wanandoa wamekuwa ni watu wa kupata pongezi kutoka kwa watu wa nje lakini kwa watu wa ndani hakuna.

Kitu ambacho mtu anatakiwa akipate ndani lakini anaenda kukipata nje, na kila binadamu anapenda kuhisi kuthaminiwa hivyo usipomthamini mwenza wako na akapata mtu anayemthamini ni rahisi sana  kutekwa na wengine.

Mke au mume wako ni mteja wako, najua unajua falsafa ya mteja ambayo ni mteja ni mfalme, bila huyo mwenza wako hakuna ndoa yaani hakuna biashara, ndiyo maana huwa nasema ndoa ni biashara na kama mteja wako ni mwandoa mwenzako.

Hebu tu kaa chini angalia jinsi unavyomhudumia mteja wako yaani mwenza wako ni huduma adimu? Kama unamhudumia hovyo akikutana na watu ambao wanahudumia vizuri je unafikiri ataweza kuvumilia kukaa kwako? Je huduma unayompatia itamfanya mteja wako arudi tena aendelee kubaki na wewe au ndiyo unamfukuza?

Wengi wa wanandoa huwa wanafukuza mwenza wao kwa huduma mbovu ndani ya ndoa. Kama unapata kile unachokitaka ndani ya ndoa yako ya nini sasa kuangaika na mambo ya nje? Hapa ni inatupaswa kujichunguza namna tunavyowahudumia wenza wetu, huenda unatoa huduma ambayo siyo adimu ni ya kawaida hivyo ikitokea akahudumiwa vizuri kile ambacho mteja anakitaka hawezi kurudi katika huduma ya kawaida.

Asili ya binadamu ni kupenda vizuri na mtu anapopata vitu vizuri anahudumiwa vizuri anahisi kuthaminiwa. Hivyo basi, unaweza kufufua mahusiano yako leo kwa kutoa huduma bora na siyo bora huduma katika ndoa yako.

Hatua ya kuchukua leo; mpongezi mwenza wako pale anapofanya vizuri, pongeza kwa kitu chochote kile ambacho ni kizuri hata kama amevaa vizuri na amependeza kuwa wa kwanza kumsifia na usiache watu wa nje wakusaidie majukumu kama hayo.

SOMA; Kitu Chenye Nguvu Kubwa Katika Maisha Ya Ndoa

Kwahiyo, unaweza kufufua ndoa yako kwa kufuata mbinu bora za kumhudumia mteja katika biashara na ipeleke katika ndoa. Hakikisha unafanya kitu cha ziada ile mteja wako asiende wala asipagawe na huduma za wengine. Fanya huduma yako ni bora ambayo hawezi kuipata sehemu nyingine yoyote ile kwako tu.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana