Mpendwa rafiki yangu,
Tukianza mahusiano ya kawaida mpaka mahusiano ya ndoa kila mahusiano yanadai ustarabu wake. Mpaka umekua na mahusiano na mtu ambaye unaye sasa basi kuna kitu kizuri ambacho umekipenda kutoka kwake ndiyo maana uko naye. Na mara nyingi watu ambao tunao sisi tumewachagua kuishi au kuwa marafiki wetu kwa sababu wanaendana na sisi kitabia.
Ndiyo maana tunaambiwa nioneshe rafiki yako, nitakuambia wewe ni nani. Yule ambaye tuko naye katika maisha umekuwa naye kwa sababu ya tabia zetu zinaendana. Sisi binadamu ni kama sumaku hivyo huwa tunatabia ya kuvuta watu wanaoendana na sisi. Jaribu kuchunguza na utaliona hivyo hata marafiki ambao unao wanaendana na tabia zako.
Kumbe basi, mahusiano mazuri yanaenda na tabia za watu ambao wako kwenye mahusiano. Kabla hujaingia kwenye mahusiano na mtu unaalikwa kujiuliza, je anaendana na tabia zako? Kama anaendana na tabia zako sawa vizuri ila kama haendani na tabia zako achana naye mtakuja kusumbuana tu huko mbeleni.
Kitu kidogo sana ambacho hakihitaji hata mtaji ambacho kinachangia kuvunja mahusiano mengi kama ya uchumba na ndoa ni heshima. Kukosa kuheshimiana kwa wana mahusiano wengi ni tatizo kubwa. Mke au mume kila mmoja anadai heshima yake, ukienda kinyume na hivyo lazima mtaanzisha mgogoro fulani.
Kama uko katika mahusiano ya ndoa hakikisha unakuwa na heshima kwa mke au mume wako. Heshima ni kitu cha bure, unapomheshimu mtu naye atakuheshimu. Baadhi ya wanandoa hawaheshimiani kabisa, wanakosa heshima hivyo kila mmoja anakua huru kumkosea heshima mwenzake mbele za watu.
Ni fedhea sana, pale unajikuta mwenza wako anakokusea heshima anakusema mbele za watu, huku ni kudharirishana. Mambo ya wanandoa yanatakiwa yamalizwe au yaongelewe kwenye kuta nne za chumba zenu.
Ila mwandoa kuanza kutangaza mambo ya mwenza wako nje kwa huko ni kukoseana heshima kabisa. Mnatakiwa kulindana, kila mmoja amtunzie mwenza wake heshima na siri zake. Siyo vizuri kumtangazia mwenza wako mambo yake binafsi hadharani au kutaja siri za mwenza wako kwa kila mtu.
SOMA; Hali Adimu Kutokea Katika Ndoa Za Siku Hizi
Mtu akikuamini katika mahusiano yoyote yale, hakikisha unamtunzia siri zake na kumpatia heshima zake. Heshima ni kitu kidogo na ni cha bure tu lakini kina nguvu ya kulinda au kuvunja kabisa mahusiano ambayo tunayo.
Hatua ya kuchukua leo; linda mahusiano yako, mpe heshima anayostahili yule ambaye uko naye kwenye mahusiano.
Kwahiyo, mahusiano yenye heshima ni mahusiano yanayofaa kuishi kwa kila mmoja wetu. kama ulikuwa unamkosea mwanamahusiano wako basi anza kujenga utamaduni wa kujengeana heshima sasa. Inawezekana hivyo anza kufanyia kazi.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana