Ukilinganisha na umri ambao dunia imekuwepo na itaendelea kuwepo, maisha yetu ni mafupi sana. Hata kama utaishi miaka mia moja, ukilinganisha na mabilioni ya miaka ambayo dunia imekuwepo, muda tunaoishi ni kama tone la maji kwenye bahari.

Kwa muda huo mfupi, wapo watu ambao wameweza kuacha alama kubwa hapa duniani, ambao licha ya kuondoka mpaka leo bado tunawakumbuka. Na wote ambao tunawakumbuka leo, walikuwa na sifa moja, walikataa kuishi maisha ambayo kila mtu anaishi.

Walikuwa na ndoto kubwa ambazo kwa wengine zilionekana haziwezekani, lakini wao waliziamini na kuzisimamia mpaka pale walipoweza kuzifikia. Kwa njia hii waliweza kuutumia muda wao mfupi wa hapa duniani vizuri.

Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyaishi maisha yako mafupi uliyonayo hapa duniani, kwa kukataa kuishi kwa mazoea, kwa kuachana kabisa na kufanya kile ambacho kila mtu anafanya na kuchagua kuishi maisha ya ndoto yako.

Unapaswa kuwa na ndoto kubwa ya namna unavyotaka maisha yako yawe na namna unavyoona dunia inaweza kuwa bora zaidi, na kuiishi ndoto hii hata kama hakuna mwingine anayeiamini.

Unapaswa kujiwekea viwango vya juu sana kwenye chochote unachofanya, kukifanya kwa hali ya ubora kabisa kuliko wengine wanavyofanya. Fanya hivi kuanzia namna unaishi maisha yako binafsi, kwenye kazi na biashara yako na hata kwenye mahusiano yako na wengine.

Yafanye maisha yako mafupi hapa duniani yawe ya utofauti mkubwa, ambao utaacha alama ya kipekee hata baada ya wewe kuwa umeshaondoka. Na hili linawezekana kama utakuwa tayari kuishi ndoto kubwa zilizopo ndani yako, maana kila mtu ana ndoto kubwa ndani yake.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha