Unaposikia mtu anasema ningependa kufanya kitu fulani ila sina muda, kuna mambo mawili hapo, labda kitu hicho siyo muhimu au mtu huyo hajui nini muhimu kwenye maisha yake.
Kwa sababu kuja na sababu kwamba huna muda na kuwa tayari kuileza na kuitetea kwa watu kunahitaji muda pia.
Hivyo kwa chochote unachotaka kwenye maisha yako, unaweza kutengeneza muda wa kukifanyia kazi au unaweza kutengeneza sababu kwa nini huna muda. Ni machaguo hayo mawili tu ambayo unayo kwenye ufanyaji wa mambo yako.
Na kwa kuwa kila mtu anaweza kutengeneza sababu, na wachache sana ndiyo wanaoweza kutengeneza muda, ningeshauri ujitoe katika wale watengeneza sababu.
Weka nguvu zako kwenye kutengeneza muda, kama jambo ni muhimu sana kwako basi weka nguvu katika kulifanyia kazi. Na kama jambo siyo muhimu basi achana nalo kabisa, wala usianze kulitafutia sababu kwa nini huwezi kulifanya.
Ni kweli muda wetu ni mfupi, tuna masaa 24 pekee kwa siku na miaka yetu ya kuwa hapa duniani siyo mingi. Hivyo kusema kwamba hujafanya kitu kwa sababu huna muda unakuwa unamaanisha nini hasa, kwamba kuna watu walikuwa wanagawiwa muda wa ziada na wewe ukaukosa?
Au ni jambo la kushangaza kwamba leo umeamka asubuhi na badala ya siku kuwa na masaa 24 imekuwa na masaa 20?
Muda wetu wa siku ni ule ule, haubadiliki, kinachobadilika kwetu ni vipaumbele vyetu. Hivyo kabla hujasema huna muda, unaonaje ukapitia kwanza vipaumbele vyako na kuona kipi muhimu zaidi kwako kufanya na yapi ya kuachana nayo.
Tengeneza muda wa kufanya yale muhimu na usipoteze muda wako kwenye kutengeneza sababu kwa nini huwezi kufanya vitu fulani. Kama siyo muhimu kwako achana navyo, na weka juhudi kwenye yale muhimu zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Safi saana bwana kocha makirita Amani, nikwel kabisa ule muda tunao tumia kutengeneza/ kutafuta sababu, ndio huo huo muda kumbe tunapaswa kuufanyia kazi maana sababu,hazitulipii,kodi,hazitulipii matibabu, hazitutatulii changamoto zetu za maisha, Bali kuturudisha nyuma tuu mafanikio,mimi binafsi nimeamua kwamba pale ntakapo ona nataka kuweka kila aina ya sababu hapo hapo natafuta njia ya kuchukua hatua sahihi ya kuleta matokeo sahihi
LikeLike
Vizuri sana Emanuel kwa maamuzi hayo, yasimamie.
LikeLike