Zama hizi kila kitu kina matoleo mengi sana, na matoleo yanatoka kila baada ya muda mfupi.

Ukinunua simu mpya leo, ambayo ndiyo toleo jipya kabisa, miezi sita ijayo kutakuwa na matoleo mengine mapya ya simu hiyo hiyo kiasi kwamba ile uliyonayo unaanza kuiona kama haifai tena.

Mfumo wa kuja na matoleo mapya na bora kabisa ya simu kila baada ya muda, yamewezesha kampuni za simu kutengeneza faida kubwa.

Hebu fikiria kama kampuni ya simu za iphone ingeishia kwenye toleo la kwanza tu, kila mtu akishakuwa na simu hiyo wasingeweza kuuza zaidi. Lakini kwa kuja na matoleo mapya kila mwaka, hata aliyenunua simu mwaka jana, anapogundua toleo jipya lina uwezo mkubwa kuliko simu aliyonayo yeye, ananunua toleo hilo jipya.

Pia kila mara ambapo toleo jipya la simu linatoka, toleo la zamani linashuka bei.

Haya tunayaona kila siku kwenye ulimwengu wa biashara na kwenye teknolojia, kila siku vitu vinabadilika, na vinabadilika kuwa bora zaidi. Na jinsi matoleo mapya na bora yanatoka, ndivyo bei inakuwa kubwa na watu wanahitaji zaidi kilicho kipya na chenye uwezo mkubwa.

Sasa nataka sisi tutumie dhana hii ya kuja na matoleo mapya ili kuweza kutengeneza soko zaidi la kazi, huduma na biashara tunazofanya.

Tunapaswa kuwa tunajibadili na kuwa toleo jipya kila baada ya muda fulani. Kwa kutumia mfumo huu wa toleo jipya, kila baada ya muda fulani, ambao unauchagua wewe mwenyewe, unabadilika na kuwa mtu mpya kabisa. Unaboresha sana kila ambacho unakifanya.

Kwa kwenda na hili la matoleo, kila wakati unapotoa toleo lako jipya, unakuza zaidi uhitaji wa kile unachofanya na kuwavutia wateja na wahitaji wengi zaidi. Hata wale ambao walishapata huduma kwako, wanapojua umekuja kwa toleo jingine, watataka kuja kupata huduma zilizo bora zaidi.

Usikubali kuendelea kubaki ulivyo na kufanya unachofanya kila siku na miaka yako yote unayofanya hicho unachofanya. Jifunze kwa makampuni ya simu, bila ya matoleo mapya na ya mara kwa mara hakuna biashara kwao.

Hivyo na wewe hakikisha kila wakati unakuja kama toleo jipya, na hapa namaanisha mabadiliko yako wewe kabla hata hujabadili unachofanya. Kazana uwe bora sana kwenye chochote unachofanya ili uweze kuwahudumia watu vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha