“I don’t agree with those who plunge headlong into the middle of the flood and who, accepting a turbulent life, struggle daily in great spirit with difficult circumstances. The wise person will endure that, but won’t choose it—choosing to be at peace, rather than at war.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 28.7

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ; USITAFUTE UGOMVI…
Wapo watu, kwa kujua wana nguvu au wana uwezo fulani, wanakazana kutafuta njia ya kuonesha au kufanya kile wanachojua.
Na katika kutafuta njia hiyo ya kuonekana, hujikuta wanaingia kwenye ugomvi au matatizo ambayo hayakuwa na ulazima kwao kuingia.

Hata kama una nguvu na uwezo mkubwa wa kumshinda yeyote, usikimbilie kutafuta ugomvi, hasa pale unapokuwa hauna maana yoyote zaidi tu ya wewe kutaka kuonekana unaweza kufanya kitu fulani.

Watu wenye hekima hawakimbilii kutafuta na kuingia kwenye ugomvi, hata kama ni kitu kilichopo ndani ya uwezo wao. Wanachagua kuwa kwenye amani kuliko kuwa kwenye vita. Na kama inawabidi kweli kuwa kwenye vita, basi inakuwa ni vita sahihi na yenye maana kubwa kwao na kwa wengine.

Usiwe mtu wa kuibua magomvi na kutokuelewana na wengine kwa mambo madogo madogo kwa sababu tu unaona unaweza kushinda kila ugomvi.
Tunza nguvu zako kwa yale muhimu zaidi kwako, yale yanayokuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutokutafuta ugomvi, siku ya kujiondoa kabisa kwenye hali ya kutaka kuonesha kwamba unajua na unaweza kushinda ugomvi wowote.
#UsitafuteUgomvi, #TunzaNguvuZakoKwaYaliyoMuhimu #PiganiaKilichoMuhimu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha