Mipango ya kutokufanya kitu, huwa inashindwa mara zote, kwa sababu sisi binadamu huwa ni vigumu sana kwetu kukaa bila ya kufanya kitu.

Hivyo unapokuwa unapanga mambo yako, badala ya kupanga nini hutafanya, panga kwanza nini utafanya. Kwenye kila muda wako pangilia nini utafanya na hili litakupa kitu cha kufanyia kazi.

Kama kuna tabia unataka kuiacha, kupanga kutokufanya tabia hiyo ni vigumu kufuata mpango huo, kwa sababu unapokuwa huna kingine cha kufanya, utarudi kufanya tabia hiyo. Lakini kama utapanga tabia nyingine ya kufanya ambayo inachukua nafasi ya tabia unayoacha, itakuwa rahisi kwako kuacha tabia hiyo ya awali.

Tukirudi kwenye nguvu ya fikra zetu, unapopanga kitu ambacho hutaki kufanya, bado unakuwa umekiweka kwenye fikra zako na hivyo fikra zako zinakuletea fursa zaidi za kufanya kitu hicho. Fikra zetu huwa zinatuweka kwenye mazingira ya kile kinachotawala akili zetu kwa muda mrefu.

Hivyo unachotaka kitawale fikra zako siyo kile ambacho hutaki, bali kile ambacho unakitaka. Hivyo kupanga unachotaka kufanya na kuruhusu kitawale fikra zako kunakuweza kwenye nafasi kubwa ya kukifikia.

Panga unachotaka kufanya, na siyo usichotaka kufanya, akili yako yote peleka kwenye unachotaka kufanya na itavuta fursa zaidi za kukuwezesha kupata unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha