Watu wengi wamekuwa wanashindwa kufanikiwa kwenye maisha kwa sababu hawajajua maana ya maisha yao. Wanaendesha maisha yao kwa mazoea, wanarudia yale yale ambayo wanafanya wengine na siku zinaenda lakini hakuna hatua kubwa wanazopiga.
Wengi hawapati nafasi ya kujua maana ya maisha yao kwa sababu jamii imewadanganya kuhusu kutafuta maana ya maisha. Wengi wanatafuta maana ya maisha nje yao, kwenye vitu vya nje au nafasi na hadhi fulani wanazopata.
Wanafikiri labda wakiwa na kiasi fulani cha fedha ndiyo maisha yao yatakuwa na maana. Au wakifikia hadhi fulani ndiyo maisha yao yatakuwa na maana.
Ukweli ni kwamba huwezi kuipata maana ya maisha kutoka nje, badala yake utaipata kutoka ndani yako. Kuipata maana ya maisha yako angalia ndani yako. Angalia vitu ambavyo unaweza kubadili na kuboresha zaidi ndani yako. Kadiri unavyokuwa bora wewe, ndivyo wanaokuzunguka na mazingira yako yanakuwa bora zaidi.
Maisha yako yatakuwa na maana zaidi pale unapochagua kupita njia iliyo ngumu, inayohitaji kujitoa na yenye mateso na kufuata njia hiyo. Utaona maisha yako kuwa na maana pale unapochagua kufanya vitu ambavyo unajua ni muhimu kwako kufanya, ila hujisikii kuvifanya. Na pia hakuna wengine wanaofanya.
Ukiondoka kwenye mazoea, ukiacha kuangalia kila mtu anafanya nini ili na wewe ufanye na ukaanza kuangalia ndani yako na kujua kipi muhimu zaidi kwenye maisha yako, utaipata maana halisi ya maisha yako na kuweza kuiishi. Haitakuwa vitu rahisi kufanya, lakini vitakuwa na maana kubwa na matokeo makubwa pia.
Ishi maana na kusudi kubwa la maisha yako kila siku, na kila siku itakuwa bora sana kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,