“For to be wise is only one thing—to fix our attention on our intelligence, which guides all things everywhere.”
—HERACLITUS, QUOTED IN DIOGENES LAERTIUS
Ni jambo la kushukuru sana kwa nafasi hii nyingine nzuri tuliyoipata leo.
Hatujaipata nafasi hii kwa sababu tuna akili au tu wajanja sana, bali tumeipata kama bahati kwetu.
Na njia pekee ya kuithamini bahati hii ni kuitumia kufanya yale yaliyo bora, na siyo kuipoteza kwa mambo ya hovyo.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari FIKIRI KABLA YA KUTENDA…
Matatizo yote makubwa ambayo umewahi kuyatengeneza kwenye maisha yako, ni matokeo ya kutenda kabla ya kufikiri.
Labda ni mtu alikukasirisha sana na ukaamua kuchukua hatua kumkomesha, kilichotokea ikawa ni umejikomesha mwenyewe.
Au ulikuwa na furaha sana na kuahidi kitu ambacho baadaye kimekuja kuwa mzigo kwako.
Kila unapokimbilia kufanya maamuzi au kuchukua hatua kabla hujafikiri kwa kina, unatengeneza matatizo zaidi.
Na pale hisia zinapokuwa juu, ni wakati ambapo fikra zinakuwa chini sana, na wakati mbovu sana kwako kufanya maamuzi yoyote.
Fikiri kabla ya kutenda, na utapunguza sana sehemu kubwa ya matatizo na changamoto unazopitia kwenye maisha yako.
Jiwekee utaratibu wa kujisubirisha kwanza, kujilazimisha kufikiri kabla ya kukimbilia kujibu au kuchukua hatua.
Na kamwe usisikumwe kujibu au kuchukua hatua kwa sababu umeambiwa au unafikiri usipochukua hatua mara moja basi utakosa kitu kizuri sana.
Hakuna kitu kizuri kinachokosekana kwa kukimbilia kuchukua hatua kabla ya kufikiri.
Jipe muda wa kufikiri na weka akili yako kwenye utulivu na utaiona hatua sahihi ya kuchukua kwako.
Akili yako ina uwezo mkubwa sana wa kukupa majibu sahihi, kama utaitumia vizuri.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufikiri kabla ya kutenda, siku ya kujipa muda wa kutafakari kabla hujajibu au kuchukua hatua.
#FikiriKablaHujatenda, #DhibitiHisiaZako, #TumiaFikraZako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha