“Clear your mind and get a hold on yourself and, as when awakened from sleep and realizing it was only a bad dream upsetting you, wake up and see that what’s there is just like those dreams.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.31
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo,
Ni nafasi nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari NI KAMA NDOTO MBAYA…
Unapoamka asubuhi na kugundua kwamba ulikuwa na ndoto mbaya usiku, hukai na kuanza kuhofia ndoto hiyo, na kufikiri labda imetokea au la. Unajua tu kwamba ilikuwa ndoto mbaya na unaendelea na maisha yako.
Hivi ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu ya kila siku, kuna mambo tunakutana nayo na yanatupa hofu na mashaka, lakini tunaendelea kukaa na hofu hizo kwa muda mrefu sana, kitu ambacho kinatuzuia kupiga hatua zaidi.
Ona kila hofu na mashaka unayokutana nayo kama ndoto mbaya, na achana nazo na endelea na mipango uliyojiwekea.
Hujawahi kuacha kuamka asubuhi kwa sababu usiku ulikuwa na ndoto mbaya na hivyo unaogopa ukiamka utakutana na ndoto hiyo.
Kadhalika usiache kuchukua hatua ulizopanga kwa sababu ya hofu uliyonayo. Chukulia hofu kama ndoto mbaya, kitu kinachopita, kwa sababu hakuna ambacho umewahi kuhofia na kikatokea kama ulivyohofia.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchukulia hofu na wasiwasi kama ndoto mbaya na hivyo kutokukubali ziwe kikwazo kwako.
#HofuKamaNdotoMbaya, #DawaYaHofuNiKuchukuaHatua, #MaishaLazimaYaendelee
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha