Unaomba ushauri utakuwaje mwandishi bora kabla hata hujakaa chini na kuandika. Au utauzaje kitabu chako kwa mafanikio wakati hata hujaandika sentensi moja ya kitabu hicho.
Ni yale yale ya kuomba ushauri wa utafanikiwaje kwenye biashara wakati hujaanza hata biashara yenyewe, na wala huna mpango wa kuanza karibuni. Au kuomba ushauri utafanikiwaje kwenye mahusiano wakati huna hata muda wa kujali kuhusu wengine.
Kubwa kabisa unaomba ushauri utapataje fedha na utajiri wakati haupo tayari kujituma, haupo tayari kufanya kila kinachopaswa kufanya ili upate hata fedha kidogo.
Rafiki, haya yote ni kujipotezea muda wako na kupoteza muda wa wale unaowaomba ushauri. Kuomba ushauri kwa kitu ambacho wewe mwenyewe hujaanza ni kupoteza muda.
Haijalishi utapewa ushauri mzuri kiasi gani, kama kwa sasa hufanyi, hautakuwa na maana, na wala usijidanganye utakuja kuukumbuka utakapoanza kufanya. Nikuhakikishie hilo halitatokea.
Omba ushauri ukiwa tayari unafanya, ukiwa umekwama na hivyo unapopewa ushauri unaufanyia kazi mara moja na hapo ndipo unaona matokeo ya ushauri huo.
Wengi wamekuwa wanafikiri ushauri ni kama muujiza, kwamba kwa kupata ushauri basi utaweza kupata nguvu na hamasa kubwa ya kuanza. Hicho kitu hakipo.
Kama huwezi kukaa chini na kuandika hata makala moja, acha kupoteza muda wako na wa wengine kwa kuomba ushauri utafanikiwaje kwenye uandishi, ushauri unaohitaji kwa hapo ulipo ni mmoja, kwanza andika. Kadhalika kwenye mengine kama kazi, biashara, mahusiano na fedha.
Usiombe ushauri utapataje fedha na utajiri wakati umekaa tu, huna chochote unachofanya cha kukuingizia kipato. Ondoka hapo ulipokaa kwanza, anza kufanya chochote kitakachokuingizia kipato na hapo ukipata ushauri utaweza kuiga hatua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,