#TANO ZA JUMA #7 2019; Lengo Kuu Ni Furaha, Jinsi Ya Kufikia Ufanisi Mkubwa Kwenye Unachofanya, Hatua Nane Za Kufurahia Chochote Unachofanya, Utajiri Kama Lengo Kuu Kwenye Maisha Na Dhibiti Taarifa Zinazoingia Kwenye Akili Yako.
Karibu sana mwanamafanikio kwenye tano za juma la 7 la mwaka huu 2018.
Ni imani yangu limekuwa juma bora kabisa kwako na umeweza kupiga hatua katika kuelekea kwenye mafanikio makubwa ya maisha yako.
Katika tano za juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa Flow: The Psychology of Optimal Experience kilichoandikwa na mwanasaikolojia Mihaly Csikszentmihalyi.
Kitabu hichi kinatufundisha jinsi ambavyo tunaweza kufikia ufanisi mkubwa na furaha kwenye chochote ambacho tunafanya, iwe kikubwa au kidogo, tunakipenda au hatukipendi.
Karibu tujifunze na tuondoke na mambo ya kufanyia kazi kwenye maisha na kazi zetu ili tuweze kupiga hatua zaidi.
#1 NENO LA JUMA; LENGO KUU NI FURAHA.
Miaka 2300 iliyopita, mwanafalsafa Aristotle alijumuisha kwamba watu wanatafuta furaha kuliko kitu kingine chochote. Kwamba lengo kuu la kila ambacho tunafanya kwenye maisha yetu, ni kutegemea kupata furaha mwishoni.
Na hili ndiyo linawasukuma watu kuchukua hatua mbalimbali, kuanzia kuboresha afya zetu, kuboresha mwonekano wetu, kupata fedha na hata madaraka ni kwa lengo la kutengeneza furaha kwenye maisha.
Lakini sasa tunapofanya furaha kuwa lengo la mwisho, hapo ndipo tunapojiangusha. Kwa sababu wengi wanafika mwisho wa kile walichofikiri kitawapa furaha, lakini hawapati furaha ambayo walifikiria wangeipata.
Hivyo njia bora ya kuipata furaha, siyo kusubiri mpaka mwisho wa kile tunachofanya, bali kutengeneza furaha wakati unakifanya.
Kama unataka furaha ya kweli kwenye maisha, basi usisubiri mpaka mwisho wa kile kitu unachofanya ndiyo uwe na furaha, badala yake tengeneza furaha kwenye kila hatua unayopiga. Furaha inapaswa kuwa matokeo ya kile unachofanya kila siku, na siyo kusubiri mpaka ufike mwisho.
Na hili ndiyo tunakwenda kujifunza kwa kina kwenye kitabu cha juma hili.
Tafiti zinaonesha kwamba furaha siyo kitu kinachotokea kwa bahati na wala siyo kitu ambacho fedha inaweza kununua au madaraka kulazimisha. Furaha haitegemei matokeo ya nje badala yake inategemea jini tunavyotafsiri yale yanayotokea.
Furaha ni hali ambayo inapaswa kuandaliwa, kutengenezwa na kulindwa na kila mtu, kwa kuwa na tafsiri sahihi ya kila kinachoendelea kwenye maisha yako.
Ni kwa kujihusisha moja kwa moja na kila kinachoendelea kwenye maisha yako, kiwe kizuri au kibaya ndiyo tunapata furaha. Siyo kwa kukimbia au kutoroka yale yanayotokea au kujaribu kuikimbiza furaha, bali kuyaishi maisha yako kwa namna yalivyo, ndiko kunakokuletea furaha.
Hivyo jibu fupi la kuwa na furaha kwenye maisha yako ni kujihusisha moja kwa moja na maisha yako na kupokea kila kinachokuja kwako, iwe kizuri au kibaya.
#2 KITABU CHA JUMA; JINSI YA KUFIKIA UFANISI MKUBWA KWENYE UNACHOFANYA.
Rafiki, kama nilivyokushirikisha kwenye utangulizi hapo juu, juma hili tunakwenda kujifunza kutoka kwenye kitabu kinachoitwa Flow: The Psychology of Optimal Experience. Hiki ni kitabu ambacho kimetokana na tafiti za kisayansi, kisaikolojia na kijamii ambazo zimeangalia ni jinsi gani watu wanaweza kuwa na ufanisi mkubwa kwenye kile wanachofanya na pia kuwa na furaha ya kudumu.
Kitabu hiki kimeangalia kwa kina kila eneo la maisha yetu na kila ambacho tunafanya kwenye maisha yetu ya kila siku, kuanzia kazi, kula, kupumzika, kufanya mapenzi na mengine madogo madogo na kuona jinsi tunavyoweza kuyafanya kwa ufanisi mkubwa na kuwa na furaha kubwa kwenye maisha yetu.
Mwandishi anaelezea FLOW kama hali ambapo mawazo na fikra za mtu zinakuwa kwenye kile kitu anachofanya, na hakuna kingine chochote kinachomsumbua kwa wakati huo. Katika hali hii ya FLOW, dhana ya muda inakuwa imepotea kabisa na umakini wa mtu unakuwa umewekwa kwenye kile anachofanya pekee.
Mtu anapokuwa kwenye FLOW ni kama dunia nzima inakuwa haipo kabisa kwenye fikra zake, kinachomsumbua ni kile anachofanya pekee na hivyo anakuwa na ufanisi mkubwa sana kwenye kile ambacho mtu anafanya.
Mwandishi anatuambia FLOW ni hali ambayo inaweza kutengenezwa kwenye kitu chochote ambacho mtu unakifanya na hilo likaongeza ufanisi mkubwa kwenye chochote mtu anafanya pamoja na furaha. Kwa mfano chanzo kikuu cha wasiwasi na kukosa furaha ni pale mtu anapokuwa anafanya kitu kimoja, lakini mawazo yake yapo kwenye vitu vingine. Lakini pale mawazo yanakuwa kwenye kile unachofanya, hali ya wasiwasi inapotea kabisa na ufanisi na furaha vinakuwa juu kabisa.
Yafuatayo ni mambo muhimu sana ya kujifunza na kufanyia kazi kwenye maisha yetu kutoka kwenye kitabu hiki cha FLOW.
MOJA; TUIANGALIE FURAHA UPYA.
Furaha ni dhana ambayo wengi tumekuwa tunaikosea, tunafikiri ni kitu cha kutafuta, kitu ambacho tunaweza kukifanyia kazi na kukipata. Lakini ukweli ni kwamba furaha haitafutwi, furaha siyo kitu unachoweza kukifanyia kazi kukipata, bali furaha ni matokeo ya namna tunavyoyaishi maisha yetu, tunavyofanya mambo yetu na tunavyopokea na kuchukulia kila kinachotokea kwenye maisha yetu.
- Furaha ni matokeo ya mtu kuwa kwenye hali ya FLOW, pale ambapo mawazo na fikra za mtu zinakuwa kwenye kile anachofanya na hakuna kingine kinachokuwa na umuhimu kwake kwa wakati huo. Pale ambapo mtu anafanya kitu kwa kuwa anataka kukifanya na siyo kwa sababu nyingine yoyote ile. Hapa ndipo furaha inapotoka, mtu anapokuwa amejipoteza kwenye kile anachofanya.
- Furaha imekuwa kitu kigumu kwa wengi kufikia kwa sababu hatujui msingi muhimu wa furaha. Tunafikiri ya kwamba dunia ipo kwa ajili ya kutupa sisi furaha, lakini ukweli ni kwamba dunia haijatengenezwa kwa lengo la kutupa sisi furaha. Dunia ipo na inajiendesha kwa misingi yake yenyewe, mtu usipojua misingi hii utaishia kuiona dunia kama sehemu mbaya na isiyo na usawa. Lakini unapoielewa misingi ya dunia na kuiishi, unaelewa kwamba dunia haijali sana kuhusu uwepo wako wala uhitaji wako wa furaha.
- Jinsi tunavyojisikia na furaha na raha tunayoipata kwenye maisha ni matokeo ya namna tunavyochuja yale tunayokutana nayo kila siku. Furaha inategemea zaidi utulivu wetu wa ndani badala ya kutegemea kuidhibiti dunia na kuifanya iende kama tunavyotaka sisi wenyewe. Hivyo kuweza kudhibiti nafsi zetu ni hitaji muhimu la kuwa na furaha kwenye maisha yetu.
- Changamoto nyingine kubwa kwenye furaha ni malengo ambayo tunayo. Wengi wamekuwa na malengo madogo, ya kutaka kuwa na maisha yenye usalama, lakini wanapofikia malengo hayo, wanaona kama kuna kitu bado kinakosekana na hali hiyo inawanyima furaha. Kwa upande wa pili, wapo wanaokuwa na malengo makubwa ambayo wakishindwa kuyafikia wanajisikia vibaya na hivyo kukosa furaha. Na pia wapo ambao wanakuwa na malengo madogo, wakiyafikia wanaweka malengo mengine na hivyo muda wote wanakuwa wanafanyia kazi malengo makubwa zaidi. Yote haya kuhusu malengo yanaathiri hali ya furaha pale ambapo mtu anakuwa anategemea akikamilisha malengo yake basi awe na furaha.
- Mifumo ya kijamii imekuwa sehemu ya kuwaondoa watu kwenye hali ya kukoa furaha. Mifumo hii ambayo imekuwa inafanya kazi kwa zawadi na adhabu imekuwa inaahidi zawadi pale mtu anapofanya vizuri na adhabu pale mtu anapofanya vibaya. Mfano wa mifumo hii ni dini, siasa, taasisi mbalimbali na hata biashara kubwa. Mifumo hii iliweza kuwa udhibiti kwa wengi kipindi cha nyuma, lakini kwa sasa inakosa nguvu. Hivyo njia pekee ya mtu kuondoka kwenye hali ya kukosa furaha ni kuweza kujidhibiti yeye mwenyewe, kuweza kutengeneza mfumo wake wa zawadi na adhabu kupitia kila anachofanya.
- Njia pekee ya kuelekea kwenye uhuru na furaha ni kujijua wewe mwenyewe na kuweza kujidhibiti mwenyewe. Kuondokana na tamaa za mwili na kuachana na mifumo ya kijamii ambayo inatumia tamaa za mwili kuwadhibiti watu. Kuwa huru kifikra na kuchagua kufanya kile ambacho ni muhimu na siyo kinacholeta raha. Ili kupata furaha ya muda mrefu, lazima uwe tayari kuahirisha raha ya muda mfupi. Kushindwa kuahirisha raha kumekuwa chanzo cha wengi kuingia kwenye matatizo na kukosa furaha
MBILI; KUHUSU UFAHAMU.
Ufahamu wetu ni ndiyo kitu pekee kinachotutofautisha na wanyama wengine. Sisi binadamu tupo juu ya viumbe wengine wote kwa sababu tuna ufahamu wa juu. Hatuchukui tu hatua kwa msukumo wa mwili, badala yake tunatumia akili zetu kufikiri na hapo tunaweza kupata hatua na njia bora ya kuchukua. Furaha ni zao la jinsi tunavyoweza kutumia na kudhibiti ufahamu wetu.
- Kazi ya ufahamu ni kuchukua taarifa kutoka kwenye mazingira yetu, kuzichakata na kuupa mwili hatua za kuchukua. Kwa kutumia ufahamu wetu tunaweza kuchuja kila aina ya taarifa inayoingia kupitia milango yetu ya fahamu na kuchagua hatua sahihi kuchukua. Wanyama wengine hawana uwezo huu, wao wanapopata taarifa wanachukua hatua mara moja bila ya kufikiri.
- Mtu anaweza kujitengeneza na kuwa na furaha au kukosa furaha bila ya kutegemea kinachotokea nje yake. Ni namna ambavyo ufahamu wake unavyopokea yale yanayotokea ndiyo kunaamua kama mtu atakuwa na furaha au atakosa furaha. Ndiyo maana katika hali moja, kuna mtu anaweza kuwa na furaha na mwingine kwenye hali hiyo hiyo akakosa furaha, kinachowatofautisha siyo kinachotokea, bali jinsi wanavyopokea kinachotokea kwenye ufahamu wao.
- Umakini wetu ndiyo nguvu kuu ya ufahamu wetu. Pale ambapo fikra zetu zote zinakuwa kwenye kitu kimoja, umakini wetu unakuwa pale na tunakuwa na nguvu kubwa ya ufahamu katika kufanya kitu hicho. Kadiri tunavyoweza kudhibiti umakini wetu kwenye kile tunachofanya, ndivyo ufanisi wetu unavyokuwa mkubwa na furaha kuwa kubwa pia. Kwa sababu nguvu yetu ya ufahamu ina ukomo, tusipoidhibiti na kuiachia isambae kwenye kila kinachojitokeza, hakuna tutakachoweza kukamilisha.
- Kipimo cha udhibiti ambao mtu anao kwenye ufahamu wake ni namna anavyoweza kudhibiti umakini wake, jinsi anavyoweza kuweka umakini wake kwenye kitu kimoja na kuepuka usumbufu wa aina nyingine yoyote. Mtu anayeweza kufanya hivi kwa chochote anachochagua, anakuwa na ufanisi mkubwa na furaha pia.
- Nafsi ni matokeo ya jinsi ambavyo umakini wa mtu umetumika. Nafsi ni mkusanyiko wa kila kinachotokea kwenye maisha ya mtu, na kwa kuwa umakini wetu ndiyo unachagua nini kitokee, basi umakini ndiyo unatengeneza nafasi, na baadaye nafsi hii inadhibiti na kuongoza umakini wetu pia. Hivyo nafsi na umakini ni vitu ambavyo vinategemeana sana.
- Pale ambapo fikra zinakuwa tofauti na kile ambacho mtu anafanya, inaleta mvurugano kwenye ufahamu na kuibua hisia ambazo siyo nzuri. Hisia za hofu, hasira, wasiwasi, maumivu na hata wivu ni matokeo ya mtu kuwa unafanya kitu hiki lakini fikra zako zipo kwenye kitu kingine. Mtu unaposhindwa kudhibiti umakini wako kwa kuweka fikra zako kwenye kile unachofanya, nafsi inavurugika na huwezi kuwa na ufanisi au furaha kwenye kile unachofanya.
- Flow ni mpangilio mzuri kwenye ufahamu, pale ambapo umakini unakuwa umedhibitiwa na fikra za mtu zipo kwenye kile ambacho anakifanya. Pale fikra na umakini wa mtu unakuwa kwenye kile anachofanya pekee, hisia za hofu, hasira, wasiwasi na hata wivu hazipati nafasi kabisa kwenye ufahamu wake. Hapa ufanisi wa mtu unakuwa mkubwa sana na furaha inakuwa ni matokeo ya mtu kuwa kwenye hali hiyo.
- Pale ambapo mtu anaweza kudhibiti na kupangilia ufahamu wake, kwa kuweza kuchagua kuweka umakini wake kwenye kile anachofanya na kuachana na mengine yote, ufanisi wake unakuwa mkubwa, maisha yake yanakuwa bora na anakuwa na furaha muda wote, bila ya kujali nini kinatokea kwenye mazingira yake. Hivyo tumeshaipata siri kuu ya kuwa na ufanisi mkubwa na furaha kwenye maisha, kudhibiti ufahamu wetu kwa kuweka umakini wetu kwenye kile tunachofanya na kusahau mengine yote.
TATU; STAREHE NA UBORA WA MAISHA.
Kuna nia mbili ambazo tunaweza kutumia kuimarisha ubora wa maisha yetu. Njia ya kwanza ni kuyafanya mazingira yaendane na malengo yetu, hapa mtu unakazana kuibadili dunia iwe kama unavyotaka wewe, kitu ambacho ni kigumu sana. Njia ya pili ni kubadili malengo yetu yaendane na jinsi dunia inavyoenda. Hili pia ni gumu kwa sababu siyo mara zote unaweza kwenda kama dunia inavyokwenda. Hivyo tunajifunza kwamba ubora wa maisha ni matokeo ya jinsi tunavyoweza kuwa na mlinganyo sahihi kwenye maeneo hayo mawili, kuibadili dunia na kubadilika sisi wenyewe.
- Raha na starehe ni vitu ambavyo watu wamekuwa wanavichanganya na hivyo kushindwa kuyafanya maisha yao kuwa bora. Raha ni ile furaha ya muda mfupi ambayo mtu unaipata kutokana na hisia ambazo zimeibuka ndani yako. Mara nyingi raha haikuhitaji utumie nguvu au ujuzi wako kuipata, kwa mfano kuangalia tv kunaleta raha kwa wengi. Kwa upande wa pili, starehe ni furaha ambayo inatokana na juhudi ambazo mtu ameweka kwenye kitu. Kwa mfano michezo mbalimbali inaleta furaha, lakini ili ufurahie michezo hiyo lazima uweke juhudi, hivyo ndivyo starehe ilivyo, lazima uweke juhudi kuipata.
- Kinacholeta flow na furaha kwenye maisha ni pale mtu anapofanya kitu ambacho kinatumia juhudi zake na kinaleta matokeo mazuri kwake. Kwa kifupi hapa ni sawa na kusema mtu anakuwa na starehe kwenye kile anachofanya. Japokuwa hali ya FLOW inaweza kuonekana kama rahisi, lakini inahitaji mtu kuweka juhudi na hasa udhibiti kuwa mkubwa sana kwenye ufahamu na umakini.
- Kuweka nguvu zako zote na fikra zako kwenye kile unachofanya ni hitaji muhimu sana la kufikia hali ya FLOW na kuwa na ufanisi mkubwa pamoja na furaha. Kufikiria kile tu ambacho mtu unafanya na kusahau mengine yote ndiyo kunakuleta ufanisi mkubwa kwenye ufanyaji wa kitu. Katika hali ya flow, hupati nafasi ya kujiuliza kwa nini unafanya au kama unafanya kwa usahihi, wewe mkazo wako unakuwa ni kufanya, na unafanya kwa sababu ya kufanya na siyo kutegemea kupata kitu chochote katika ufanyaji huo. Kwenye flow, mfanyaji unakuwa kitu kimoja na kile unachofanya, na hili ndiyo linaleta matokeo makubwa sana.
- Hali ya flow ina nguvu kubwa na kama nguvu hii isipotumika vizuri inaweza kuwa na madhara makubwa sana kwa mtu. Nguvu ya flow ni kama moto, moto ni mzuri sana ukidhibitiwa, lakini ni mbaya kama hautadhibitiwa. Iwapo mtu ataweka hali ya flow kwenye mambo mabaya, basi ubaya wake utakuwa mkubwa na wenye madhara makubwa kwake na kwa wengine.
NNE; HALI ZINAZOATHIRI FLOW.
Ili kufikia flow kwenye chochote ambacho mtu unafanya, lazima uwe na lengo la kile unachofanya, na pia uwe na ujuzi na kuzijua sheria za kitu hicho. Lazima uwe na mejesho wa namna unavyofanya pamoja na kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya. Katika hali ya flow, dhana ya muda kwako inafutika kabisa.
Zipo hali ambazo zinaathiri uwezo wetu wa kufika kwenye flow kupitia chochote tunachofanya;
- Hali ya kwanza ni kushindwa kuidhibiti nafsi na hivyo umakini kukosekana, hapa mtu unaruhusu umakini wako kuzurura kwenye mambo mengi kwa wakati mmoja kitu ambacho kinapunguza nguvu ya ufahamu na kushindwa kuweka umakini wako wote kwenye kitu kimoja. Mtu ambaye hawezi kujidhibiti na kuweka umakini wake wote kwenye kile anachofanya, hawezi kufikia hali ya flow.
- Hali ya pili ni kuwa na udhibiti mkali sana kwenye nafsi kiasi kwamba umakini unakuwa kiasi cha mtu kushindwa kuchukua hatua. Hapa udhibiti unakuwa umepitiliza kiasi kwamba mtu anashindwa kuchukua hatua kama kuna kitu fulani hakijakamilika kama anavyotaka. Ili kufikia hali ya flow, lazima tuweze kuwa na mlinganyo kwenye hali hizi mbili, tuepuke kukosa kabisa udhibiti wa nafsi na pia tuepuke kuidhibiti nafsi kupitiliza.
TANO; MWILI KATIKA HALI YA FLOW.
Tunapokuwa hatuna furaha, tunapokuwa na sonona au kuchoka tuna suluhisho rahisi kuchukua; kutumia mwili wetu kwa vyote ulivyo navyo. Mwili wetu ni hazina kubwa sana kwetu, una vitu vingi tunavyoweza kufanya ambavyo vinatupeleka kwenye hali ya flow na kuyafanya maisha yetu kuwa bora na ya furaha. Miili yetu inaweza kufanya mambo mengi sana, kuona, kusikia, kushika, kukimbia, kuogelea, kurusha vitu, kukamata vitu, kupanda milima na mengine mengi. Mambo yote haya ambayo miili yetu inaweza kufanya tunaweza kuyatumia kwenye hali ya flow.
- Mazoezi ya mwili kama kukimbia, kupanda milima, kuogelea na mengineyo ni sehemu nzuri ya kuzalisha hali ya flow pale ambapo mtu anayafanya kwa umakini mkubwa. Pale mtu unapoweka fikra zako zote kwenye zoezi unalofanya, unaweza kufanya kwa ukubwa zaidi, kwa ubora kuliko mwanzo na hata kwa uimara zaidi. Hivyo kuweka hali ya flow kwenye mazoezi kunatufanya kuwa bora zaidi.
- Ufanyaji wa mapenzi pia unaweza kuwekwa kwenye hali ya flow, pale ambapo mtu unaweka umakini wako wote kwa mpenzi au mwenza ambaye unakuwa naye na kuacha kufikiria mambo mengine. Ufanyaji wa mapenzi umekuwa unatumika kama sehemu ya kupata raha pekee, na hii ndiyo imekuwa inawasukuma wengi kuwa na wapenzi wengi. Lakini unapoyatumia mapenzi kama kitu cha kuzalisha hali ya flow, unagundua unapaswa kuuweka umakini wako kwa mtu mmoja, na hili linaimarisha sana mahusiano yenu na kuyafanya maisha kuwa bora na tulivu, na yanayofurahiwa pia.
- Mazoezi ya umakini na usawa kama yoga nayo yanaweza kutumika kama flow. Katika ufanyaji wa mazoezi haya, lazima umakini wa mtu uwe kwenye kile anachofanya na asahau mengine yote. Pia ufanyaji wa tahajudi ni sehemu nzuri ya kuwa na flow kwa sababu fikra zako zote zinaelekezwa kwenye kitu kimoja na kusahau mengine yote.
- Muziki pia ni sehemu nzuri ya kuuwezesha mwili kufika kwenye hali ya flow. Na hili linapatikana katika pande zote mbili. Upande wa kwanza ni kusikiliza muziki, hapa mtu anaweka umakini wake wote kusikiliza muziki, hasa pale anapokuwa ameupenda na umeshika hisia zake. Upande wa pili ni kutengeneza muziki, hili pia linahitaji umakini wa hali ya juu na utulivu ambao unazalisha hali ya flow. Wapigaji wa vyombo mbalimbali vya muziki huwa wanaweka umakini mkubwa kwenye kupiga vyombo hivyo kiasi cha kutokuruhusu kabisa usumbufu wa aina nyingine yoyote kuwaingia wakati wakipiga vyombo vyao. Hili linazalisha muziki ambao ni mzuri sana.
- Kula pia ni kitu kinachoweza kuzalisha flow, na pale ambapo mtu unaweka umakini wako wote kwenye kula, unapata ladha nzuri sana ya chakula hicho, hata kama ni chakula cha kawaida. Huwa tumezoea kuchukulia kula kama kitu cha kumaliza kufanya haraka ili tuendelee na mambo mengine. Lakini kama utaanza kuweka hali ya flow kwenye zoezi la ulaji, utaweza kufurahia sana ulaji wako na kuwa na utulivu mkubwa kwenye maisha yako.
Kama ambavyo dini na falsafa nyingi zinasema mwili ni hekalu la Mungu, kama tukiweza kuitumia miili yetu vizuri, tukaweka umakini kwa chochote tunachofanya, tutaweza kufanya kwa ubora wa hali ya juu, tukawa na utulivu mkubwa na kupata furaha kubwa sana katika kufanya.
SITA; FLOW KATIKA KUFIKIRI.
Vitu vizuri kwenye maisha havitokani na mwili pekee, bali fikra zetu zinaweza kutuletea vitu vizuri sana kwenye maisha yetu. Baadhi ya hali bora kabisa tunazopitia kwenye maisha yetu ni matokeo ya kinachoendelea kwenye fikra zetu. Hivyo tunaweza kuzalisha flow kupitia kufikiri kwetu.
- Mwili na akili vinashirikiana, mambo yote ambayo tumeona mwili inaweza kuyafurahia tunapoyafanya kwa hali ya flow, siyo mwili pekee ambao unazalisha hali hiyo, bali akili inahusika sana. Lazima mtu uweze kudhibiti akili yako ndiyo uweze kufurahia mazoezi, chakula, mapenzi, muziki na kadhalika. Hivyo akili na fikra zetu zina mchango mkubwa sana kwetu kuweza kufikia hali ya flow.
- Kumbukumbu ni moja ya njia za kutumia akili kama sehemu ya kutengeneza flow. Mtu anayeweza kukumbuka hadithi mbalimbali, kukumbuka mashairi au mistari ya nyimbo mbalimbali, kukumbuka kanuni za hesabu na sayansi, anakuwa katika nafasi nzuri ya kufurahia maisha yake kuliko ambaye hawezi kuwa na kumbukumbu nzuri. Kwa mfano mtu anapojikuta kwenye hali ambayo hana cha kufanya, mwenye kumbukumbu nzuri anaweza kupata hali ya flow kwa kuzipitia kumbukumbu alizonazo. Hivyo kujijengea kumbukumbu nzuri ni hitaji muhimu la kufikia hali ya flow.
- Sayansi na falsafa ni maeneo mengi ambapo tunaweza kutengeneza flow kwa kupitia akili na fikra zetu. Pale tunapoweka fikra zetu zote katika kufikiria jambo la kisayansi au katika kutafakari falsafa, tunajitoa kwenye mengine yote na kuweka umakini wetu kwenye kile tunachofanya. Na siyo lazima uwe mwanasayansi mkubwa au mwanafalsafa ili kuweza kutengeneza flow kwenye maeneo hayo. Kitendo cha kuchagua kuweka umakini wako katika kufuatilia, kinatosha kuzalisha hali ya flow.
SABA; KAZI KAMA FLOW.
Sehemu kubwa ya maisha yetu tunaitumia kwenye kufanya kazi ili kuwezesha maisha yetu kwenda. Hakuna njia ya mkato katika kupata mahitaji ya maisha, lazima tutumie nguvu na muda katika kufanya kazi ndiyo tuweze kutimiza mahitaji ya maisha yetu. Kazi ni moja ya vitu ambavyo vinaonekana kama adhabu na wengi hawapendi kufanya. Lakini kazi ni moja ya vitu ambavyo tukibadili mtazamo wetu tunaweza kunufaika nayo sana. Kazi inaweza kuzalisha flow kwenye maisha yako na kuyafanya kuwa bora sana.
- Ili kufikia flow kwenye kazi unayoifanya kwanza kabisa lazima uipende na kuweka umakini wako wote katika kuifanya. Lazima uichukulie kazi hiyo kuwa ndiyo kipaumbele pekee kwako wakati unaifanya. Kwa kuweka umakini huu, kazi yoyote itazalisha hali ya flow, hata kama ni kazi ya kawaida sana.
- Ili kazi iwe bora na ya kufurahia, lazima mfanyaji uwe na uhuru kwenye kazi hiyo, uifanye kwa sababu umechagua kuifanya na ni muhimu kwako na siyo kwa sababu umelazimishwa kuifanya au huna namna bali lazima uifanye.
- Kazi yoyote ile inaweza kuzalisha flow kama itafuata hali zinazoleta flow, lazima mtu uwe na lengo la kukamilisha kwenye kazi yako, lazima uwe na ujuzi unaoendana na kazi unayofanya, lazima uwe na njia ya kupima ufanisi wako, na uweze kuweka umakini wako wote katika kufanya majukumu yako ya kazi.
NANE; KUFURAHIA UKWEPE NA KUWA NA WATU WENGINE.
Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, huwa tunajisikia vizuri pale tunapokuwa ndani ya jamii, tunapojihusisha na wengine. Hali ya upweke huwa tunakazana kuikimbia kwenye maisha yetu. Lakini ili kuwa na maisha bora, huwezi kujichanganya na wengine mara zote, unahitaji kuwa na muda wako peke yako. Maisha bora ni jinsi unavyoweza kuwa na mlinganyo kati ya muda wa kuwa na wewe peke yako na muda wa kuwa na wengine.
- Watu wengine wanaweza kuwa chanzo cha furaha kwetu au matatizo makubwa kwetu. Jinsi ambavyo wengine wanaathiri maisha yetu kunaanza na jinsi ambavyo tunapokea yale wanayofanya kwenye maisha yao na yetu pia. Unapotaka kila mtu afanye kama unavyotaka wewe, watu wengine wanakuwa tatizo kubwa kwako. Lakini pale unapowaacha wengine wafanye wanavyofanya na kuchukua yale yenye maana kwako maisha yako na mahusiano yanakuwa bora.
- Tunaogopa upweke kwa sababu katika hali ya upweke na tunapokuwa hatuna cha kufanya akili zetu huanza kufikiria yale mambo ambayo tunahofia. Ni rahisi kwa akili kwenda kwenye fikra hasi kama hajatingwa na jambo lolote muhimu. Kwa kuwa watu hawapendi fikra hizo hasi na kwa kuwa wanakuwa hawana mengine ya kufikiria, watu hukazana kuwa na wengine mara zote na pale ambapo haiwezekani basi hutafuta kitu cha kuwasumbua kama kuangalia tv au kutembelea mitandao ya kijamii.
- Upweke ni hitaji muhimu sana kwenye ukuaji wa nafsi na hata kuweza kujidhibiti. Ili uweze kufurahia upweke na hata kupata flow kwenye upweke, unapaswa kuwa na lengo ambalo unalifanyia kazi kwenye upweke wako. Usiruhusu akili yako izurure tu inavyotaka yenyewe, badala yake kuwa na vitu ambavyo unapanga kuvitafakari kwa kina pale unapokuwa mwenyewe. Kwa hali hii utaufurahia sana upweke na kuweza kupata majibu ya mengi yanayohusu maisha yako.
TISA; KUYATOROKA MACHAFUKO KWENYE MAISHA.
Maisha huwa hayaendi kama tunavyopanga sisi, kwenye maisha huwa kuna mambo yanayotokea tofauti kabisa na tulivyopanga, hii ni hali ya machafuko kwenye ufahamu na nafsi zetu. Katika hali hii ya machafuko, wapo watu ambao wanakata tamaa na kukubali maisha yao yaharibike kabisa, lakini pia wapo ambao wanakuwa imara zaidi na maisha yao kuwa bora baada ya machafuko. Kwa mfano wapo watu ambao wamekuwa na maisha bora baada ya kupoteza viungo vya miili yao kama miguu, mikono, macho na kadhalika. Baada ya kukutana na hali zilizowapelekea kukosa viungo hivyo, inakuwa kama ndiyo wamefunuliwa umuhimu wa kuyaishi maisha yao.
Njia pekee tunayoweza kuitumia kuyatoroka machafuko kwenye maisha ni kuyatumia kutufanya kuwa bora zaidi. Pale ambapo jambo ambalo hukulitegemea limetokea, usikubali likurudishe nyuma wala kukukatisha tamaa, badala yake litumie kupiga hatua zaidi. Na kwa kila jambo, hata liwe baya kiasi gani, kuna namna unaweza kulitumia vizuri na ukapiga hatua zaidi.
KUMI; KUTENGENEZA MAANA KWENYE MAISHA.
Lengo kuu la kutengeneza hali ya flow kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yetu siyo tu kupata furaha wakati tunafanya mambo hayo, bali kutengeneza maana kubwa ya maisha yetu. Haitoshi tu kujidhibiti nafsi yako na kuweka umakini kwenye kile unachofanya, mwisho wa siku lazima kuwe na maana ya maisha yako. Lazima uwe na sababu kubwa inayokusukuma kuendelea kujidhibiti na kutumia umakini wako vizuri.
Kutengeneza maana kwenye maisha ni matokeo ya kutengeneza utaratibu kwenye ufahamu wako. Kuyaelekeza yale yote unayofanya katika kuzalisha hali ambayo inayafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Zipo hatua tatu muhimu za kukuwezesha kutengeneza maana ya maisha yako.
- Moja unapaswa kuwa na kusudi la maisha yako, unapaswa kuwa na kitu ambacho kinakusukuma kuweka juhudi zaidi kwenye yale unayofanya kwenye maisha yako. Kusudi lako la maisha ndiyo linalokusukuma kuweka umakini wako kwenye yale unayofanya na hata kujituma zaidi pale unapojisikia kukata tamaa. Kusudi la maisha ndiyo linalokuwezesha kuvuka vikwazo na magumu mbalimbali unayokutana nayo.
- Mbili ni kuwa na malengo ambayo yanakufikisha kwenye kusudi la maisha yako. Kusudi lako halitafikiwa kama ajali, lazima ukae chini uweke malengo na mipango itakayokuwezesha kufikia kusudi hilo. Malengo yako ndiyo yanayoamua wapi uweke umakini wako na jinsi gani utumie nguvu za ufahamu wako. Bila ya malengo utatawanya vibaya nguvu zako za ufahamu, utachoka huku ukiwa hakuna kubwa ulilofanya. Malengo ndiyo yanayotuweka kwenye mstari wa kulifikia kusudi la maisha yetu.
- Tatu ni kuwa na maelewano kati ya kusudi na malengo, hili ndiyo muhimu sana kwa sababu bila ya maelewano mazuri baina ya kusudi lako na malengo unayoweka, hutaweza kupiga hatua. Lazima kila unachofanya kiwe kinachangia kwenye kufikia kusudi lako, na fikra zako ziwe kwenye unachofanya. Kama unafanya kitu kimoja huku mawazo yako yapo kwenye kitu kingine, kama ukianza kufanya kile ulichopanga unafikiria kufanya kingine tofauti, utaiweka nafsi na ufahamu wako katika hali ya machafuko na utatumia nguvu nyingi kwenye machafuko hayo kuliko kwenye kuchukua hatua. Maelewano baina ya kusudi na malengo yanaleta utulivu wa nafsi na ufahamu na hili linakuweka kwenye hali ya flow, maisha yako yote yanakuwa kwenye flow na hapo unakuwa na maisha bora na yenye furaha ya kudumu. Kila unachofanya lazima uweze kukielezea kinachangiaje kwenye malengo na kusudi la maisha yako.
Rafiki yangu mpendwa, FLOW ni moja ya vitabu vinavyotupa nafasi ya kujitathmini kwa kina, kuangalia kila tunachofanya kwenye maisha yetu na kuona ni kwa namna gani tunaweza kuwa bora zaidi. Kupitia uchambuzi huu kuna mengi mno ambayo nimekushirikisha, ambayo ukiyafanyia kazi tu hutabaki hapo ulipo sasa. Nenda kafanyie kazi haya uliyojifunza, kuwa na udhibiti kwenye nafsi na ufahamu wako na ishi kusudi la maisha yako.
#3 MAKALA YA JUMA; HATUA NANE ZA KUFURAHIA CHOCHOTE UNACHOFANYA.
Rafiki, wapo watu ambao wanafanya kazi ambazo kwa nje zinaonekana ni za hovyo na hazina maana, lakini wanazifurahia sana. Lakini pia wapo watu ambao wanafanya kazi ambazo kwa nje zinaonekana ni bora sana lakini wao binafsi hawazifurahii. Hii ni hali ambayo imekuwa inawashangaza wengi, na kushindwa kuielewa.
Katika kitabu cha juma hili, tunajifunza hatua nane za kufurahia chochote ambacho unakifanya na kuyawezesha maisha yako kuwa bora sana.
Makala ya juma hili imezijadili hatua hizo nane na jinsi unavyoweza kuziweka kwenye chochote unachofanya kwenye maisha yako.
Kama hujasoma makala hiyo, isome sasa hapa; Hatua Nane (08) Zitakazokuwezesha Ufurahie Chochote Unachofanya Na Kuwa Na Furaha Kwenye Maisha. (https://amkamtanzania.com/2019/02/15/hatua-nane-08-zitakazokuwezesha-ufurahie-chochote-unachofanya-na-kuwa-na-furaha-kwenye-maisha/)
Rafiki, nina habari njema sana kwako ambazo zitakuwezesha kupata maarifa zaidi na kuweza kuyatumia kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Nimeanzisha programu mpya ya kupata vitabu vya kusoma pamoja na chambuzi za vitabu. Kama bado hujajua na kujiunga na programu hii, soma hapa na uchukue hatua sasa; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kusoma Vitabu Zaidi Ya 50 Kwa Mwaka Hata Kama Huna Muda Au Fedha Za Kununua Vitabu Vingi. (https://amkamtanzania.com/2019/02/13/hivi-ndivyo-unavyoweza-kusoma-vitabu-zaidi-ya-50-kwa-mwaka-hata-kama-huna-muda-au-fedha-za-kununua-vitabu-vingi/)
#4 TUONGEE PESA; UTAJIRI KAMA LENGO KUU KWENYE MAISHA.
Rafiki, kwenye kitabu chetu cha juma hili, ambacho kinaangalia jinsi ambavyo tunaweza kufikia ufanisi mkubwa sana kwenye chochote tunachofanya, pamoja na kufurahia sana tunachofanya na maisha yetu kwa ujumla, mwandishi anatuambia tunapaswa kuwa na kusudi kuu la maisha yetu, kisha kuwa na malengo yanayoendana na kusudi hilo, na mwisho kuhakikisha kila tunachofanya kinaendana na kusudi na malengo kwenye maisha yetu.
Mwandishi anatuambia bila ya kuwa na kusudi kuu mtu atapoteza nguvu zake nyingi asijue kipi muhimu kwake kufanya na kipi siyo muhimu. Lakini pia kuwa na kusudi lakini ukakosa malengo, utajikuta unashindwa kujua ufanye nini na hilo linakuumiza zaidi kwa sababu unalijua kusudi, lakini hulifikii.
Mwandishi anasema haijalishi kusudi kuwa zuri au kuwa baya, lakini lazima liwe na sababu ambayo inamsukuma mtu kulifikia ili aweze kuweka malengo na kuchukua hatua ya kulifikia.
Na hapa ndipo nilipofikiria kufanya utajiri kuwa lengo kuu la maisha yako. Soma kwa makini hapo, sijasema utajiri uwe kusudi, bali uwe lengo kuu. Sasa kama utajiri utakuwa ndiyo lengo, je kusudi litakuwa nini? Na hapo sasa ndipo wewe unapoweza kuweka chochote ambacho kinakusukuma kupata fedha zaidi.
Labda unataka kuwa na maisha bora, maisha yenye uhuru na yasiyosumbuliwa na hofu za kukosa fedha. Labda unataka kuisaidia jamii kwenye mambo mbalimbali ambayo wengi wanapata shida. Labda kuna tatizo kubwa la kijamii unataka kulitatua na hivyo ukiwa na fedha itakuwa rahisi kwako kulitatua.
Chagua chochote ambacho kinakusukuma sana kupata fedha, na kifanye hicho kuwa kusudi kuu la maisha yako. Baada ya kuwa na hilo kusudi, sasa lengo kubwa kwako ni kupata fedha, na weka kabia kiasi ambacho unahitaji kukipata, maana kusema tu fedha nyingi hakutoshi.
Baada ya kuwa na kusudi kuu linalokusukuma, na ukaweka kupata utajiri kama lengo kuu, sasa kila unachokifanya jiulize je kinapelekea wewe kupata fedha zaidi ili kufikia kusudi lako? Kama jibu ni hapana basi achana nacho mara moja.
Umefanya kazi na ukajisikia kuanza kuchoka, ukashika simu yako na kutaka kuingia kwenye mitandao ya kijamii, kabla hujaingia jiulize je kuingia kwako kwenye mitandao hiyo kunakuwezesha kupata fedha zaidi, kama jibu ni hapana, na ni hapana kwa asilimia 99 ya watu, basi usiingie na fanya kile kinachokuwezesha kupata fedha zaidi. Na kama umechoka kweli, njia bora ni kupumzika ili unapotoka kwenye mapumziko uwe na nguvu za kuchukua hatua zaidi, badala ya kuingia kwenye mitandao, ukapoteza muda zaidi na kujichosha zaidi.
Kila mmoja anapaswa kufanya utajiri kuwa lengo kuu la maisha yake, lakini kuwa na kusudi kubwa nyuma ya lengo hilo, kisha kupima kila unachotaka kufanya kama kweli kinakusogeza karibu na lengo hilo au kinakuondoa kabisa kwenye lengo hilo.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; DHIBITI TAARIFA ZINAZOINGIA KWENYE AKILI YAKO.
“Everything we experience – joy or pain, interest or boredom – is represented in the mind as information. If we are able to control this information, we can decide what our lives will be like.” – Mihaly Csikszentmihalyi
Hisia zozote ambazo tunazipata kwenye maisha yetu ni matokeo ya taarifa zinazoingia kwenye akili yetu na sisi kutafsiri taarifa hizo. Hivyo kama tunataka kudhibiti hisia zetu, basi kitu cha kwanza tunachopaswa kukidhibiti ni zile taarifa ambazo zinaingia kwenye akili zetu.
Na mifano iko wazi kabisa, unaweza kuwa una ujasiri na unafanya kitu fulani bila ya woga wowote, baadaye watu wanaanza kukuambia hatari ya kitu hicho na jinsi wengine wameshindwa, hapo hofu inakujaa na unashindwa kuendelea.
Na watu wanajua nguvu hii ya taarifa kwenye kuathiri hisia za wengine na wamekuwa wanaitumia kuwasukuma watu wafanye kile ambacho wanataka wao. Ulinzi mkubwa unaopaswa kuufanya kwenye maisha yako ni juu ya taarifa unazoruhusu ziingie kwenye akili yako. Lazima uzichuje sana, usikubali taarifa za hovyo ziingie. Na pia tafsiri taarifa zozote unazopata kwa njia chanya kwako, njia itakayokufanya uchukue hatua zaidi.
Kudhibiti hisia zako na kuweza kuendesha vizuri maisha yako, dhibiti taarifa ambazo zinaingia kwenye akili yako.
Rafiki, hizi ndizo tano za juma la 7 la mwaka huu 2019, ni tano zenye funzo kubwa kuhusu kuongeza ufanisi na kutengeneza furaha ya kudumu kwenye maisha yetu. Nenda kayaweke kwenye maisha yako haya uliyojifunza na utaweza kuwa na ufanisi mkubwa kwenye chochote unachofanya huku ukiwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako.
MUHIMU; Kama unataka kupata kitabu tulichojifunza kwenye juma hili, pamoja na mafunzo mengine muhimu ya ziada kutoka kwenye kitabu hiki kama sababu tatu za wengi kutoridhishwa na kazi na jinsi ya kuzivuka, nguvu kubwa inayoziweka familia pamoja na jinsi ya kuvuka hali yoyote ya msongo wa mawazo unayokutana nayo kwenye maisha basi karibu ujiunge na CHANNEL YA TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA. Tuma ujumbe kwa njia ya TELEGRAM MESSENGER kwenda namba 0717396253 wenye maneno TANO ZA JUMA na nitakuunganisha mara moja. Utapata nafasi ya kujifunza hayo na mengine mengi bure kwa wiki moja, na baada ya hapo utalipia elfu moja kila wiki. Karibu sana tujifunze kwa kina na kuyafanya maisha yetu kuwa bora.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu