“It is quite impossible to unite happiness with a yearning for what we don’t have. Happiness has all that it wants, and resembling the well-fed, there shouldn’t be hunger or thirst.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 3.24.17

Siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubww ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ADUI MKUU WA FURAHA..
Adui mkuu ww furaha ni kujipima kwa vitu ambavyo mtu huna.
Pale unapojiwekea lengo kwamba utakuwa na furaha ukishapata kitu fulani au kufikia hatua fulani, unajiandaa kutokuwa na furaha.
Kwa sababu kwanza unaahirisha furaha yako sasa kwa hicho unachopanga, lakini hata ukikifikia, utaona kuna kingine kikubwa zaidi cha kufikia.

Hii ndiyo inafanya kutafuta furaha kuwa kama mchezo wa kukimbiza kipepeo, kila unapokaribia kumfikia anaongeza mwendo zaidi, na wewe unaongeza mwendo, unapokuja kustuka umeshapotea kabisa kwa kuwa ulisahau mengine yote na kumkimbiza kupepeo, ambaye pia hukumkamata.

Usikubali kuahirisha furaha yako kwa jambo lolote lile. Wakati wako wa kuwa na furaha ni sasa, hapo ulipo sasa na kwa chochote unachofanya sasa, iwe unakipenda au la.
Ni rahisi sana kujidanganya kwamba furaha itakuja utakapopata kitu fulani au kufika hatua fulani.
Lakini nikutahadharishe tu, kama huna furaha hapo ulipo sasa, hakuna chochote utakachopata au kufikia kitakachokupa furaha, badala yake utazidi kujisikia hali ya kutokuwa na furaha.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuyafurahia maisha yako kwa pale ulipo sasa bila ya kuahirisha au kusubiri chochote.
#FurahaNiSasa, #UsikimbizeFuraha, #UsiahirisheMaisha

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha