Mapinduzi makubwa yanayoendelea kwenye sayansi na teknolojia, hasa ukuaji wa sekta ya TEHAMA, unaleta mvurugano mkubwa sana kwenye eneo la kazi.
Kazi ambazo zilikuwa zinafanywa na watu, sasa hivi zinaweza kufanywa vizuri sana kwa kompyuta na programu mbalimbali.
Hili limepunguza sana uhitaji wa watu kwenye maeneo ya kazi. Hili limewafanya wengi kukosa kazi za kufanya kwa kuwa teknolojia imewezesha kazi hizo kuwa rahisi zaidi.
Wale wanaoachwa nyuma kikazi na teknolojia hizi, ni wale ambao wanakazana kufanya kazi zao kama zilivyo, kufanya kwa mazoea, kama walivyofanya mwaka jana na miaka 10 iliyopita ambayo wapo kwenye kazi hiyo.
Rafiki yangu, leo nakukumbusha hili muhimu, kazi yako sasa hivi siyo kufanya kazi yako kama ulivyozoea kufanya. Badala yake kazi yako kubwa ni kuangalia njia bora ya kutoa thamani zaidi kwenye kile unachofanya.
Unapaswa kuangalia njia ya kufanya chochote unachofanya kwa ubora wa hali ya juu sana, kuweka utu wako kwenye kile unachofanya, kiasi kwamba hakuna kompyuta au teknolojia yoyote inayoweza kuchukua nafasi yako.
Kwa kila kazi unayofanya, jiulize je kompyuta inaweza kufanya kwa ubora kuliko wewe? Kama jibu ni ndiyo basi jua huna kazi, unavuta tu muda, ipo siku kazi hiyo itapewa kompyuta na wewe hutakuwa na cha kufanya.
Kazana kuwa bora sana, chochote unachokigusa kiguse kwa mguso wa kibinadamu, mguso wa kuongeza sana thamani kiasi ambacho hakuna mwingine awezaye kufanya.
Kazi yako katika zama hizi ni kutafuta majukumu bora zaidi unayoweza kuyafanya kwa utofauti ambao hakuna mtu mwingine au teknolojia inayoweza kufanya kwa ubora kuliko wewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,