“Robbers, perverts, killers, and tyrants—gather for your inspection their so-called pleasures!”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.34

Ni siku mpya, nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari GWARIDE KUU LA TAMAA…
Kama unataka kuyajua madhara ya tamaa kwenye maisha, waangalie wale ambao wamekubali maisha yao yaongozwe na tamaa.
Waangalie walevi, wazinzi, wezi, wauaji na hata watu jeuri, angalia jinsi maisha yao yanavyokuwa hovyo kwa kuruhusu tamaa ziwatawale na kuwaongoza.

Watu hao ni kama wako kwenye gwaride kuu la tamaa, na wewe ndiye unayekagua gwaride hilo.
Angalia jinsi ambavyo walichofikiri kingewaletea raha, kinakuwa mzigo kwao na kuvuruga maisha yao.
Na kabla hujaruhusu tamaa zikutawale, jikumbushe yale unayoona kwa wengine waliotawaliwa na furaha, na jiulize kama ndiyo aina ya maisha unayotaka.

Kuna raha ya muda mfupi kwenye tamaa, lakini mateso ya muda mrefu.
Usikubali kabisa tamaa ikuongoze na kukutawala, mara zote tumia fikra zako kwa usahihi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuondokana na tamaa na kutumia vyema fikra zako.
#TamaaNiMateso, #TumiaFikraZako, #JifunzeKwaWanaotawaliwaNaTamaa

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha