Mtu mmoja amewahi kusema kama maisha ni vita basi hakuna anayetoka akiwa hai. Akiwa na maana kwamba mwisho wa siku wote tutakufa, hivyo tunachopaswa kufanya ni kupambana kwenye kile ambacho tunapitia.
Kila mtu anapitia magumu kwenye maisha yake, hakuna ambaye maisha yake yamenyooka na anapata kila anachotaka kwa wakati anaotaka. Ni rahisi kuona maisha ya wengine ni rahisi, hasa ukiangalia kwenye mitandao ya kijamii, lakini ukiwekwa kwenye maisha yao, utaona wewe ni afadhali.
Sasa kwa kuwa magumu hayakwepeki, kuyalalamikia au kutaka kuyakwepa ni kupoteza muda wako, na kupoteza maisha yako pia.
Unapojikuta upo kwenye magumu, basi usilalamike wala kutaka kukimbia, badala yake endelea kuweka juhudi ambazo unapaswa kuweka. Pia pokea magumu hayo kama sehemu ya maisha yako, kama sehemu ya wewe kujifunza zaidi kuhusu wewe mwenyewe na kuhusu dunia pia.
Magumu unayopitia ni darasa, ni mtihani ambao unapaswa kuufaulu ili kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, hivyo usikimbie ugumu wowote, ukabili na kuuvuka na utamaliza ukiwa bora kuliko ulivyoanza.
Na kwa upande wa pili, kama bado hujakutana na magumu, usijisahau sana, jua kuna wakati utakutana na magumu, hivyo usikutane nayo na kuanza kulalamika kwamba dunia haipo sawa. Ni swala la muda tu, kila mtu anakutana na magumu kwenye maisha yake.
Lakini ipo njia moja ya kutokukutana na ugumu kabisa kwenye maisha yako, njia hiyo ni kutokufanya chochote, kutokusema chochote na kwa kifupi kutokuwa na maisha kabisa, yaani kuwa upo upo tu. Na hasara ya hili ni kwamba maisha yako hayatakuwa na maana na huenda ukaishia kuwa na sonona, na ukawa umerudi tena kwenye ugumu.
Magumu ni darasa, hayakwepeki wala kukimbilika, yakabili na utakuwa bora zaidi na kupiga hatua kwenye maisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,