“Remember that it’s not only the desire for wealth and position that debases and subjugates us, but also the desire for peace, leisure, travel, and learning. It doesn’t matter what the external thing is, the value we place on it subjugates us to another . . . where our heart is set, there our impediment lies.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 4.4.1–2; 15
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USITAMANI WALA USITAKE…
Ni rahisi sana kwetu kutamani kuwa na kila tunachotaka,
Pia huwa tunataka kila kitu kiende kama ambavyo tumepanga, kama tunavyotaka sisi wenyewe.
Tunataka dunia iache kila kitu na ihangaike na matakwa yetu.
Na hapo ndipo tunapojiangusha na kujikatisha tamaa,
Kwa sababu dunia haijali sana kuhusu matakwa yako, wala haijui kama hata upo. Dunia inajiendesha kwa misingi na kanuni zake yenyewe, hivyo kuitaka iende utakavyo wewe ni kujikatisha tamaa na kujiandaa kushindwa.
Kila unachotaka angalia kama ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako kukidhibiti. Kama ndiyo kifanyie kazi.
Lakini kama kitu kipo nje ya uwezo wako, basi usijiumize pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea.
Badala yake pokea kila kinachotokea na kitumie kwa manufaa zaidi kwako.
Utakuwa huru na mwenye furaha kama utakuwa tayari kupokea yale yaliyo nje ya uwezo wako na kuyafanya kuwa bora sana kwako.
Na kadiri unavyotamani vitu vichache, ndivyo unavyokuwa na uhuru mkubwa wa maisha yako.
Wengi wanajiingiza kwenye maisha ya mateso na utumwa kwa kutamani vitu ambavyo havina umuhimu mkubwa kwao. Hebu fikiri mtu anayekopa fedha ili kununua nguo ambayo ameona wengine wamevaa. Hivyo ndivyo tamaani inavyowaingiza watu kwenye utumwa.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutokutaka na kutokutamani, bali kupokea kila kinachokuja na kukitumia kwa ubora.
#TamaaNiMateso, #UsitamaniUsitake, #TumiaKilaUnachopataKwaUbora
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha