Tunapoyaangalia mafanikio kwenye ujasiriamali na hata maisha kwa ujumla huwa tunaangalia mambo makubwa makubwa. Kama kuwa na wazo la kimapinduzi, kuwa na mtaji mkubwa na hapa kuwa na timu kubwa ya kutuwezesha kupiga hatua zaidi.
Yote haya ni mazuri sana, lakini wote tunajua kwamba ni wachache sana wanaopata bahati ya kuanzia juu na kuwa na kila wanachohitaji. Kwa wengi wetu, tunaanzia chini kabisa, tunakua kidogo kidogo na siku moja tunakuwa juu kabisa.
Tunaanza tukiwa hatuna kila tunachotaka, lakini tunapambana mpaka kufika hatua ya kuwa na kila tunachotaka. Na ili kuweza kufanikiwa kwa kuanzia hatua za chini kabisa, kuna tabia ndogondogo ambazo tunapaswa kuzizingatia ili kufanikiwa.
Moja; kujipenda wewe mwewe.
Huu ndiyo msingi mkuu wa mafanikio kwenye jambo lolote, anza kwa kujipenda wewe mwenyewe. Ukijipenda mwenyewe unajithamini na kujisukuma zaidi ili kufanikiwa. Kama hujipendi utakata tamaa na kuishia njiani.
Mbili; penda kile unachofanya.
Unapaswa kupenda sana kile unachofanya, kwa sababu mwanzoni kitakachokusukuma ni mapenzi yako kwa kila unachofanya. Hakuna malipo makubwa utakayokuwa unayapata. Mapenzi ndiyo yatakupa hamasa ya kuendelea.
Penda sana bidhaa au huduma unayotoa kwa wateja wako, ipende na kuiamini kwamba hilo ndiyo suluhisho sahihi kwa wateja wako.
Tatu; wapende wateja wako.
Kuwapenda wateja wako kunakusukuma kuwa tayari kuwasaidia zaidi, na wao kuwa tayari kufanya kazi na wewe zaidi. Kuwapenda wateja kunakupa nafasi ya kuwahudumia zaidi hata kama hakuna manufaa makubwa ya kifedha unayoyapata. Kwa kujitoa zaidi kwa wateja wako kunakujengea sifa nzuri kwao.
Nne; kuwasikiliza wateja wako.
Kusikiliza unajifunza mengi sana kuliko kutokusikiliza. Ukiwa msikilizaji utaziona fursa nyingi za wewe kupiga hatua zaidi.
Tano; tafuta matatizo zaidi ya kutatua.
Kila unapokutana na wateja wako, tafuta matatizo zaidi waliyonayo ambayo unaweza kuyatatua. Na hili litawezekana kama unapenda unachofanya na unawapenda wateja wako. Unapotafuta matatizo zaidi unazipata fursa zaidi za kuwahudumia wateja wako.
Kama unaanzia chini kabisa, usikatishwe tamaa na ugumu wa safari au umbali unaopaswa kwenda, badala yake weka nguvu zako kwenye tabia hizi ndogo ndogo na utaziona fursa nyingi zinakuja kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,