Kabla ya kufikia mafanikio makubwa, lazima kwanza ubobee kwenye kile unachofanya. Iwe ni kazi, biashara au chochote unachofanya, lazima uwe mbobezi, lazima uwe kwenye asilimia 1 ya juu ya wale wanaofanya kitu hicho.

Sasa wengi wamekuwa wanakwama kwenye ubobezi, wanaanza kufanya kitu, mwanzoni wanakuwa na kasi kubwa kwenye kujifunza na kupiga hatua, lakini wanafika kwenye hatua ambayo wanakwama, hawawezi kwenda juu zaidi. Hapa ndipo wengi huvurugwa na kuona hawawezi kupiga hatua zaidi.

Lakini hatua zaidi zinawezekana, bila ya kujali mtu amefikia ngazi gani. Lakini ili kupiga hatua zaidi kuelekea kwenye ubobezi, sifa kuu mbili lazima zizingatiwe sana, la sivyo safari itakuwa ngumu na utakwama.

Sifa ya kwanza ni msimamo, lazima uwe tayari kufanya kile unachopanga kufanya kila siku bila ya kujali nini kinaendelea ndani yako au kwenye mazingira yako. Wengi wamekuwa wanakosa msimamo, kuanza kila mtu anaweza, lakini kuendelea ndipo wengi wanakwama. Unahitaji msimamo wa hali ya juu sana, wa kuendelea kufanya hata pale unapokuwa umechoka au hujisikii kufanya. Msimamo wa kuendelea kufanya hata mambo madogo madogo ambayo yanaonekana hayana umuhimu sana.

Sifa ya pili ni subira, unahitaji kuwa na subira kubwa, kwa sababu ubobezi hautokei kama ajali. Ubobezi ni mchakato, unahitaji subira ili kuweza kuufikia. Kwa wengi inachukua siyo chini ya miaka kumi kufikia ubobezi kwenye kile wanachofanya. Na hiyo ni miaka kumi ya kuendelea kufanya kwa msimamo. Unapoupa muda nafasi, huku wewe ukiendelea kuchukua hatua bila ya kuacha, hakuna kinachoweza kukuzuia usifikie ubobezi kwenye eneo lolote ulilochagua.

Jijengee sifa hizo mbili na ziimarishe kila siku, usikubali kuipoteza siku bila ya kuchukua hatua, na usikimbilie kutafuta njia za mkato.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha