“You shouldn’t give circumstances the power to rouse anger, for they don’t care at all.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.38
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HALI HAZIJALI HISIA ZAKO…
Usikubali hali yoyote inayotokea au kuendelea kwenye maisha yako iibue na kuchochea hisia zako.
Kwa sababu hakuna hali inayojali sana kuhusu hisia zako.
Mambo yanatokea kama yanavyotokea, na siyo kwa ajili yako.
Dunia inaenda kama inavyojiendesha, asili inaenda kama inavyojiendesha, haijali kama wewe upo au unachukuliaje kila kinachoenda.
Kuwaka hisia kutokana na yale yanayotokea ni kujiumiza na kujisumbua wewe mwenyewe.
Kama ulipanga kufanya kitu fulani kwenye siku yako, kitu ambacho kinahitaji uwepo wa jua, lakini siku hiyo mvua kubwa ikanyesha, kukasirika au kujisikia vibaya kwa kuwa mvua imenyesha na kuharibu mipango yako ni kujiumiza na kupoteza nguvu zako.
Mvua inanyesha au kutokunyesha kwa ratiba zake yenyewe na siyo kwa kuangalia wewe leo umepanga kufanya nini.
Tukielewa hili na kuliishi kila siku, tutapunguza matatizo mengi kwenye maisha yetu na kuwa na utulivu mkubwa. Kwa sababu kwa kila kitakachotokeam tutajikumbusha kwamba kinatokea kwa mipango yake yenyewe, na siyo kuangalia wewe umepanga nini.
Ukawe na siku bora sana leo, siku ya kutoruhusu yanayotokea yaibue hisia kali kwako, bali kuyapokea na kuyatumia vyema.
#DuniaHaiendiKwaMatakwaYako, #PokeaUnachokutanaNacho, #DhibitiHisiaZako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha