“Keep in mind that it isn’t the one who has it in for you and takes a swipe that harms you, but rather the harm comes from your own belief about the abuse. So when someone arouses your anger, know that it’s really your own opinion fueling it. Instead, make it your first response not to be carried away by such impressions, for with time and distance self-mastery is more easily achieved.”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 20

Ni jambo la kushukuru sana kwa nafasi hii mpya na ya kipekee ambayo tumeipata leo.
Siyo kwa akili wala nguvu zetu tumepata nafasi hii, bali kwa bahati na kwa kuwa bado tuna majukumu ya kutekeleza hapa duniani.
Tutumie muda tulioupata vizuri, huenda tusipate muda mwingine kama huu.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KINACHOKUUMIZA SIYO KINACHOTOKEA…
Huwa tunalalamika tumeumizwa na vitu fulani au watu fulani.
Lakini ukweli ni kwamba kinachokuumiza siyo kile kinachotokea, wala wale wanaofanya kitu fulani.
Kinachokuumiza ni tafsiri yako mwenyewe kwenye kile kinachotokea au wengine wanachofanya.

Kwa kifupi umekuwa unajiumiza wewe mwenyewe kwa maana ambazo unaweka kwenye yale ambayo yanayokea au watu wanafanya.
Hebu fikiria hili, wewe ni mchaga, ukakutana na mkurya, halafu akakutukana kwa lugha ya kikurya, ambayo hata huijui, hivyo hujui kaongea nini. Je hilo linakuumiza? Wala halitakufanya ufikiria, utapuuza na kuendelea na yako.
Lakini chukulia hali hiyo hiyo, katika mazungumzo yako na mkurya yule aliyekutukana kwa kikurya, kuna rafiki yako ambaye ni mkurya, akakutafsiria neno lile ambalo mtu amekuambia, na ukagundua ni tusi kubwa mno. Hapi utaumia sana, utakasirika, utapanga kulipa kwa maneno makali zaidi.
Lakini ukiangalia kilichobadilika ni maana pekee ambayo wewe umeingiza kwenye akili yako.

Hivyo kama unataka kuondokana na maumivu kwenye maisha, acha kutengeneza maana zinazokuumiza.
Mtu anapofanya kitu usichukulie kama amefanya makusudi kukuumiza wewe, na chochote kinachotokea usichukulie kama kimetokea kukulenga wewe.
Kwa mambo mengi, nenda kama hujaona au hujasikia, na hakuna chochote kitakachokuumiza.

Uwe na siku bora sana ya leo, siku ya kutokutengeneza maana za kukuumiza,
#UnajiumizaMwenyewe, #PuuzaYasiyoMuhimu, #DhibitiHisiaZako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha