Moja ya sababu zinazopelekea watu wengi kukwama kwenye hatua wanazochukua, ni kukosa maarifa sahihi.
Lakini kwa dunia ya sasa, ambayo ina wingi wa maarifa kuliko mtu yeyote anavyoweza kuyatumia, wengi huwa hawapendi kukubali kwamba hawana maarifa sahihi.
Wengi hufikiri kwamba kwa kuzungukwa na maarifa basi tayari wanayo. Haina tofauti na kufikiri kwamba ukikaa pembeni ya mto basi kiu yako inakatika mara moja.
Pia zama tunazoishi zimekuwa zama za zaidi na zaidi, pale mtu anapokwama basi anajua anahitaji kufanya zaidi. Lakini kama huna maarifa sahihi, zaidi haitakupa unachotaka, bali itakupoteza.
Kama haupo kwenye njia sahihi ya kufika unakokwenda, kuongeza kasi hakutakufikisha haraka, bali kutazidi kukupoteza zaidi.
Hivyo kwa kila eneo ambalo umekwama, kabla hujakimbilia kuchukua hatua zaidi, hebu jipe dakika chache za kutafakari kwa kina. Jiulize kama una maarifa sahihi kwenye eneo hilo. Jiulize kwa kile unachojua na hali ya mambo ilivyo, je kufanya zaidi kutaleta matokeo ya tofauti?
Kwa kuchukua muda mfupi wa kufanya tafakari hiyo, utaokoa muda mwingi sana ambao ungeupoteza kwa kukazana kufanya. Kwa sababu hakuna kiwango cha ufanyaji kitakachokupa matokeo sahihi, kama hauna maarifa sahihi juu ya kile unachofanya.
Ondoka kwenye wimbi la wale wanaofanya ili tu kuonekana wanafanya, ingia kwenye upekee wa kutafakari kila unachofanya, wa kuchukua muda na kuboresha maarifa yako ili uweze kufanya kwa usahihi na ubora zaidi.
Kwa maarifa sahihi na kuchukua hatua sahihi utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,