“Keep a list before your mind of those who burned with anger and resentment about something, of even the most renowned for success, misfortune, evil deeds, or any special distinction. Then ask yourself, how did that work out? Smoke and dust, the stuff of simple myth trying to be legend . . .”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 12.27
Ni siku moya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UTAPITA KAMA VUMBI NA MOSHI…
Kuna wakati tunaruhusu vitu vidogo vidogo vitusumbue kama vile tutaishi milele.
Vitu kama hisia za wivu, hasira, chuki na hata tamaa ya kupata zaidi, havipaswi kabisa kuvuruga utulivu wetu, kwa sababu hivyo vinapita na hata sisi wenyewe tunapota kama vumbi na moshi.
Hata vumbi litimke kubwa kiasi gani, hata kama ni kimbunga kikubwa kiasi gani ambacho kimetimua vumbi kubwa, wote tunajua baada ya muda vumbi hilo litatulia, kamwe halitatimka milele.
Kadhalika kwenye moshi, hata uwe mzito kiasi gani, tunajua baada ya muda utapita.
Hivi ndivyo tunapaswa kuyapeleka maisha yetu, maana yanapita haraka kama vumbi na moshi.
Badala ya kuyapoteza kwa yasiyo muhimu, ni vyema kuweka muda na nguvu zetu kwa yale ambayo ni muhimu zaidi.
Acha kuhangaika na kila kitu, hasa mambo madogo madogo kama vile utaishi milele, miaka 100 ijayo mengi unayohangaika nayo leo hakuna hata atakayekuwa anayakumbuka.
Kazana na yale muhimu, yake yatakayofanya maisha yako kuwa bora zaidi leo, yale yatakayofanya uifurahie siku ya leo, hata kama hujapata kila unachotaka.
Ukawe na siku bora ya leo, siku ya kuzingatia yale muhimu na kuachana na yasiyo muhimu.
#HutaishiMilele, #ZingatiaYaleMuhimu, #UnapitaKamaVumbi
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha