“Another has done me wrong? Let him see to it. He has his own tendencies, and his own affairs. What I have now is what the common nature has willed, and what I endeavor to accomplish now is what my nature wills.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 5.25

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo,
Ni siku bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUWAONESHA WALIOKUKOSEA…
Kuna wakati watu wanafanya tofauti na ulivyotegemea wafanye, wanakukosea.
Katika wakati huo unaweza kupata hasira sana na kutaka kuwaonesha kwamba wamekukosea ili wasirudie tena.
Unataka kuwaonesha makosa yao na kuwaonya wasiyarudie tena.
Lakini mara nyingi hatua yoyote unayochukua katika hali kama hiyo huwa unaishia kuijutia baadaye.

Hasa pale nia yako ya kuwaonesha watu kwamba wamekosea inapopitiliza au unapokuja kugundua kwamba wengi wanaokukosea wala hawafanyi hivyo kwa makusudi.
Na pia unapokuja kugundua kwamba kuwabadili watu siyo kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako, unaona ni kwa namna gani umepoteza nguvu zako.

Ondokana na dhana ya kumwonesha kila ambaye amekukosea, mara nyingi unapofanya hivyo unaibua matatizo mengi zaidi ya yale ya awali.
Mtu anapokukosea, tafakari kile alichofanya na ona kama ni lazima sana wewe kumweleza kile alichokosea na fanya hivyo.
Lakini usiwe na nia ya kumwonesha, yaani kutaka kulipa kile alichokosea, utafanya jambo dogo liwe kubwa sana, na likupotezee muda na nguvu zaidi.

Watu hawataacha kukukosea, ukiwa na nia ya kumwonesha na kumkomesha kila anayekukosea, maisha yako yote yatakuwa ya kuhangaika na watu na usiweze kufanya yale muhimu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuondokana na fikra za kuwaonesha na kuwakomoa wale wanaokukosea.
#UsikipeUbayaKwaUbaya, #HuweziKumdhibitiMwingine, #UsihangaikeNaMamboMadogo

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha