Ukiangalia binadamu kwa ujumla, utagundua tumegawanyika kwenye makundi mawili. Kundi la kwanza ni la wale wanaoweza kujiongoza wenyewe, hawa ndiyo wanaishia kuwa viongozi na kwa wengine pia na wanaofanikiwa sana. Kundi la pili ni wale ambao hawawezi kujiongoza wenyewe, hawa huishia kuwa wafuasi na hawapigi hatua kubwa kwenye maisha yao.

Chukua kundi la watu ambao hata hawajuani, waweke sehemu moja, na baada ya muda kuna wachache watakuwa viongozi na wengi watakuwa wafuasi. Kinachowatofautisha watu kwenye makundi haya mawili ni tabia walizonazo.

Kuna tabia ambazo wafuasi wengi wanazo, zinazowafanya washindwe kujiongoza na hata kuwazuia kufanikiwa. Ukizijua tabia hizi na kuachana nazo, utaweza kuwa kiongozi wako mwenyewe na hata kiongozi kwa wengine pia.

Hapa nakushirikisha tabia chache ambazo wafuasi wengi wanazo, ambazo ni kikwazo kikubwa kwao, na kama unazo pia basi achana nazo.

Moja; maigizo.

Wafuasi wengi wanapenda sana maigizo, kila wanachofanya ni kwa ajili ya kuonekana. Hawafanyi chochote kama hawaonekani. Hata kama ni sehemu ya kazi, watakimbilia majukumu ambao yanawafanya waonekane wanafanya kazi sana. Watakuwa waongeaji na wapigaji wa kelele sana ili waonekane wanajua au wanafanya sana.

Viongozi siyo watu wa maigizo, viongozi wanafanya yale ambayo ni sahihi, iwe wanaonekana au la. Hawasukumwi kufanya vitu visivyo na thamani kwa sababu tu wanataka waonekane, wanafanya yale muhimu.

Mbili; udaku.

Wafuasi ni mashine za kuzalisha na kusambaza udaku. Wanajua kuhusu kila mtu na kila anachofanya. Wanayajua maisha ya wengine kuliko maisha yao binafsi. Ni mafundi wa kuzalisha na kusambaza tetesi ambazo hata hazina ushahidi.

Viongozi wanakuwa wametingwa na kazi zao kiasi kwamba hawajui hata maisha ya wengine yanakwendaje. Wao wanakazana na yale muhimu kwao, na kuacha wengine wakazane na yao.

Tatu; tabia ya mdudu kaa.

Kaa ni wadudu wenye tabia ya ajabu sana, wakamate kaa wawili na waweke kwenye kopo, kisha ondoa mfuniko wa juu na kaa hao hawataweza kuondoka kwenye kopo hilo. Kwa sababu mmoja akipanda juu ili atoke, mwenzake atamvuta chini. Kinachotokea wote wanabaki pale.

Hivi ndivyo wafuasi wengi walivyo, hawawezi kuvumilia kuona mtu mwingine anapiga hatua na kufanikiwa. Lazima watatafuta njia ya kumrudisha nyuma, kumkwamisha na hata kumfanya ashindwe ili asipige hatua kuliko wao.

Lakini viongozi wanapenda kuona wengine wakipiga hatua na kufanikiwa zaidi. Viongozi wanajua wengine wanapofanikiwa, na wao wanafanikiwa pia. Wanajua hakuna hatari yoyote kwa mtu mwingine kufanikiwa, bali ni faida kwao.

Nne; kulalamika.

Wafuasi huwa wanalalamika kwa kila kitu. Yaani haiwezi kuisha siku au kitu kikapita wakawa hawana kitu cha kulalamikia. Hata vitu vidogo kiasi gani, watatafuta mtu au kitu cha kulaumu. Watachelewa wenyewe eneo la kazi au kwenye jukumu muhimu na watakuwa na vitu vingi vya kulaumu, kuanzia foleni na hata hali ya hewa, lakini hawatajiweka wao kama tatizo.

Viongozi siyo walalamikaji, ni watu wa kupokea majukumu na kuchukua hatua. Viongozi wanapokutana na kitu ambacho hawakutegemea, wanaangalia kama iko ndani ya uwezo wao na wanachukua hatua na kama ipo nje ya uwezo wao wanachagua kuachana na kitu hicho na kupelekea nguvu zao kwenye mambo muhimu zaidi.

Tano; usimamizi.

Wafuasi hawawezi kufanya kitu kwa ukamilifu bila ya usimamizi wa karibu. Wakipewa jukumu lolote ni mpaka awepo mtu wa kuwasimamia kwa karibu au wa kuja kuwakagua kama wamefanya kwa usahihi.

Viongozi hata hawasubiri kupangiwa jukumu, wanajua kipi cha kufanya na wanakifanya. Viongozi wanazalisha matokeo na hayo ndiyo yanawawezesha kufanikiwa.

Chagua leo kama unataka kubaki kuwa mfuasi na uwe na maisha ya kawaida, au unataka kuwa kiongozi na uweze kufanikiwa sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha