Ni kanuni ya asili kwamba hakuna kitu kinachokua kama hakichochewi. Washa moto na kama hakutakuwa na vichocheo viwili; nishati na hewa ya oksijeni moto huo hautawaka.
Kadhalika panda mbegu na kama hakutakuwa na maji na rutuba, mbegu hiyo haitaweza kuota.
Kila kitu kwenye maisha kinahitaji kichocheo ili kukua zaidi.
Na hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye hofu ambazo mtu unakuwa nazo. Ili hofu hizo zipate nguvu, ziendelee kuwepo na kukua zaidi, zinahitaji kupata kichocheo.
Labda nikuulize kitu, umewahi kupita sehemu ambayo hujui kama kuna chochote kinaendelea, na ukapita bila ya wasiwasi wowote. Kisha baadaye ukasikia hadithi kwamba sehemu ile ina maajabu yasiyoeleweka, na watu wanaopita pale wamekuwa wanakutana na vitu vya ajabu. Safari nyingine unapita pale unaanza kupata hofu ya kukutana na vitu vya ajabu. Nini kimebadilika, sehemu ni ile ile, lakini hadithi unayojiambia ndani yako ndiyo inabadilika.
Ili hofu ipate nguvu na kukua, inahitaji kuchochewa na hadithi tunazojiambia. Hadithi tulizonazo juu ya maisha na yale tunayofanya, ndiyo ambazo zimekuwa zinachochea hofu mbalimbali ambazo tumekuwa nazo.
Ili hofu iendelee kuwepo, lazima uendelee kujikumbusha kuhusu hadithi inayoendana na hofu ile.
Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye hisia nyingine, kwenye chuki, huwezi kuwa na chuki kama hujikumbushi yale ambayo wengine wamekufanyia. Hata kwenye upendo pia.
Rafiki, hii ni kusema kwamba, kama tunataka kudhibiti hisia mbalimbali tulizonazo, eneo sahihi la kuanzia ni kwenye zile hadithi ambazo tunajiambia na kujikumbusha kila mara. Tukishachagua hadithi sahihi ambazo zinatuletea hisia bora kwetu, itakuwa rahisi kwetu kudhibiti hisia zetu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,