Mwanafalsafa Socrates alichukuliwa kama mtu ambaye alikuwa akijua sana katika enzi alizoishi, na hata mpaka sasa ndivyo ilivyo.
Lakini Socrates alipoulizwa kwa nini yeye ni mtu anayejua sana kuliko wengine? Na jibu lake lilikuwa kwamba kitu pekee ambacho yeye anajua ni kwamba hajui chochote.
Hivyo kama hajui chochote, kazi yake kubwa ni kujifunza. Lakini kama angekuwa anajichukulia kwamba tayari anajua, asingeweza kujifunza na asingeweza kujua zaidi.
Rafiki, nimependa kukukumbusha hili muhimu sana leo, umuhimu wa kukiri kutokujua ili uweze kujifunza zaidi.
Tunafanya makosa makubwa sana pale tunapofikiri kwamba tunajua kila kitu. Pale tunapoona tayari tunajua kila tunachopaswa kujua.
Mara nyingi hatujui kile tunachofikiri tunajua. Na kama unataka kubisha hili, chagua kitu chochote unachofikiri unakijua vizuri, kisha chukua karatasi na kalamu na andika kwa namna unavyokijua, kisha tafuta mtaalamu wa kitu hicho na mpe maelezo hayo na uone ni kwa kiasi gani atakukosoa.
Hata kama umebobea kwenye eneo fulani, bado yapo mengi ambayo bado huyajui, hivyo kuendelea kujifunza ni hitaji muhimu sana la kupiga hatua.
Na kwa zama tunazoishi sasa, ni zama za kujidanganya sana, kwa kuwa tumezungukwa na maarifa mengi, basi tunaamini tunajua sana. Kwa kuwa una vitabu vingi basi unafikiri unajua, wakati hakuna hata kimoja ambacho umesoma mwanzo mpaka mwisho na kukielewa.
Kubali kwamba hujui na hilo likupe msukumo wa kujifunza kwenye kila kitu na kwa kila mtu. Ukilinganisha na yale ambayo hujui, chochote unachofikiri unajua ni tone la maji kwenye bahari. Kuwa tayari kujifunza na utaweza kuwa bora na kupiga hatua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,