Lengo kuu la kila mtu kwenye maisha ni kuwa na furaha.

Kila tunachofanya ni kwa mategemeo ya kuwa na furaha zaidi.

Hakuna mtu anayeamka asubuhi na kusema leo nataka nikawe na siku ya hovyo kabisa. Kila mtu anategemea kuwa na siku nzuri na yenye furaha.

Hata wanaofanya uhalifu kama kuiba au kudanganya, ni kwa sababu wameshawishika watakuwa na furaha zaidi kwa kupata wanachoiba au wanachodanganya kuliko kinyume chake.

Sasa asilimia kubwa ya watu wamekuwa wanashindwa kwenye kupata furaha, kwa sababu njia wanayotumia siyo sahihi.

Kuna njia mbili kuu za kuelekea kwenye furaha, moja ni sahihi na inatumiwa na wachache, nyingine siyo sahihi na inatumiwa na wengi.

Njia sahihi ya kuelekea kwenye furaha ni SHUKRANI, unapokuwa mtu wa shukrani kwa kila kinachotokea kwenye maisha yako, unajiweka kwenye nafasi ya kuwa na furaha na maisha yako, bila ya kujali nini kimetokea. Shukrani inakufanya uangalie upande bora wa kila jambo, hata kama linaonekana kuwa jambo baya, na hii inakuwezesha kupata nafasi nzuri zaidi kwa kila unachokutana nacho.

Njia isiyo sahihi ya kuelekea kwenye furaha ni MATARAJIO, kila unapoweka matarajio fulani kwenye maisha au unachofanya, unajiweka kwenye hali ya kutokuwa na furaha. Kwa sababu ni mara chache sana mambo yatakwenda kama ulivyotarajia. Mara nyingi unapanga hivi na yanatokea mengine kabisa. Sasa unapokuwa na matarajio makubwa, na kuona utakuwa na furaha ukiyafikia, unajiandaa kutokuwa na furaha, kwa sababu huwezi kudhibiti kinachotokea. Matarajio yoyote unayoweka kwenye vitu au watu yatakuangusha, kwa sababu vitatokea vitu ambavyo hata hukutegemea vitokee.

Hivyo kazana kuwa mtu wa shukrani na acha kulazimisha matarajio yako ndiyo yatokee, weka malengo na mipango, weka juhudi kubwa kisha matokeo unayoyapata yapokee kwa shukrani, jifunze na kisha chukua hatua bora zaidi. Kwa namna hii utakuwa unakua zaidi kila mara na huku ukiwa na furaha wakati wote, hata kama hujapata ulichotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha