“So, concerning the things we pursue, and for which we vigorously exert ourselves, we owe this consideration—either there is nothing useful in them, or most aren’t useful. Some of them are superfluous, while others aren’t worth that much. But we don’t discern this and see them as free, when they cost us dearly.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 42.6

Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KILA KITU KINAKUGHARIMU…
Kila unachotafuta, unachonunua, unachopokea na hata kukubaliana nacho, kinakuja kwako na gharama.
Kila kitu unachokuwa nacho, hata kama umepewa bure, kinakuja na gharama kwako.
Kila mali unayokuwa nayo inakuja na gharama kwako,
Kila mahusiano unayokuwa nayo yanakuja na gharama kwako,
Na kila hisia unazokuwa nazi, zinakuja na gharama kwako.
Hata vitu unavyopeww bure, bado inakuingia gharama kukaa navyo na kuvitunza.

Hivyo njia moja ya kupima umuhimu wa vitu kwako ni kulinganisha manufaa yake na gharama unayoingia kuwa na vitu hivyo.
Kwa kulinganisha huku, utaweza kuona vitu ambavyo vina gharama kubwa kwako, lakini havina manufaa yoyote.
Unakazana kuvitafuta au kuvitunza na hakuna kizuri vinaleta kwenye maisha yako.

Chukua mfano wa hasira, ili uwe na hasira na mtu lazima uendelee kubeba kumbukumbu za mabaya aliyokufanyia. Hivyo kila unapokutana naye lazima ujikumbushe hadithi nzima ili kuibua hisia za hasira ndani yako.
Hivyo kukaa na hasira ni gharama kwako, kwa sababu hazitakuruhusu usahau chochote kilichotokea huko nyuma.

Kadhalika kwenye mahusiano na hata mali, kila mahusiano uliyonayo, kila mali unayomiliki, ni gharama kwako kuhakikisha unaendelea kuwa na vitu hivyo.
Hivyo unachopaswa kuangalia ni kama gharama unazolipa zinaendana na manufaa unayopata kwenye kitu husika.
Tafakari hili kwa kila unachofanya au unachomiliki na kuondoa yale yanayokugharimu sana muda na nguvu zako lakini manufaa yake ni madogo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kugharamikia vile ambavyo ni muhimu zaidi kwako, vile ambavyo vinayafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Katika siku hii hakikisha unakwepa sana kupokea vitu unavyopewa bure, kwa kuwa hivi huja na gharama kubwa zaidi.
#KilaKituKinaGharama, #EpukaVituVyaBure, #HangaikaNaYaleMuhimu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha