Lipo neno ambalo ni rahisi sana kutamka, lakini lina madhara makubwa sana kwa wengi. Neno hilo ni HAIWEZEKANI.

Ni rahisi sana kutumia neno hili pale tunapoweka mipango mbalimbali lakini katika utekelezaji tunakutana na vikwazo au changamoto.

Pia ni rahisi kutumia neno hili pale tunapowaangalia wengine ambao wamejaribu wakashindwa.

Rafiki, hakuna kitu ambacho hakiwezekani, hivyo kutumia neno HAIWEZEKANI ni kuchagua kuacha kufanya, kwa sababu hutaki kuweka juhudi zaidi kwenye kile unachofanya.

Badala ya kutumia neno haiwezekani, hebu anza kutumia neno INAWEZEKANA. Hata kama umekutana na magumu kiasi gani, anza kwa kujiambia inawezekana. Hata kama kila aliyejaribu ameshindwa, wewe jiambie inawezekana.

Ukishajiambia inawezekana sasa wajibu wako ni kuangalia njia ya kuwezesha hilo kutokea.

Kubadili tu kutoka kwenye HAIWEZEKANI kwenda kwenye INAWEZEKANA, kunabadili kitu kikubwa sana kwenye fikra zako. Mfano unaposema haiwezekani akili yako inajifunza na haiangalii tena njia mbadala za kufanya. Lakini unaposema INAWEZEKANA, hata kama hujui inawezekanaje, akili yako inaingia kazini kutafuta njia mbadala za hilo kuwezekana.

Nguvu za kufanya chochote tunachotaka zipo ndani yetu, na uwezo pia tunao, tunachohitaji ni kuwa na nia ya kupata kile tunachotaka, nia ambayo haivunjiki na kuisimamia mpaka tupate tunachotaka.

Anza sasa kutumia neno INAWEZEKANA kwenye kila eneo la maisha yako na utaleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha