“In public avoid talking often and excessively about your accomplishments and dangers, for however much you enjoy recounting your dangers, it’s not so pleasant for others to hear about your affairs.”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 33.14
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIWE MUONGEAJI SANA…
Kila mtu anapenda kuongea sana, hasa mambo yake binafsi.
Wapo wanaopenda kuongelea sana yale mafanikio yao,
Na wapo ambao kila wakati wanaongelea matatizo na changamoto zao.
Na kwa zama hizi za mitandao ya kijamii, watu hawana tena subira ya kutulia na kitu, chochote kinachotokea wanakimbilia kukiweka kwenye mitandao ya kijamii.
Mstoa Epictetus anatuonya kuhusu kuongelea sana mafanikio yetu na hata hatari zetu.
Kwa sababu haijalishi ni nzuri kiasi gani, watu wengi hawataki kusikia nini kinaendelea kwenye maisha yetu.
Kila mtu anapenda kusikilizwa zaidi, hivyo unapokuwa muongeaji zaidi, hasa wa mambo yako binafsi, wengi watakuepuka.
Kuwa msikilizaji zaidi badala ya kuongeaji zaidi,
Kuwa mtu wa kutaka kujua nini kinaendelea kwenye maisha ya wengine badala ya kuwa unajisifia kila mahali.
Na ongelea mafanikio na changamoto zako pale tu ambapo zinaweza kumsaidia mwingine, kutoa hamasa au matumaini kwa wengine kupiga hatua zaidi.
Lakini isiwe ndiyo mazungumzo yako kila unapokutana na wengine, watu wanachoka kusikia kila mara kuhusu wewe.
Na muhimu sana, weka mipaka ya vitu gani vitabaki ndani yako na vipi vitajulikana na wengine.
Na vitu hivi vitatu, Afya yako, utajiri wako na maisha binafsi ya kifamilia, vinapaswa kubaki ndani yako na siyo hadithi za kumweleza kila mtu au kuweka mitandaoni.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupunguza kuongea sana kuhusu wewe na kuwasikiliza wengine zaidi.
#KaaKimyaNaSikiliza, #HujifunziKwaKuongea, #OngeaWakatiMuhimu
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha