Kama hutafanya mabadiliko sasa kwenye maisha yako, hutafanya mabadiliko kabisa kwenye maisha yako.
Najua ni rahisi kwako kusema nitaanza kesho, nitaanza nikiwa tayari au nitaanza nikishamaliza kitu fulani.
Zote hizo ni njia za kujidanganya, usiukabili ukweli kwamba huwezi au hutaki kuanza, unatafuta sababu ambazo hazitakuumiza wewe.
Lakini ukweli unabaki wazi kwamba kama hutafanya mabadiliko sasa, kama hutaanza leo, hutaweza kubadilika wala kuanza.
Kama hutaanza leo kujifunza yale unayotaka kujifunza, nafasi ya wewe kuanza kesho au unapofikiri utakuwa tayari ni ndogo sana.
Kama hutaanza kuamka mapema leo, kama hutaanza kufanya mazoezi leo, kama hutaanza kula kwa afya leo, uwezekano wa kuanza siku zijazo ni mdogo mno.
Kama hutaanza biashara yako sasa, kama hutaanza kuweka juhudi zaidi kwenye kile unachofanya sasa, nafasi ya wewe kuwa bora zaidi siku zijazo ni ndogo, kwa kifupi haipo kabisa.
Ni vigumu sana kufanya mabadiliko kwenye maisha yetu kwa kupanga kuanza baadaye.
Ndiyo maana mtu anaweza kuwa kwenye ajira miaka mingi, akijiambia kuna siku atatoka na kwenda kujiajiri au kufanya biashara, lakini siku hiyo inakuwa haifiki kabisa. Inatokea siku moja anafukuzwa kazi, na hapo sasa ndipo mabadiliko ya kweli yanatokea kwenye maisha yake. Hasira anayoipata kwenye kufukuzwa anaiweka kwenye kujiajiri ili asitokee tena mtu wa kumnyanyasa na hapo anafanikiwa. Katika hali hii, mtu anakuwa amelazimishwa kubadilika na mazingira, na yamemfanya abadilike sasa na siyo kupanga kubadilika baadaye.
Kama unataka kufanya mabadiliko yoyote kwenye maisha yako, basi wakati sahihi wa kuyafanya ni sasa. Kama unajiambia unapanga kufanya mabadiliko, jua tu ya kwamba hakuna mabadiliko hapo, bali unajifurahisha na hutaki kuukabili ukweli kwamba hutaki kubadilika.
Mabadiliko ya kweli yanatokea pale unaposema IMETOSHA SASA, na kuchukua hatua sasa, siyo kupanga kubadilika baadaye. Chagua kubadilika sasa, au jiambie wazi kwamba hutaki kubadilika.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,