“Heraclitus called self-deception an awful disease and eyesight a lying sense.” —DIOGENES LAERTIUS, LIVES OF THE EMINENT PHILOSOPHERS, 9.7

Ni siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni fursa nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata katokeo ya tofauti kwetu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIAMINI SANA HISIA ZAKO…
Kama unafanya maamuzi kwa kusukumwa na hisia pekee, basi unafanya makosa makubwa sana kwenye maamuzi unayofanya.
Kwa kuwa mara nyingi hisia zetu huwa zinatudanganya.

Hata milango yetu ya fahamu tunayoiamini sana, kuna wakati inaweza kutudanganya sana, kama hatutakuwa makini.
Hasa kwenye kuona na kusikia, kuna vitu utaona na kufikiri vipo hivi, kumbe vipo tofauti kabisa.
Kadhalika kwenye kusikia, unaweza kufikiri umesikia vizuri kabisa, kumbe ulichosikia siyo kikichosemwa.

Mara nyingi tunasikia na kuona kile tunachotaka sisi, mtu anaweza kusema kitu fulani, lakini sisi tukasikia tunavyotaka kusikia wenyewe. Na hata kwenye kuona, kinaweza kufanywa kitu fulani lakini sisi tukaona kile tunachotaka kuona.

Hivyo kabla hatujakimbilia kufanya maamuzi, tuchukue kwanza muda wa kudhibitisha hisia zetu na hqta tulichoona au kusikia.
Jihoji na kutafakari kwa kina iwapo kile unachofikiria, ulichoona au kusikia ndiyo sahihi au hisia zako zimeingilia katikati.

Pia kwa kila unachotaka kufanya maamuzi, hebu fikiria kama kinyume chake ndiyo kingekuwa sahihi. Yaani jichukulie kama umekosea kabisa na upande mwingine uko sahihi. Sasa hapo unajipima upande uliopo na upande mwingine kuona upi sahihi zaidi.

Ni rahisi sana kujidanganya hasa pale hisia zinapokuwa juu.
Lakini tunapaswa kuepuka kufanya maamuzi katika hali hizo kwa sababu yanakuwa siyo maamuzi bora.
Tujenge msingi wetu kwenye utambuzi, kwa kufanya maamuzi sahihi na siyo ya kusukumwa na hisia.

Ukawe na siku bora ya leo, siku ya kufanya maamuzi sahihi na siyo kwa hisia.
#UsiaminiHisiaZako, #UnaonaUnachotakaKuona, #FikiriUpandeWaPili

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha