Huwa tunapenda sana kufuatilia hadithi za mafanikio ya wengine. Zinatupa hamasa na matumaini makubwa kwamba kama wengine wameweza na sisi tunaweza pia.
Na tunapoangalia kwamba walianzia chini kuliko sisi, na wakapitia magumu kuliko sisi, basi tunakuwa hatuna sababu kwa nini na sisi tusifanikiwe kama wao.
Na hili limefanya hadithi za mafanikio kuwa maarufu sana, vitabu vingi kuandikwa na hata biashara nyingi za maarifa kutengenezwa kwenye msingi huu.
Lakini kitu kimoja kimekuwa kinakosekana, licha ya watu kufuatilia hadithi hizi za mafanikio, bado wengi hawafanikiwi kama wale ambao wanafuatilia hadithi zao. Licha ya wengi kujua kwa hakika waliofanikiwa wametoka chini na kufika juu, bado wao wenyewe hawawezi kutoka walipo na kwenda juu zaidi.
Na hii ni kwa sababu kuna kitu kimoja ambacho wengi wanashindwa kukiona kwenye hadithi nyingi za mafanikio. Wengi hawaangalii kitu hicho muhimu na hivyo kushindwa kupiga hatua licha ya kujua hatua za kutoka chini mpaka juu.
Eneo ambalo wengi hawaangalii kwenye hadithi za mafanikio ni kafara iliyotolewa. Hakuna mtu ambaye amewahi kufanikiwa bila ya kutoa kafara, lazima mtu apoteze kitu fulani ndiyo apate mafanikio makubwa. Na ninaposema kafara hapa simaanishi imani za kishirikina, bali katika hali ya kawaida, kuna vitu inabidi upoteze ndiyo uweze kufanikiwa.
Wapo wanaopoteza usingizi wao, usiku na mchana hawalali, wanapambana kufanikiwa. Wapo wanaopoteza mahusiano yao, kwa kuweka muda na nguvu kubwa kwenye kile wanachofanya mahusiano yao na wengine yanavunjika kabisa. Wapo wanaopoteza fedha nyingi sana kabla hawajafanikiwa, wanakuwa wamejaribu vitu vingi ambavyo vimepoteza fedha zao nyingi kabla hawajafanikiwa.
Angalia kwenye kila hadithi ya mafanikio na utaona ku a kitu mtu alipoteza, na huenda hicho kisipewe uzito sana, lakini kwa kuangalia utaona. Hivyo sasa unapotaka kufikia mafanikio makubwa kama wale unaoangalia hadithi zao, swali la kwanza kujiuliza je ni kitu gani upo tayari kupoteza?
Kama unataka kupata mafanikio makubwa, huku maisha yako yakiendelea kuwa na kila ulichonacho au unachotaka, siyo tu unajidanganya, bali unapoteza nguvu zozote unazojaribu kuweka ili ufanikiwe. Kuna vitu inabidi upoteze ili kupata unachotaka, na kuna vitu ulivyonavyo sasa ndiyo vikwazo kwako kufanikiwa zaidi.
Kumbuka kujiuliza hili kila unapoangalia hadithi za mafanikio ya wengine, kipi walipoteza. Na kila unapoyafikiria mafanikio yako, jiulize ni vitu gani umeamua kupoteza.
Kwa kujua inabidi upoteze na kuchagua kupoteza baadhi ya vitu, unakuwa na amani na utulivu wa moyo, kwa kuwa hata wengine watakapokuambia mbona upande huu uko hivi, utajua huo umeamua kuachana nao ili ufanikiwe kwenye yale maeneo unayoyalenga.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,