Rafiki yangu mpendwa,
Mara nyingi tunaposikia miujiza, huwa tunaona ni watu wachache wanaoweza kuifanya. Mara nyingi wale ambao ni viongozi wa dini au wenye imani kali za kidini au hata za kishirikina.
Tumekuwa tunasikia hadithi mbalimbali za watu kufanya yale ambayo yanaaminika kwamba hayawezekani kufanyika. Tumekuwa tunasikia watu wanaoponywa magonjwa sugu na yasiyoponyeka kama saratani. Na tunaposikia habari kama hizi huwa tunafikiri ni uongo au wale walioweza kufanya hivyo wana uwezo wa miujiza, ambao sisi hatuna.
Lakini kitu kimoja ambacho kitakushangaza sana ni kwamba kila mmoja wetu ana uwezo mkubwa sana ndani yake, uwezo wa kufanya miujiza mikubwa sana kwenye maisha yake.
Hapo ulipo, ndani yako una nguvu kubwa sana unayoweza kuitumia kufanya miujiza mikubwa kwenye maisha yako. Unaweza kujiponya ugonjwa wowote unaokusumbua, na unaweza kuvuta kwako chochote unachotaka.
Na uzuri ni kwamba ili kutumia nguvu hizo kubwa ulizonazo, unachopaswa ni kujua kwamba zipo na kuzitumia. Huhitaji maombi au kufanyiwa chochote na yeyote, unachopaswa kufanya ni kujua nguvu zilipo na jinsi unavyoweza kuzitumia.
Sisi binadamu tuna nguvu kubwa sana ndani yetu, lakini hatujafundishwa kuhusu uwepo wa nguvu hizi. Hivyo tumekuwa tunaziacha zina dumaa au tunazitumia vibaya.
Kwa mfano kuna matumizi mabaya sana tumekuwa tunayafanya kwa nguvu zetu kubwa tulizonazo. Matumizi hayo ni kwenye hofu na msongo wa mawazo. Unapokuwa na msongo wa mawazo, mwili wako unajawa na homoni zinazouandaa mwili kwa kupambana au kukimbia. Mwili unakuwa na homoni hizo kwa wingi na hivyo unakuwa na nguvu kubwa ya kupambana au kukimbia, lakini unakosa nguvu kwenye kinga ya mwili. Na ndiyo maana mtu anapokuwa na msongo wa mawazo, afya yake inazorota sana.
Magonjwa mengi ambayo yanatusumbua sisi wanadamu, chanzo kikuu ni msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo unanyonya nguvu zetu nyingi na hivyo mwili hauwezi kutumia nguvu hizo kwenye kuimarisha kinga yake, kwa kurekebisha seli zilizoharibika na hata kupambana na viambukizi vya magonjwa.
Hofu na msongo wa mawazo ni moja ya njia ambazo tunatumia nazo vibaya nguvu kubwa ya kufanya maajabu iliyopo ndani yetu.
Kwenye kitabu chake cha BECOMING SUPERNATURAL, Dr. Joe Dispeza ametuonesha jinsi ambavyo watu wa kawaida wanafanya mambo ambayo siyo ya kawaida, kwa kutumia nguvu kubwa zilizopo ndani yao.
Joe anatufundisha kuhusu nguvu hizi, siyo tu kwa kutumia imani kama ilivyo kwenye dini mbalimbali, bali yeye anatumia tafiti za kisayansi, ambazo zinadhibitisha uwepo wa nguvu kubwa za kufanya miujiza ndani yetu.
Hivyo kama ulipoanza kusoma hapa ulijiambia haya ni mambo ya kusadikika, nikuambie tu ni mambo halisi, ambayo sayansi imedhibitisha ni kweli na yanafanya kazi.
Katika makala hii ya leo nakwenda kukushirikisha vituo nane ambavyo nguvu za kufanya miujiza zipo kwenye miili yetu na jinsi ya kutumia vizuri nguvu hizi ili kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yetu. Kwa kuvielewa vizuri vitu hivi nane, na kuweza kuvitumia vizuri, utaweza kuyafanya maisha yako yawe unavyotaka wewe na hata kuvutia chochote unachotaka kwenye maisha yako.
Karibu tujifunze vituo vikuu vya nguvu kwenye miili yetu na jinsi ya kuvitumia vyema.
KITUO CHA KWANZA; VIUNGO VYA UZAZI.
Kituo cha kwanza cha nguvu kipo kwenye viungo vyetu vya uzazi na kinadhibiti sehemu za mwili zilizopo chini ya kitovu. Hapa inahusika uke, uume, kibofu cha mkojo, sehemu ya mwisho ya utumbo na hata ngozi na misuli inayozunguka maeneo haya.
Kazi kubwa ya kituo hiki ni uzali, jinsia, kujamiiana na kutoa uchafu mwilini. Homoni za uzazi huzalishwa kwenye kituo hiki. Kituo hiki kina nguvu kubwa sana ya ubunifu na uumbaji, fikiria nguvu ambayo inatumika katika kujamiiana na hata kupata mtoto.
Watu wengi wamekuwa wanatumia nguvu ya kituo hiki vibaya kwa kuelekeza nguvu zao nyingi kwenye kujamiiana na kuwa na mahusiano mengi ya kingono. Hili linawapunguzia uwezo wa kufanya makubwa kwenye maisha yao.
Ili uweze kutumia nguvu hii ya kituo cha kwanza katika kufanya miujiza, unapaswa kujidhibiti sana kwenye eneo la ngono, kwa kuwa hili ndiyo linapoteza nguvu za wengi.
KITUO CHA PILI; TUMBO LA CHINI.
Kituo cha pili cha nguvu kwenye mwili ni tumbo la chini, hili ni eneo la mwili kwenye usawa wa kitovu. Kituo hiki kinadhibiti utumbo mpana, kongosho, kiuno, mifuko ya mayai na tumbo la uzazi kwa wanawake.
Kituo hiki kinahusika na ulaji, umeng’enyaji na utoaji wa mabaki ya chakula mwilini. Homoni mbalimbali huzalisha kwenye kituo hiki ambazo zinahusika na umeng’enyaji wa vyakula.
Kazi kubwa ya kituo hiki ni mahusiano ya kijamii, familia, utamaduni na hata mahusiano baina ya mtu mmoja na mwingine. Hiki ni kituo cha kushikilia au kuachilia au kuondoa. Kituo hiki kinapokuwa vizuri, mtu unakuwa na utulivu na kujisikia salama na amani.
Watu wengi wamekuwa wanatumia nguvu ya kituo hiki vibaya kwa kuwa na hasira na vinyongo kwa wengine na kukosa maelewano mazuri na wengine. Kila unaposhikilia kitu ndani yako dhidi ya mtu mwingine, unashikilia nguvu ambayo ungeweza kuitumia kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Ulaji uliopitiliza pia unaathiri kituo hiki kwa nguvu kubwa kutumika kumeng’enya chakula na kuondoa uchafu mwilini kitu ambacho kinazuia nguvu hiyo kutumika kwenye kutenda miujiza.
Ili kuweza kutumia vizuri nguvu ya kituo hiki, tunapaswa kudhibiti ulaji wetu na kuimarisha mahusiano yetu na wengine.
KITUO CHA TATU; TUMBO LA JUU.
Kituo cha tatu cha nguvu kwenye miili yetu ni tumbo la juu, hili ni eneo la mwili juu ya kitovu. Kituo hiki kinadhibiti tumbo la chakula, utumbo mwembamba, bandama, ini, mfuko wa nyongo, figo na tezi zilizopo juu ya figo.
Kituo hiki kinahusika na matakwa yetu, nguvu zetu, udhibiti, hamasa, msukumo na utawala. Hiki ni kituo cha mashindano na nguvu binafsi, kujithamini na hata kuwatawala wengine.
Kituo hiki kinapokuwa vizuri, unaweza kutumia nguvu za kituo hiki kufikia malengo yako, kuwa na hamasa ya kupiga hatua zaidi na kuzivuka changamoto mbalimbali unazokutana nazo. Kituo hiki pia kinakupa nguvu ya kujilinda wewe mwenyewe na kuwalinda wale wa karibu kwako.
Watu wamekuwa wanatumia vibaya nguvu za kituo hiki kwa kujiona wao ni wa muhimu kuliko wengine, kutaka kuwatawala wengine na hata kuwaonea wengine pale mtu anapokuwa na mamlaka au nguvu fulani.
Kutumia vizuri nguvu za kituo hiki tunapaswa kujijua sisi wenyewe na kujua nini hasa tunachotaka kisha kuweka nguvu zetu kwenye maeneo hayo. Hatupaswi kujionesha kwa wengine au kuwalazimisha wengine wawe kama tunavyotaka sisi.
KITUO CHA NNE; KIFUA.
Kituo cha nne cha nguvu kwenye mwili wako kipo kifuani kwako. Kituo hiki kinadhibiti moyo, mapafu, na tezi inayoitwa thymus ambayo ni tezi kuu ya kuzalisha kinga za mwili.
Kituo hiki kinahusika na hisia za upendo, kujali, huruma, shukrani, wema, kutokuwa mbinafsi, uzima na uaminifu. Kituo hiki ndipo imani na uungu wetu unapoanzia, ndiyo nafsi yetu ilipo. Kile tunachosema mtu ana roho nzuri, ni kwamba kituo hiki kinafanya kazi vizuri.
Kitu hiki kinapokuwa vizuri, tunajali kuhusu wengine, tunashirikiana vizuri na wengine, tunakuwa na mapenzi bora kwa wengine na maisha kwa ujumla na pia tunajiona wakamilifu na kuridhika na vile tulivyo.
Kukosa upendo, huruma na kutojali wengine ni kiashiria kwamba kituo hiki cha nne hakifanyi vizuri kwenye maisha ya mtu. Nguvu ya kituo hiki inakuwa haitumiki vizuri kumnufaisha mtu.
KITUO CHA TANO; KOO.
Kituo cha nne cha nguvu kwenye miili yetu kipo kwenye koo. Kitu hiki kinahusisha tezi za thyroid, tezi za mate, na tishu nyingine zilizopo kwenye eneo la kifua.
Kituo hiki kinahusika na kuonesha na kueleza upendo ambao unapatikana kwenye kituo cha nne pamoja na kuongea ukweli na kujidhihirisha wewe mwenyewe kupitia lugha na sauti.
Kituo hiki kinapofanya kazi vizuri sauti yako inawasilisha ukweli na kuonesha upendo wako kwa wengine. Unajisikia vizuri pale unapoweza kuwasiliana na wengine na kuwashirikisha mawazo na hisia zako.
Pale unaposhindwa kusema ukweli na kuwasilisha mawazo na hisia zako, ni kiashiria kwamba nguvu za kituo hiki hazitumiki vizuri kwako.
KITUO CHA SITA; UBONGO WA CHINI.
Kituo cha sita cha nguvu kwenye mwili kipo kwenye ubongo wa chini, kati ya nyuma ya koo na kichogo. Kituo hiki kinadhibiti tezi inayoitwa pineal ambayo ni tezi yenye nguvu kubwa ya kimiujiza. Tezi hii huwa inajulikana kama jicho la tatu, kwa kuwa ndiyo mlango mkuu wa kuelekea kwenye utambuzi wa hali ya juu.
Kituo hiki huwa kinafanya kazi kama antena ya redio, ambayo inanasa mawimbi ya stesheni za redio mbalimbali. Unapowasha kituo hiki, unaweza kunasa mawimbi ya juu kabisa, yaliyo juu ya milango mitano ya fahamu tuliyoizoea. Ni kupitia kituo hiki ndiyo tunaweza kufanya miujiza mikubwa, tunaweza kufanya yale ambayo kwa hali ya kawaida hayawezi kufanyika.
Kituo hiki kinapofanya kazi vizuri, ubongo wako unafanya kazi vizuri na unakuwa na uelewa sahihi wa ndani na nje yako. Unaweza kuona yale ambayo wengine hawaoni kwa urahisi.
Watu wengi wamekuwa hawajui wala kutumia kituo hiki cha sita, na hivyo nguvu kubwa ya kituo hiki inakuwa imelala ndani yao.
KITUO CHA SABA; UBONGO WA KATI.
Kituo cha saba cha nguvu kwenye mwili ni ubongo wa kati. Kituo hiki kinadhibiti tezi ya pituitary ambayo ndiyo tezi kuu inayodhibiti tezi zote za mwili. Hiki ndiyo kituo ambacho unapata uelewa na utambuzi mkubwa sana. Kwenye kituo hiki ndipo imani na utambuzi unapoanzia.
Kituo hiki kinapokuwa vizuri unakuwa na maelewano na vitu vyote kwenye maisha yako.
Pale ambapo unaona maisha yako hayaeleweki, hakuna kinachoenda kama unavyotaka na huna furaha, ni kwa sababu kituo hiki hakifanyi kazi vizuri, hujaweza kutumia nguvu yake kuweka maisha yako kwenye maelewano mazuri.
KITUO CHA NANE; JUU YA KICHWA.
Hiki ni kituo pekee cha nguvu ya mwili wako, ambacho hakipo ndani ya mwili wako. Kitu hiki kipo juu ya kichwa chako, usawa wa inchi 16 (sentimita 40) juu ya kichwa. Kituo hiki ndiyo kinadhibiti mwili mzima na kutuunganisha sisi na ulimwengu mzima.
Kituo hiki kinapokuwa vizuri unaweza kupokea miujiza na nguvu kubwa zinazoendesha ulimwengu. Ni kupitia kitu hiki ndiyo unapata mawazo ya kibunifu, ambayo hakuna mtu mwingine anayo au amewahi kuyafikiria.
Watu wengi hawajui kuhusu uwepo wa kituo hiki, na hivyo wamekuwa hawanufaiki na nguvu kubwa ya kituo hiki. Wanaishi maisha yao yote kwa kufanya yale waliyozoea kufanya, wasipate mawazo ya kibunifu ambayo yanatokana na kituo hiki.
Rafiki, hivi ndiyo vituo nane vya nguvu kubwa za miili yetu, ambazo tunaweza kuzitumia kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.
Vituo vitatu vya kwanza ni kwa ajili ya kuishi, hivyo nguvu zetu zinatumika sana kwenye vitu hivi kuhakikisha tunakula na kuzaliana na kujilinda, kazi kuu tatu za maisha yetu kuendelea kuwepo. Vituo vitano vya juu ni vya utambuzi na uwezo wa kufanya makubwa, kama upendo kwa wengine, kujitambua sisi wenyewe na hata kuweza kutumia nguvu kubwa inayoendesha ulimwengu.
Ili kuweza kutumia nguvu kubwa zilizopo kwenye miili yetu, tunapaswa kudhibiti vituo saba vya nguvu vilivyopo kwenye miili yetu, na kukusanya nguvu kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine.
Ugumu wa maisha unakuna pale nguvu zinapokwama kwenye kituo kimoja, hasa kwenye vituo vitatu vya chini. Mfano nguvu inapokwama kwenye ngono, mtu anafikiria na kuendeshwa na ufanyaji wa ngono pekee. Au nguvu inapokwama kwenye chakula, mtu anasukumwa na kutafuta chakula pekee.
Njia bora ya kutumia nguvu zetu ni kwa kufuata mtiririko ufuatao;
Kwenye kituo cha kwanza jiwekee uhakika na usalama wa kuweza kuzaliana, kisha nguvu kubwa ya ubunifu inayobaki inaenda kwenye kituo cha pili. Katika kituo hiki, tunahakikisha tunaweza kuvuka changamoto za mazingira, nguvu inayobaki tunaipeleka kwenye kituo cha tatu. Katika kituo hiki tunatumia nguvu hii kupiga hatua zaidi kwenye maisha yetu, kupata yale muhimu tunayotaka.
Nguvu inayobaki tunaipeleka kwenye kituo cha nne, ambayo inatumika kutengeneza upendo na uhuru, ambapo nguvu hii inapelekea kituo cha tano kuweza kuonesha na kueleza upendo wetu kwa wengine. Nguvu hii inapofika kwenye kituo cha sita, tunafungua milango yetu ya ufahamu na kuweza kuona yale ambayo wengine hawaoni. Nguvu hii ikifika kwenye kituo cha saba, mwili wetu unakuwa kwenye maelewano mazuri na vituo vyote saba vinafanya kazi kwa pamoja. Kwa nguvu hii kuwa kwenye kituo cha saba, na mwili kuwa na umoja, inakuwa rahisi kwetu kushirikiana na nguvu kubwa inayoongoza ulimwengu wote kwenye kituo cha nane. Hapa ndipo tunapopata ubunifu wa kipekee, tunapoweza kuvutia chochote tunachotaka na kufikia utambuzi wa hali ya juu sana.
Rafiki, fikiria mtiririko huu wa nguvu kwenye vitu hivi nane kama maji ambayo yanavukwa kutoka kwenye kisima, yanaanzia chini na kupanda juu zaidi.
Katika kitabu cha BECOMING SUPERNATURAL, ambacho nitakushirikisha uchambuzi wake kwa kina kwenye makala ya tano za juma la 10 2019, mwandishi ametufundisha namna bora ya kuamsha na kudhibiti vituo vyote vya nguvu vilivyopo kwenye miili yetu ili kuweza kufanya miujiza kwenye maisha yetu.
Anza kwa kuelewa vituo hivi nane vya nguvu, na kama utapenda kujifunza zaidi kuhusu uwezo wako wa kufanya miujiza na jinsi ya kuutumia, basi jiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 ya mwaka na utapata kitabu hiki pamoja na uchambuzi wake wa kina. Tuma ujumbe kwa kutumia app ya TELEGRAM wenye maneno TANO ZA JUMA na utaunganishwa kwenye channel.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge