#TANO ZA JUMA #10 2019; Unaweza Kufanya Miujiza, Nguvu Kubwa Ya Kufanya Miujiza Iliyopo Ndani Yako, Vituo Nane Vya Nguvu Za Miujiza Ndani Ya Mwili Wako, Jinsi Ya Kuvuta Fedha Zije Kwako Na Njia Pekee Ya Kubadili Maisha Yako.

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye tano za juma la 10 la mwaka huu 2019. Tunakwenda kumaliza juma jingine ambalo nina uhakika lilikuwa bora kabisa kwako. Na katika kulimaliza juma hili kwa ubora zaidi, tutakwenda kujifunza kuhusu nguvu kubwa za kufanya miujiza ambazo zipo ndani ya kila mmoja wetu na jinsi tunavyoweza kuzitumia.

Sisi binadamu tuna uwezo mkubwa sana, kuliko tunavyojua na kuliko tunavyoweza kujua. Imekuwa inasemwa kwamba tunatumia chini ya asilimia kumi ya uwezo ambao tunao. Yaani ukijichukulia wewe kama shamba lenye rutuba, ambalo lina heka 10, basi maisha yako yote umekuwa unalima heka moja pekee. Sasa hebu pata picha ni manufaa kiasi gani kama utaongeza mpaka kulima heka 3 au tano!

Juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa Becoming Supernatural: How Common People Are Doing the Uncommon kilichoandikwa na Dr. Joe Dispenza. Hiki ni kitabu ambacho kinakwenda kutufundisha namna ya kutumia nguvu kubwa iliyopo ndani ya kila mmoja wetu kufanya makubwa kwenye maisha yetu.

Becoming Supernatural

Karibu kwenye tano za juma hili, ambapo tutajifunza jinsi ya kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yetu na kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yetu, ikiwepo kupata chochote ambacho tunataka.

#1 NENO LA JUMA; UNAWEZA KUFANYA MIUJIZA.

Rafiki, kitu kimoja ambacho nataka kukuhakikishia ni kwamba, unaweza kufanya miujiza. Najua hili halitakuwa rahisi kwako kukubali wala kuelewa, lakini huo ndiyo ukweli.

Ukweli ni kwamba ndani yako una uwezo mkubwa sana, una nguvu kubwa sana ya kufanya miujiza, lakini hakuna mtu amewahi kukuambia uwepo wake. Na kama unavyojua, kama hujui kuhusu kitu basi huwezi kunufaika nacho.

Na hata kwa wale wachache ambao wamewahi kuonja miujiza kwenye maisha yao, bado wengi hawajawahi kujua wanaweza kusababisha miujiza hiyo peke yao. Wengi hufikiri wanaweza kupata miujiza kama ya uponyaji kama wakifanyiwa miujiza na wengine, labda kwa njia ya maombi au imani nyingine. Lakini ukweli ni kwamba humhitaji yeyote kupata miujiza, ni kitu unachoweza kufanya mwenyewe.

Sasa hatua ya kwanza kabisa katika kufanya miujiza kwenye maisha yako, ni kukubali kwamba dunia ni zaidi ya unachoona wewe.

Iko hivi rafiki, tangu tukiwa watoto mpaka tunakua, tumekuwa tunafundishwa dunia ni kile tunachoona, kwamba vitu pekee vilivyopo duniani ni vile tunavyoweza kuvidhibitisha kwa milango yetu mitano ya fahamu. Kwamba uweze kuona, kusikia, kugusa, kunusa na kuonja. Kama huwezi kudhibitisha kitu kwa njia hizo tano basi hakipo.

Sasa elimu hiyo ya kudhibitisha vitu kwa milango mitano ya fahamu imepitwa na wakati na ndiyo kikwazo kwako kufanya miujiza. Kwa sababu miujiza kwenye maisha huwa haiji kupitia milango hiyo mitano ya fahamu, bali huja nje ya milango hiyo.

Hii ni kusema kwamba, ipo nguvu kubwa ambayo inaiendesha dunia, ambayo hatuwezi kuiona, hatuwezi kuisikia, hatuwezi kuigusa, wala kuinusa au kuionja. Nguvu hii ni mawimbi ya umeme na sumaku, ambayo yana nguvu kubwa ya kusababisha chochote.

Chukua mfano huu ili kuelewa vizuri, ukiwa ndani ya chumba ambacho hakuna kitu bali uko na redio pekee, kuna mawimbi ya redio yanapita kwenye chumba hicho, lakini huwezi kuyadhibitisha kwa milango mitano ya fahamu. Lakini unapowasha redio yako, inanasa mawimbi hayo na unaanza kusikia sauti. Ukibadili stesheni unasikia redio nyingine.

Hivyo ndivyo unavyoweza kufanya miujiza kwenye maisha yako, kuelewa kwamba ipo nguvu kubwa ya mawimbi inayoendesha dunia, na unachohitaji ni kuiweka akili yako katika nguvu hiyo ya mawimbi na kuweza kutumia nguvu hiyo kuleta vitu vya tofauti kwenye maisha yako.

Kama redio inavyonasa mawimbi ya redio ikiwashwa na kufikia mawimbi husika, ndiyo na wewe unaweza kufanya miujiza kwa kuzalisha mawimbi kwenye akili yako, yanayoendana na mawimbi yanayoendesha dunia na hapo unaweza kutumia nguvu ya dunia kufanya chochote unachotaka.

Katika uchambuzi wa kitabu cha juma hapo chini, tutakwenda kujifunza njia sahihi za kuweza kuiweka akili yako kwenye mawimbi yanayoweza kunasa mawimbi yanayoendesha dunia na kuweza kufanya miujiza mikubwa.

#2 KITABU CHA JUMA; NGUVU KUBWA YA KUFANYA MIUJIZA ILIYOPO NDANI YAKO.

Juma hili la 10 tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa Becoming Supernatural: How Common People Are Doing the Uncommon kilichoandikwa na Dr. Joe Dispenza.

Dr Joe Dispenza ni daktari wa tiba mbadala na mbobezi wa sayansi ya akili na uwezo wa binadamu. Kupitia taaluma yake na hata uzoefu wake binafsi, ameweza kugundua uwezo mkubwa uliopo ndani ya akili na miili yetu, ambayo kama tukiweza kuutumia vizuri, tunaweza kupata chochote tunachotaka. Safari ya Joe katika eneo hili la uwezo mkubwa na miujiza ilianza pale alipoweza kujiponya mwenyewe maumivu ya mgongo ambayo madaktari walimwambia atahitaji kufanyiwa upasuaji na hataweza kutembea tena. Lakini kupitia nguvu ya akili, aliweza kujitibu bila ya upasuaji na mpaka sasa anaweza kutembea kama vile hajawahi kuwa na shida yoyote.

Katika kitabu hiki cha BECOMING SUPERNATURAL, Joe anatuonesha nguvu kubwa iliyopo ndani yetu, vikwazo vya nguvu hii kubwa na jinsi ya kuweza kuvivuka ili tuweze kufanya miujiza na kupata chochote tunachotaka.

Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu, uondoke na mambo ya kwenda kufanyia kazi kwenye maisha yako ili uweze kufanya miujiza na kufikia makubwa unayotaka.

MOJA; FUNGUA MLANGO WA MIUJIZA.

Joe anatuambia kikwazo cha kwanza kinachotuzuia sisi kufanya miujiza ni kuishi kwenye msongo. Jeo anatukumbusha jinsi mwili wetu unavyopokea na kutengeneza hali ya msongo. Tunapokuwa kwenye hali ya hatari, mfumo wetu wa mwili unaolinda mwili unazalisha homoni za hali ya hatari. Homoni hizi zinaleta mabadiliko makubwa sana kwenye mwili, ambayo yote yanauandaa mwili kwa ajili ya kupambana au kukimbia.

Pale homoni za msongo zinapokuwa juu, damu inapelekwa kwenye viungo vya pembeni kama mikono na miguu, mapigo ya moyo yanaongezeka ili kusukuma damu na nguvu zaidi ya kupambana na hali ya hatari.

Sasa kwa muda mfupi, hali hii haina ubaya, tena wakati mwingine inaimarisha mwili. Lakini inapokuwa ndiyo hali ya kila siku, kama kwa wale wanaoishi kwenye msongo kila siku, mwili mara zote unakuwa kwenye hali ya maandalizi ya kupambana.

Hivyo nguvu zote za mwili zinapotelea kwenye kujiandaa na hatari ambayo haiishi. Hali hii inapelekea kinga ya mwili kushuka kwa sababu nguvu hazipo kwenye kuutengeneza mwili bali kujiandaa na hatari. Pia akili haipati muda wa kufikiria na kuziona fursa zinazokuzunguka, kwa sababu mawazo yako yote yanakuwa kwenye hatari unazofikiria.

Hivyo hatua ya kwanza kabisa ya kufungua mlango wa miujiza ni kuacha kuishi kwenye hali ya hatari. Na katika zama tunazoishi sasa, hakuna hatari kubwa inayoweza kuondoa maisha yako kama kipindi ambacho wanadamu tuliishi misituni pamoja na wanyama wakali.

Hivyo pitia kila kinachokusumbua na kukukosesha amani, iwe ni kazi au biashara yako, mahusiano yako na wengine na hata mambo ambayo yamewahi kutokea huko nyuma. Kuwa tayari kuyapokea na kutoruhusu yawe sababu ya wewe kuishi kwenye hali ya hatari, hali ambayo inatumia nguvu zako kubwa za mwili lakini hupati matokeo yoyote mazuri.

MBILI; NGUVU YA WAKATI ULIONAO SASA.

Ili kuweza kufanya miujiza kwenye maisha yako, basi unapaswa kubobea kwenye wakati ulionao sasa. Hii ni changamoto kubwa kwa wengi, kwa sababu mara nyingi watu wanatumia muda mwingi kwenye yale yaliyopita, ambayo hawawezi kuyabadili, au kwenye yale yajayo ambayo hawawezi kuyaathiri.

Watu wanapoteza muda bora walionao sasa kwa kujutia yale waliyofanya huko nyuma au kuhofia yale yanayokuja. Huwezi kufanya miujiza kwenye maisha yako kwa kuishi jana au kesho. Miujiza inatokea pale unapoweza kuishi sasa, kuweka akili na umakini wako wote kwenye wakati ulionao sasa, kwenye kile unachokuwa unafanya.

Hatua muhimu ya kufanya miujiza kwenye maisha yako ni kujisahau kabisa wewe mwenyewe, kuweka umakini wako kwenye wakati ulionao sasa, kiasi kwamba unasahau kabisa wewe ni nani, uko wapi na ni wakati gani.

Sehemu kubwa ya maisha yetu tumekuwa tunaendesha kwa mazoea, tunakuwa tumeshazoea kufanya kitu kiasi kwamba tunaweza kukifanya bila hata ya kufikiria. Hebu fikiria kama umekuwa unaenda kwenye kazi au biashara yako kwa kupitia njia ile ile kila siku, kuna siku utatoka nyumbani na kufika eneo lako la kazi bila ya kukumbuka njia uliyopita. Yaani ulikuwa unaenda tu kwa sababu akili yako imeshazoea, na hivyo inakuwa sehemu ya mwili.

Sasa kwa kuendesha maisha kwa mazoea, huwezi kufanya miujiza, kwa sababu miujiza ni hali ya sasa, ambayo inahitaji uwepo wako kiakili. Unapofanya kitu kwa mazoea, akili yako inakuwa haipo kwenye kila unachofanya.

Ili kuweza kujiweka kwenye wakati wa sasa, kuweka akili yako kwenye chochote unachofanya, unapaswa kufanya tahajudi.

Tahajudi ni njia ya kushika udhibiti wa akili yako, kuiweka kwenye eneo moja na kuizuia isizurure kama ilivyo tabia ya akili. Utagundua kwamba bila ya kujidhibiti ni vigumu sana kutuliza akili yako sehemu moja. Akili inakuwa inahama hama yenyewe kutoka kwenye wazo moja kwenda jingine. Huwezi kutenda miujiza na akili ya aina hii, lazima uitulize, na njia ya kufanya hivyo ni kupitia tahajudi.

Kwa tahajudi, unakaa eneo lililotulia, unafunga macho yako kisha kuelekeza akili yako kwenye pumzi zako. Unapumua kwa kina huku fikra zako zote zikiwa kwenye pumzi yako. Utakapoanza kufanya hivi, akili yako itahama, lakini wewe irudishe kwenye pumzi yako. Fanya hivi kwa muda na utashika udhibiti wa akili yako na kuiweka kwenye wakati uliopo badala ya kuiacha izurure hovyo.

Miujiza inatendeka kwenye wakati uliopo na njia pekee ya kuiweka akili yako kwenye wakati uliopo ni kufanya tahajudi.

TATU; KUINGIA KWENYE UWEZO MKUBWA WA MAWIMBI YANAYOOENDESHA ULIMWENGU.

Kama ambavyo tumeshaona, dunia inaendeshwa na nguvu kubwa ya mawimbi ya umeme na sumaku. Mawimbi haya ndiyo yanayozalisha kila tunachokiona hapa duniani. Hivyo katika kufanya miujiza kwenye maisha yako, lazima uweze kuingia kwenye mawimbi haya yanayoendesha ulimwengu. Na njia pekee ya kuingia kwenye mawimbi haya, ni kutengeneza mawimbi ya akili yako ambayo yataendana na mawimbi ya ulimwengu.

Kumbuka mfano wa redio niliokupa, ukiwa hujawasha redio, huwezi kunasa stesheni yoyote. Lakini unapoiwasha redio, na kutafuta stesheni husika kwa kuweka namba ya mawimbi, unapata stesheni hiyo. Mfano unapoweka namba ya mawimbi 88.5Mhz kwenye redio yako, unaungana na redio fulani, ukienda namba nyingine, mfano 89.5Mhz, unanasa redio nyingine.

Hivyo nguvu ya miujiza tayari ipo kwenye mawimbi yanayoendesha ulimwengu, unachohitaji ni wewe kuwasha mawimbi ya akili yako ili uweze kuungana na mawimbi hayo na kupakua miujiza yako.

Ili kuwasha mawimbi yako ya kiakili unahitaji vitu viwili muhimu;

Kwanza unahitaji kuwa na nia dhabiti, kujua nini hasa unachotaka. Hili ni muhimu sana, hutapata muujiza kama hujui unataka nini. Hivyo anza na kile unachotaka. Kama ni afya, uponyaji, fedha, mali, kazi, biashara na chochote unachotaka kupata, lazima ujue kwa hakika unataka nini.

Kitu cha pili ni hisia chanya za kile unachotaka. Unapaswa kujua hisia chanya zinazoendana na kile unachotaka, hisia ambazo utazipata baada ya kupata unachotaka. Hizi ni hisia za furaha, shukrani, uhuru, ukamilifu, kujali wengine na nyinginezo.

Katika kupokea muujiza, vitu hivi viwili ni muhimu kwa sababu vinaunganisha akili yako (nia) na moyo wako (hisia). Muujiza unakuja pale akili na moyo vinapofanya kazi kwa pamoja, vinapokwenda sambamba.

Na hii ndiyo sababu kwa nini ni muhimu kuanza na kuondokana na msongo, ili kurudisha nguvu kwenye mwili, na pia kuweza kutumia wakati ulionao sasa, ili kutuliza akili na kuiweka kwenye kile unachotaka.

Kwa kufanyia kazi nia uliyonayo, na kuziishi hisia za nia hiyo kama tayari umeshapata unachotaka, unaunganisha akili na moyo wako na hii inatoa mawimbi ambayo yanaenda kuungana na mawimbi yanayoendesha dunia, na hapo utaanza kuona yale yanayoendana na kile unachotaka, hivi ndivyo miujiza inavyozaliwa.

NNE; KUBARIKI VITUO VYA NGUVU VILIVYOPO KWENYE MWILI WAKO.

Kwenye makala ya juma hapo chini, nimekushirikisha vituo nane vya nguvu ambavyo vipo kwenye mwili, na ambavyo ndivyo utakavyotumia kufanya miujiza mbalimbali kwenye maisha yako.

Sasa kwa tabia zetu sisi wanadamu, huwa nguvu nyingi zinaishia kwenye vituo vitatu vya chini, ambavyo vinatumia nguvu nyingi kwenye kufanya mapenzi, kula na kutaka kutawala wengine.

Ili kuweza kufanya miujiza kwenye maisha yako, unahitaji nguvu nyingi, na hivyo njia pekee ni kuondoa nguvu unayopoteza kwenye vitu vya chini na kuipeleka kwenye vituo vya juu.

Katika kubariki vituo vya nguvu kwenye mwili wako, unapaswa kufanya tahajudi ambayo unaweka fikra zako kwenye kila kituo, ukianzia kituo cha chini na kwenda kinachofuata mpaka kufika juu kabisa.

Kama ambavyo mwandishi amekuwa anatusisitiza, pale unapoweka umakini wako, ndipo nguvu zako zinapoenda. Unapofanya tahajudi ya vituo hivi, ukiweka umakini wako kwenye kituo kimoja, nguvu zako zote zinaenda pale. Ukihamisha umakini kutoka kituo hicho na kwenda kituo cha juu, unahamisha nguvu ile na kuipeleka kitu cha juu. Ukiendelea kupanda hivyo, utapeleka nguvu nyingi zaidi kwenye vituo vya juu. Na kadiri vituo vya juu vinapokuwa na nguvu kubwa, ndivyo unavyoweza kufanya miujiza mikubwa kwenye maisha yako.

Tumia nguvu unayopoteza kwenye vituo vya chini vya nguvu kuweza kufanya miujiza zaidi kwa kufanya tahajudi inayokusanya nguvu zako.

TANO; AKILI YA MOYO.

Moyo ni kituo cha nne cha nguvu kwenye miili yetu. Moyo ni daraja kati ya vituo vitatu vya chini, ambavyo huwa vinahusika zaidi na ulaji, uzalianaji na kujilinda na vituo vitatu vya juu ambavyo vinahusika na uungu na uwezo mkubwa tulionao. Moyo una nguvu kubwa ya upendo, kujali, huruma na utulivu kwenye maisha.

Huwezi kufanya miujiza kwenye maisha yako, kama moyo wako haupo kwenye utulivu na hauendi pamoja na akili yako. Pale moyo na akili vinapokwenda pamoja, nguvu ya kufanya miujiza inakuwa kubwa zaidi.

Tangu enzi na enzi, moyo umekuwa unachukuliwa kama kiungo muhimu sana kwenye maisha ya mwanadamu. Japokuwa kwa sasa kiungo muhimu kinachukuliwa kuwa ubongo, lakini tafiti zinaonesha moyo unaweza kufanya kazi wenyewe bila hata ua ubongo. Ndiyo maana wapo watu ambao wanaweza kuwa wamekufa ubongo, lakini mapigo ya moyo bado yapo, kwa kiingereza hii inaitwa BRAIN DEAD.

Tafiti pia zinaonesha moyo una mfumo wake wa fahamu ambao unadhibiti mwili kutokana na yale yanayoendelea kwenye mwili. Hivyo kama tukiweza kuelewa mioyo yetu vizuri na kuitumia, tutaweza kufanya miujiza mikubwa.

Mchango wa moyo kwenye miujiza ni kuzalisha hisia chanya ambazo ni kali. Hisia  za shukrani, uhuru, wema, kujali, huruma, upendo na furaha ni muhimu sana katika kufanya miujiza. Hisia hizi zinapokutana na nia iliyopo kwenye akili, zinazalisha mawimbi ambayo yanaungana na mawimbi ya ulimwengu kuzalisha miujiza.

Msongo wa mawazo wa muda mrefu ndiyo unaowazuia wengi kuweza kutumia nguvu ya mioyo yao kutenda miujiza. Msongo wa mawazo ndiyo chanzo kikubwa cha magonjwa ya moyo kama shinikizo la juu la damu na hata shambulio la moyo. Kuondokana na hali hii ya msongo, tunapaswa kuchochea hisia chanya na kuziishi muda wote. Hisia chanya haziwezi kukaa pamoja na msongo wa mawazo.

SITA; NGUVU YA SINEMA YA KIAKILI KATIKA KUZALISHA MIUJIZA.

Moja ya njia unazoweza kutumia kuwasha mawimbi ya akili yako ili kuvuta miujiza kwako ni kutengeneza sinema za kiakili. Hapa unatengeneza sinema ambayo inahusisha vile vitu unavyotaka kupata kwenye maisha.

Jinsi ya kutengeneza sinema hii, unachagua wimbo ambao unaupenda sana, wimbo ambao ukiusikiliza unaibua hisia chanya ndani yako. Kisha unakusanya picha zinazoendana na vile vitu unavyotaka. Unaunganisha picha hizo pamoja na wimbi ule unaoupenda kutengeneza sinema (video) fupi.

Hii inakuwa ndiyo sinema yako ya kiakili, unapoiangalia, akili inaona kile unachotaka huku wimbi ukiibua hisia chanya ndani yako. Kwa kuamsha vitu hivyo viwili kwa pamoja, inakuwa rahisi kwako kufanya miujiza.

Hii ni sawa na kuandika malengo yako kila siku, lakini ina nguvu zaidi kwa sababu unaona picha za kile unachotaka, huku muziki unaoupenda ukichochea hisia chanya ndani yako. Hisia na nia vinapokwenda pamoja, muujiza unatokea.

SABA; TAHAJUDI YA KUTEMBEA.

Zipo aina nne za kufanya tahajudi, unaweza kufanya ukiwa umekaa, ukiwa umesimama, ukiwa umelala na ukiwa unatembea. Tahajudi maarufu na inayofanywa na wengi ni ile ya kukaa. Lakini siyo mara zote utapata nafasi ya kukaa na kufanya tahajudi. Hivyo tunapaswa kujifunza namna ya kufanya tahajudi ya kutembea, ili hata unapokuwa unatembea kuelekea eneo fulani, badala ya kupoteza muda kufikiria mambo yasiyo muhimu, unatembea ukifanya tahajudi, hivyo unapata manufaa zaidi.

Katika ufanyaji, hakuna tofauti ya tahajudi ya kutembea na ya kukaa, zote unapeleka mawazo yako kwenye kitu kimoja. Lakini kwenye tahajudi ya kutembea, siyo lazima uweke mawazo yako kwenye pumzi yako kama unavyofanya kwenye tahajudi ya kukaa, badala yake unaweza kuweka mawazo yako kwenye kile unachotaka.

Yaani wakati unatembea, unatembea kama mtu ambaye tayari ameshapata kile ambacho unataka. Aina hii ya tahajudi kwa jina jingine inaitwa kuelekea kwenye muujiza wako. Kwa kuwa unatembea kama mtu ambaye ameshapokea muujiza wake, na kwa kuwa na hisia za mtu mbaye tayari ameshapata muujiza, inakuwa rahisi zaidi kwako kupokea muujiza wako.

Unapofanya tahajudi hii, unajiona kama mtu ambaye ameshapata kile anachotaka, huweki mawazo yako kwenye kile unachotaka, bali unaweka mawazo yako kwenye aina ya mtu ambaye umeshakuwa baada ya kupata unachotaka. Hivyo unaufanya mwili utoe mawimbi yanayoendana na kile unachotaka na hilo kurahisisha mijuiza.

Tumia fursa nyingi ulizonazo za kutembea kufanya tahajudi ya kutembea, ambayo itakuwezesha kufikia miujiza zaidi.

NANE; UHUSIANO WA NAFASI NA MUDA.

Katika ulimwengu ambao tumezoea kuishi, ulimwengu wa nafasi, tunapima kitu kutokana na nafasi yake. Tunatumia milango mitano ya fahamu kudhibitisha uwepo wa kitu, na kama hatuwezi kudhibitisha kitu kwa milango hiyo mitano basi hakipo. Kama tulivyojifunza, huo ni uongo ambao umewazuia wengi wasiweze kufanya miujiza.

Kuna nguvu kubwa ya mawimbi ambayo inaiendesha dunia, ambayo hatuwezi kuidhibitisha kwa milango yetu ya fahamu. Njia pekee ya kudhibitisha na kutumia nguvu hii ni kujua uhusiano wa nafasi na muda.

Huwa tunasema kila kitu kinachukua nafasi na muda, lakini kwenye ulimwengu wa mawimbi nafasi na muda vinakuwa kitu kimoja, na kitu hicho kinakuwa ni nguvu.

Mwanasayansi Albert Einstein alikuja na kanuni inayoleta pamoja nafasi a muda, kwenye kanuni hii; E = M X C, E ni nguvu/nishati, M ni uzito au nafasi ya kitu na C ni mwendokasi wa mwanga ambao unawakilisha muda.

Hivyo kuelewa vizuri uhusiano wa nafasi na muda, tunapaswa kujua kitu kimoja kinachounganisha dunia ni nguvu/nishati. Na hivyo mawimbi yanayoiendesha dunia yana nguvu kubwa ndani yake. Ili kuweza kufikia mawimbi haya na kufanya muujiza, lazima tuinue nguvu zetu kifikra, kwa kufikiria nafasi na muda kwa wakati mmoja.

Ili kutumia vizuri dhana hii ya nafasi na muda, kwanza unapaswa kuacha kujifikiria wewe kama mtu fulani na kujifikiria kama kuwa pamoja na kila mtu na mwisho kufikiria kuwa kama yeyote. Kadiri unavyoweza kujitenganisha na nafsi yako ya nyuma, na kuacha kufikria nafsi yako ya kesho, na kuwa katika wakati ulionao kwa ukamilifu, ndivyo unavyoweza kujiunga na nguvu kubwa inayoendesha dunia na kuweza kupokea miujiza mikubwa.

Kwa maneno mengine, kupokea miujiza mikubwa, lazima uwe tayari kujiachilia, kujisahau kabisa kuhusu wewe na kuamini nguvu kubwa ya dunia itakupa mazuri kama ukiiamini na kuiruhusu ifanye kazi yake.

TISA; TEZI YA PINEA.

Kituo cha sita kwenye vituo nane vya nguvu mwilini kipo kwenye ubongo wa chini, kwenye tezi inayoitwa pinea. Hii ni tezi ambayo huzalisha homoni mbili; serotonin na melatonin. Serotonin huzalishwa wakati wa mchana, hivyo mwana unapofika kwenye ubongo, pinea inachochewa kuzalisha serotonin ambayo inatuweka kwenye hali ya kuamka. Pale giza linapokuja, mwanga unapokuwa haufiki kwenye ubongo, pinea inazisha homoni ya melatonin ambayo ndiyo inaleta hali ya usingizi.

Homoni ya melatonin ndiyo inayoonekana kuwa na nguvu kubwa sana kwenye kufanya miujiza mikubwa kwenye maisha. Hivyo tunapaswa kujua njia za kuichochea tezi ya pinea katika kuzalisha homoni hii kwa wingi.

Moja ni kufuata muda, homoni hii huzalishwa kwa wingi kati ya saa saba usiku na saa kumi alfajiri, hivyo ukifanya tahajudi kwenye muda huo, akili yako inakuwa kwenye hali ya kupokea zaidi na hivyo kuweza kufanya miujiza mikubwa.

Njia ya pili ni kufanya tahajudi ya kubariki vituo vya nguvu, kwa kuanzia kituo cha kwanza na kupanda juu, unapofika kituo cha sita ambacho ni tezi ya pinea, unaelekeza nguvu kubwa pale ambazo zinakuwezesha kufanya miujiza mikubwa.

Tezi ya pinea ni kama antena ambayo inanasa mawimbi yanayoendesha ulimwengu, ni tezi yenye nguvu kubwa sana kwenye miujiza. Kwa jina jingine imekuwa inaitwa jicho la tatu, kwa sababu imekuwa inawawezesha wengi kuona kile ambacho hakionekani katika hali ya kawaida. Jifunze kuchochea tezi hii kuzalisha homoni ya melatonin ambayo inakuwezesha kufanya miujiza.

KUMI; KUIFANYA DUNIA KUWA SEHEMU BORA YA KUISHI.

Tafiti mbalimbali zimekuwa zinaonesha kwamba kama watu wakikusanyika pamoja na kufanya tahajudi kwa lengo la kuifanya dunia kuwa bora zaidi, katika kipindi hicho ambacho watu wanafanya tahajudi, dunia inakuwa katika hali nzuri. Vita vinapungua, ajali zinapungua na amani inakuwepo.

Hii ina maana kwamba, kila mmoja wetu, anayo nguvu ya kuifanya dunia kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi, kama kila mmoja wetu atafanya tahajudi kwa lengo la kuleta muujiza duniani, kwa kuondoa matatizo na kuleta amani, tunaweza kuifanya dunia kuwa sehemu bora kabisa ua kuishi.

Hivyo unapojifunza njia hizi za kuleta miujiza kwenye maisha yako, usiwe mbinafsi na kujifikiria wewe mwenyewe, badala yake leta muujiza na kwa dunia pia. Kwama wengi tutafanya hivi kwa pamoja, dunia itakuwa sehemu salama sana ya kuishi kwa kila mmoja wetu.

HITIMISHO; KUWA AMANI.

Umejifunza namna ya kufanya miujiza mikubwa kwenye maisha yako, lakini njia hizi zitafanya kazi, kama maisha yako yatakuwa bora wakati wote, yaani kama wakati wote utakuwa na amani na utulivu. Kwa sababu siyo kwamba utapata muujiza kwa kufanya tahajudi mara moja, bali kwa kurudia kufanya kila wakati, ndipo utakutana na muujiza.

Hivyo kama ukifanya tahajudi unakuwa na utulivu, lakini ukishamaliza tahajudi unarudi kwenye maisha ya awali, maisha ya kuwa na chuki, wivu, hasira, vinyongo, hutaweza kupata muujiza unaotaka kupata. Ili kutengeneza miujiza, lazima maisha yako yawe ya amani, kila kitu kiendane na ile hali ya tahajudi unayokuwa unayo wakati wa kutengeneza miujiza. Tawaliwa na hisia chanya wakati wote, kuwa na mahusiano bora na watu wengine na kuachilia, kutokushikilia chochote ambacho kinapingana na maisha ya amani.

Muujiza siyo kitu unachopata mara moja kama kunywa dawa, bali ni kitu unachokitengeneza kwa aina ya maisha unayochagua kufanya.

Nina imani unakwenda kuchagua maisha ya amani, maisha ya tahajudi, ya kuongozwa na nia njema na kuwa na hisia chanya wakati wote.

Kila la kheri katika kufanyia kazi haya uliyojifunza kwenye uchambuzi huu wa kitabu, ili uweze kuishi maisha ya miujiza, maisha bora na ya mafanikio makubwa kwako.

#3 MAKALA YA JUMA; VITUO NANE VYA NGUVU ZA MIUJIZA NDANI YA MWILI WAKO.

Katika kitabu chetu cha juma, tumejifunza mengi kuhusu uwezo mkubwa uliopo ndani yetu wa kufanya miujiza. Na ili kuweza kufanya miujiza, tunapaswa kujua vituo vya nguvu vilivyopo ndani yetu, ambavyo kwa kuvitumia vizuri, tunaweza kufanya miujiza mikubwa kwenye maisha yetu.

Katika makala ya juma, nimekushirikisha vituo hivi nane vyenye nguvu kubwa za kufanya miujiza kwenye maisha yetu. Vituo saba vipo ndani ya mwili wako, na kituo kimoja kipo nje.

Vituo vitatu vya kwanza vimekuwa vinanyonya nguvu kwa wengi na ndiyo kikwazo kwa wengi kufanya makubwa kwenye maisha yao. Kituo cha nne ni kama daraja linalounganisha vituo vitatu vya chini na vituo vitatu vya juu. Vituo vitatu vya juu, kuanzia cha tano, sita na saba, ni vituo vya ukuu na uungu ndani yetu, ambavyo tukiweza kuvitumia vizuri tutaweza kufanya makubwa. Na kituo cha nane, ambacho kipo nje ya mwili wetu, ndiyo kinaunganisha mawili yetu na mawimbi yanayoendesha ulimwengu na hapo ndipo tunapoweza kupokea miujiza mikubwa.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hii nzuri na muhimu kwako kuweza kufanya miujiza mikubwa, isome sasa hapa; Hii Ndiyo Nguvu Kubwa Iliyopo Ndani Yako Na Jinsi Unavyoweza Kuitumia Kufanya Miujiza.

#4 TUONGEE PESA; JINSI YA KUVUTA FEDHA ZIJE KWAKO.

Rafiki,

Tumejifunza mengi hapa kuhusu miujiza, na swali ambalo wengi wanaweza kuwa wanajiuliza ni je unaweza kutumia nguvu hii ya miujiza kwenye kupata fedha? Na jibu ni ndiyo. Unaweza kutumia nguvu yako ya kutenda miujiza kuvutia fedha zije kwako.

Na unachohitaji ni kufuata kanuni ya miujiza ambayo ni kuyatengeneza mawimbi ya mwili na akili yako yaendane na mawimbi yanayoongoza ulimwengu. Mawimbi hayo yakishaendana, fursa za kupata fedha zitajitokeza kwake, katika wakati ambao hukutegemea kukutana na fura kama hizo.

Katika kutengeneza muujiza wako wa kifedha, fanya hatua zifuatazo;

Moja; chukua karatasi na kalamu, kwenye karatasi hiyo andika herufi moja ambayo inawasilisha fedha, kwa kiwango unachotaka. Kama ni milioni unaweza kuandika M, kama ni bilioni unaweza kuandika B. Unaweza kutumia herufi yoyote lakini ambayo kwako ukiiona unajua inawasilisha fedha.

Mbili; baada ya kuandika herufi hiyo, izungushie mistari miwili ya duara, mistari hii inawakilisha mawimbi ambayo yanazunguka fedha duniani. Unaweka mawimbi haya ili uweze kutengeneza mawimbi ya mwili, yanayoendana na mawimbi ya dunia yanayodhibiti fedha.

Tatu; upande wa kushoto wa herufi yako ya fedha, andika nia ya wewe kutaka kupata fedha unayotaka kupata. Hapa weka sababu zote zinazokupa msukumo wa kupata fedha hiyo unayotaka na pia andika vigezo ambavyo unataka fedha hizo zije navyo. Andika pia kile utakachotoa ili kupata kiwango hicho cha fedha, thamani ambayo utaitoa kwa wengine.

Nne; upande wa kulia wa herufi yako ya fedha, andika hisia ambazo utakuwa nazo ukishapata kiasi hicho cha fedha. Orodhesha hisia za juu kabisa ambazo utakuwa nazo baada ya kupata kiasi hicho cha fedha. Hisia hizi zinaweza kuwa shukrani, upendo, uhuru, kujali wengine na kadhalika.

Tano; hapa sasa unakuwa unafanyia kazi picha uliyoitengeneza kila siku, kila siku pitia mpango wako wa fedha, na kuwa na hisia kama tayari umeshapata fedha hizo. Kwa kufanya hivi kila siku, utashangaa fursa zaidi za kupata fedha zinakuja kwako. Kadiri unavyopitia picha hii ndivyo unavyounganisha mawimbi yako ya kiakili na mawimbi yanayodhibiti fedha, na unapokuwa na hisia kama tayari umeshapata fedha unazotaka, zinakuja kwako kwa urahisi zaidi.

ANGALIZO; Zoezi hili halimaanishi kwamba fedha zitakuja kwako bila ya kufanya kazi, kwamba utakaa tu na kufikiria fedha na kuweka hisia halafu fedha zinakudondokea, lazima uendelee kuweka kazi na kutoa thamani zaidi. Zoezi hili litakusaidia kuleta fursa nyingi zaidi kwako za kukuwezesha kupata kiasi cha fedha unachotaka. Lakini haliondoi ufanyaji wako wa kazi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; NJIA PEKEE YA KUBADILI MAISHA YAKO.

“The only way we can change our lives is to change our energy — to change the electromagnetic field we are constantly broadcasting. In other words, to change our state of being, we have to change how we think and how we feel.”

― Joe Dispenza

Njia pekee ya wewe kubadili maisha yako ni kubadili unakoweka nguvu zako, kubadili mawimbi ya umeme na sumaku unayosambaza kutoka kwenye akili yako. kwa maneno mengine, ili kubadilika, lazima kwanza ubadili fikra zako na hisia zako.

Joe amekuwa anarudia kauli hii mara kwa mara, kwamba pale unapoweka umakini wako, ndipo nguvu zako zinapokwenda. Hivyo kama tunataka kubadilika, lazima tuanze kubadili tunapoweka umakini wetu. Lazima tubadili fikra zetu na hisia zetu, kwa kuweka fikra na hisia kwenye yale maeneo tunayotaka na kuziondoa kwenye maeneo tusiyotaka.

Nguvu ya kufanya miujiza ipo ndani yako na umeshajua jinsi ya kuitumia, uwezo wa kubadili maisha yako unao na umeshajua jinsi ya kuutumia, ni wajibu wako sasa kushika hatamu ya maisha yako, na kuyafanya yawe kama unavyotaka wewe badala ya kuishi kwa mazoea.

Rafiki, nikutakie kila la kheri katika kufanyia kazi mambo haya uliyojifunza, ili maisha yako yawe ya miujiza, uweze kutengeneza maisha unayoyataka mwenyewe na kuishi maisha ambayo ni bora zaidi kwako.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Kwenye #MAKINIKIA ya kitabu hiki, nakwenda kukushirikisha TAHAJUDI TANO unazopaswa kuzifanya kila siku ili kutengeneza miujiza mikubwa kwenye maisha yako. Hakikisha upo kwenye CHANNEL YA TANO ZA JUMA ili usikose tahajudi hizi tano muhimu za kuzalisha miujiza kwenye maisha yako.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu