Rafiki,
Sisi binadamu tuna uwezo mkubwa sana ambao upo ndani yetu. Akili zetu zina uwezo wa kufanya makubwa sana. Na kabla hujaanza kujiuliza tunawezaje kufanya makubwa, kwanza angalia ushahidi uliopo. Anza na kifaa unachotumia kusoma maandishi haya niliyokuandikia, iwe ni simu au kompyuta, tambua kwamba karne moja iliyopita kifaa hicho hakikuwepo kabisa. Na wala hakuna aliyewahi kufikiri kingeweza kuwepo. Lakini leo hii unaona ni kifaa cha kawaida sana.
Maendeleo yote makubwa ambayo tumeweza kuyafanya hapa duniani, ni matokeo ya matumizi ya uwezo mkubwa wa kufanya miujiza wa akili zetu. Kila mtu anao uwezo huu, ila ni wachache sana wanaoweza kuutumia.
Wachache ndiyo wanaoweza kutumia uwezo huu kwa sababu wanakutana nao kama bahati au mazingira yanawalazimisha kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yao.
Akili yetu imegawanyika katika sehemu kuu mbili, kuna akili inayofikiri, hii inaitwa conscious mind, hii ndiyo akili inayofikiri na kufanya maaamuzi. Uwezo wa akili hii ni mkubwa katika kufikiri, lakini haiwezi kubeba taarifa nyingi kwa wakati mmoja. Sehemu ya pili ni akili isiyofikiri, hii inaitwa subconscious mind, akili hii huwa inapokea taarifa na kuzitunza, na inaweza kutunza taarifa nyingi na kwa muda mrefu. Sehemu hii ya akili ni kubwa na inabeba kila kitu ambacho mtu amewahi kukutana nacho kwenye maisha, iwe kwa kujua au kutokujua.
Watu wanaweza kufanya makubwa pale wanapoweza kuifikia na kuitumia akili ambayo haifikiri. Kitu ambacho siyo rahisi katika mazingira ya kawaida. Kwa sababu unapokuwa macho, akili inayofanya kazi zaidi ni ile inayofikiri. Na unapokuwa umelala, akili inayofikiri inapumzika, na akili isiyofikiri inaendelea kufanya kazi. Hiki ndiyo kinacholeta ndoto wakati unapokuwa umelala. Lakini ni vigumu kutumia akili hii kama utategemea wakati wa kulala pekee.
Watu mbalimbali wamegundua njia za kuifikia akili hii isiyofikiri, na kuweza kuchota uwezo wake kufanya makubwa. Baadhi ya njia hizo ni kama tahajudi (meditation), madawa yanayotuliza akili inayofikiri (psychedelics) na hata teknolojia ya sauti na picha. Watu wote ambao wamewahi kupata mpenyo wa kuja na kitu kipya ambacho kimeinufaisha sana jamii, waliweza kuitumia akili isiyofikiri, akili ambayo ina majibu ya kila kitu.
Rafiki, je wewe usingependa kuweza kufikia akili hii ili uweze kufanya makubwa? Je usingependa kuweza kuituliza akili inayofikiri kwa muda ili uweze kuchota majibu kwenye akili isiyofikiri? Naamini kila mmoja anapenda hili, changamoto ni kwamba wengi hawajui linafanyikaje.
Kwenye kitabu cha STEALING FIRE, waandishi Jamie Wheal na Steven Kotler wametufundisha jinsi ambavyo tunaweza kutumia njia mbalimbali kufikia akili yetu ya ndani isiyofikiri na kuweza kufanya makubwa. Kwenye kitabu hiki wametupa mifano mbalimbali ya watu wanaotumia njia hizo kufanya makubwa sana. Wakianza na makomandoo wa jeshi la marekani, wabunifu wa teknolojia mpya na hata wanasayansi wanavyoweza kuja na vitu bora kwa kuweza kufikia na kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yao.
Katika makala ya tano za juma hili la 11, nitakushirikisha uchambuzi wa kina a kitabu hiki, ili ujue njia unazoweza kuzitumia kufikia uwezo mkubwa uliopo ndani yako na kuweza kuja na majibu kwa changamoto au ugumu wowote unaopitia kwenye maisha yako, pamoja na kuweza kufanya makubwa.
Kwenye makala ya leo nakwenda kukushirikisha hali nne ambazo mtu unazipata pale akili yako inatoka kwenye hali ya kawaida na kwenda kwenye hali ya kufanya miujiza. Hali hizi nne zina manufaa sana kwa maisha yako na ukiweza kuzipata mara kwa mara utakuwa na maisha bora sana.
MOJA; KUONDOA UBINAFSI.
Unapoivuka akili inayofikiri na kuweza kuitumia akili isiyofikiri, hali ya ubinafsi inaondoka kabisa. Ule utofauti kati yako na wengine unapotea kabisa, unajiona wewe ni sehemu ya kila kitu na kila kitu kipo ndani yako.
Katika hali hii unasahau matatizo yako, unasahau chochote kinachokusumbua na unaona jinsi uwezo wako ulivyo mkubwa na unavyoweza kufanya chochote.
Unapokuwa katika hali ya kuondoa ubinafsi, unaacha kujikosoa mwenyewe na kujipa uhuru wa kufanya chochote. Mara nyingi huwa tunakuwa na mipango mizuri ya kufanyia kazi, lakini tunaanza kujikosoa wenyewe na kujiambia hatuwezi kufanya au haiwezekani. Lakini unapopoteza nafsi yako, kila kitu kinawezekana.
Faidia ya kuondoa ubinafsi au kuikosa nafsi unapokuwa kwenye akili isiyofikiri ni kwamba unaelewa nguvu iliyopo ndani yako na jinsi unavyoweza kuitumia pale unaporudi kwenye nafsi yako. Unapoikosa nafsi yako unakuwa kama mtu mwingine ambaye anakuangalia wewe, na unapojiangalia kama mtu mwingine kuna vitu unaviona, ambavyo usingeweza kuviona kama ungekuwa ndani ya nafsi yako.
MBILI; KUKOSA UKOMO WA MUDA.
Muda ni changamoto kwa kila mmoja wetu, mambo tuliyonayo ya kufanya ni mengi na muda tulio nao ni mchache, hivyo kila mtu anakimbizana na muda. Mbaya zaidi tunapoteza muda mchache tulionao kwa kufikiria jana ambayo imeshapita au kesho ambayo bado hatujaifikia.
Unapokuwa kwenye akili isiyofikiri, muda unakosa ukomo. Hii ni kwa sababu fikra zako zote zinakuwa kwenye muda uliopo na hivyo akili yako kuweza kubeba taarifa nyingi kwa wakati mmoja. Kwa wingi wa taarifa unazobeba, muda unafutika kabisa kwenye fikra zako.
Unaweza kuwa kwenye hali hii kwa muda mfupi, lakini ukaona kama umekaa masaa. Pia unaweza kuwa kwenye hali hii kwa masaa lakini ukaona kama umekaa kwa muda mfupi.
Unapokuwa kwenye hali isiyo ya kawaida, dhana ya muda inafutika kabisa na unachosumbuka nacho ni kile kilicho mbele yako, yaliyopita na yajayo hayapati nafasi kabisa kwako.
TATU; KUTOKUHITAJI KUTUMIA NGUVU.
Tunaishi kwenye zama ambazo taarifa na maarifa ni mengi, lakini hamasa ya kuchukua hatua haipo kabisa. Sasa hivi kila mtu anaweza kujua chochote anachotaka kujua, lakini licha ya kujua, wengi wamebaki pale walipo, kwa sababu hawana hamasa ya kuweza kuchukua hatua. Na hata wanapochukua hatua, wengi hukata tamaa na kuishia njiani.
Unapokuwa kwenye hali isiyo ya kawaida unapata msukumo mkubwa kutoka ndani yako wa kukuwezesha kuchukua hatua na kutokukata tamaa. Katika hali hii ubongo unazalisha homoni sita ambazo zina nguvu kubwa sana ya kutusukuma. Katika makala ya tano za juma, tutaziangalia kwa kina homoni hizi.
Katika hali hii ya kutokutumia nguvu, tunakuwa tayari kuchukua hatua kubwa kwa sababu hamasa ya ndani yetu inakuwa kubwa na kuweza kuvuka kikwazo chochote. Hatukatishwi tamaa na chochote tunachokutana nacho.
NNE; UTAJIRI.
Hali ya nne tunayoipata tunapokuwa kwenye hali isiyo ya kawaida ni utajiri. Katika hali hii unakuwa na utele na hakuna uhaba. Unajiunga na nguvu kubwa inayoiendesha dunia na chochote unachotaka unaona uwezekano wa kukipata.
Unapoweza kufikia akili yako isiyofikiri, inakuwa na majibu ya kila swali ulilonalo, inakuwa na uwezo wa kukupa kila unachotaka na hapa ndipo miujiza inapoanzia.
Katika hali hii, akili yetu inakuwa na utulivu wa hali ya juu sana na hakuna ambacho kinashindikana, hakuna uhaba na unajiunga na nguvu kubwa inayoendesha ulimwengu mzima.
Rafiki, hizo ndizo hali nne unazozipata pale unapotuliza akili yako inayofikiri na kufikia akili isiyofikiri ambayo inakuwezesha kufanya makubwa na miujiza.
Katika makala ya tano za juma la 11, tutakwenda kujifunza kwa kina jinsi ya kufikia hali hii isiyo ya kawaida, ili na wewe uweze kuwa na ubunifu mkubwa, uweze kufanya miujiza kwenye maisha yako na kupata kila unachotaka.
Kila la kheri.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge