#TANO ZA JUMA #11 2019; Utambuzi Wa Hali Ya Juu Ulionao, Mapinduzi Makubwa Ya Kiutambuzi Yanayoendelea Duniani, Hali Nne Unazozipata Wakati Ukiwa Kwenye Utambuzi Wa Hali Ya Juu, Utambuzi Wa Hali Ya Juu Kwenye Fedha Na Siyo Kila Tatizo Ni Msumari Kwa Nyundo Yako.

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye makala ya tano za juma la 11 kwa mwaka huu 2019. Ni imani yangu hili limekuwa juma bora sana kwako, juma ambalo umeweza kupiga hatua kubwa kwenye mipango ambayo ulikuwa umejiwekea.

Katika tano za juma hili, tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa STEALING FIRE: How Silicon Valley, the Navy SEALs, and Maverick Scientists Are Revolutionizing the Way We Live and Work kilichoandikwa na waandishi Steven Kotler na Jamie Wheal.

stealing fire

Hiki ni kitabu kinachotuonesha mapinduzi makubwa ya kiutambuzi yanayoendelea duniani, ambayo wachache wanaoyaelewa wanayatumia kufanya makubwa sana kwenye kazi zao na hata maisha yao kwa ujumla.

Waandishi wanatuambia kinachowatofautisha wale wanaofanikiwa sana, ambao wanakuja na vitu vipya na vya tofauti na wale wanaobaki kawaida, siyo kufanya kazi sana wala kuwa wavumilivu sana, bali uwezo wa kutumia utambuzi wa hali ya juu ndiyo unaowapa mawazo mapya na ya kiubunifu yanayoleta mafanikio makubwa kwao na kwa wengine.

Waandishi wametuonesha kwa mifano jinsi makomandoo wa jeshi la marekani pamoja na wajasiriamali wakubwa kwenye teknolojia na wanasayansi wanaokuja na uvumbuzi mkubwa wanavyoelewa na kutumia mapinduzi ya utambuzi mkubwa katika kufanya makubwa.

Pia waandishi wametuonesha jinsi gani na sisi watu wa kawaida, yaani watu ambao hawapo kwenye jeshi au sayansi na wasio na uwezo mkubwa wa kuwekeza kwenye hali hizi za utambuzi wa hali ya juu, tunavyoweza kutumia mapinduzi haya ya utambuzi katika kufanya makubwa kwenye maisha yetu.

Karibu kwenye tano hizi za juma, uelewe mapinduzi ya kiutambuzi na uweze kuyatumia kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

#1 NENO LA JUMA; UTAMBUZI WA HALI YA JUU UALIONAO.

Kila zama kumekuwa na mapinduzi yake, mapinduzi ya kwanza na makubwa kabisa kutokea dunia ilikuwa ugunduzi wa moto. Moto ulileta mabadiliko makubwa kwenye maisha ya wanadamu, na kama wengi wanavyosema, moto ulifanya wanadamu kuwa na nguvu ya uungu. Ni kupitia moto ndiyo maendeleo yote makubwa yameweza kutokea. Moto umetumika katika zama za chuma, kwa kuwa moto ndiyo ulioyeyusha vyuma kupata zana mbalimbali. Na hata katika mapinduzi ya viwanda, moto ndiyo msingi mkuu, kwa sababu msingi wa ufanyaji kazi wa injini yoyote ile, unategemea moto.

Sasa hivi tunaishi kwenye mapinduzi mengine ya tofauti na makubwa sana, haya ni mapinduzi ya kiutambuzi. Kwa kipindi kirefu, watu wa kawaida wamekuwa gizani, kwa kutumia utambuzi wa kawaida, ambao unawawezesha kupata yale mahitaji muhimu ya maisha, chakula, mavazi, malazi na kufanya mapenzi.

Lakini watu wachache, kwa bahati na kutokujua, wamekuwa wanajikuta kwenye utambuzi wa hali ya juu sana, utambuzi huu unawafanya waweze kuyaona matatizo kwa namna ya tofauti na suluhisho kuja kwa urahisi kuliko wanapokuwa kwenye utambuzi wa kawaida. Kipindi cha nyuma, wale waliofika kwenye hali hii ya utambuzi walieleza kwamba wameingiwa na Roho fulani au wamezungumza na Mungu na amewapa maelekezo, ambayo kweli yalikuwa bora na yenye manufaa.

Lakini kwa sasa tunaelewa kwamba hali hizi za utambuzi wa juu siyo kitu kinachotokea kwa bahati au ajali, bali ni kitu ambacho kinaweza kutengenezwa. Na watu wengi kwa sasa wanakazana kutengeneza hali hizi na zimeweza kuleta matokeo bora, sana. Maendeleo yote tunayoyaona kwenye sayansi na teknolojia, hasa upande wa teknolojia ya habari, ni matokeo ya watu kutumia utambuzi wa hali ya juu.

Tafiti nyingi zimefanywa na zinaonesha kwamba kila mtu ana uwezo wa kufikia utambuzi wa hali ya juu sana, utambuzi ambao siyo wa kawaida, ambao unamwezesha mtu kuona vitu kwa mtazamo wa tofauti na hata kupata suluhisho la matatizo ambayo yamemsumbua kwa muda mrefu.

Hii ni kusema kwamba, hapo ulipo, una uwezo mkubwa wa kufikia utambuzi wa hali ya juu kuliko ule ambao umekuwa unautumia kila siku. Utambuzi huu utakuwezesha kufanya makubwa sana kwenye maisha yako, kwa kifupi unaweza kufanya miujiza pale unapoweza kufikia utambuzi huo wa hali ya juu.

Usikubali kubaki gizani tena, anza sasa safari ya kufikia na kutumia utambuzi wa hali ya juu uliopo ndani yako, ambao unaweza kuufikia kwa njia mbalimbali unazokwenda kujifunza kwenye kitabu cha juma hili cha STEALING FIRE.

#2 KITABU CHA JUMA; MAPINDUZI MAKUBWA YA KIUTAMBUZI YANAYOENDELEA DUNIANI.

Rafiki yangu mpendwa,

Juma hili tunakwenda kujifunza mapinduzi makubwa ya kiutambuzi yanayoendelea duniani na jinsi watu wanavyonufaika nayo, na wewe pia unavyoweza kunufaika nayo. Haya ni mapinduzi ambayo waandishi wa kitabu cha STEALING FIRE: How Silicon Valley, the Navy SEALs, and Maverick Scientists Are Revolutionizing the Way We Live and Work wameyafananisha na wizi wa moto.

Kitabu cha STEALING FIRE kimeandikwa kwenye msingi wa hadithi maarufu ya wizi wa moto. Hadithi hii inamwelezea Prometheus ambaye alipewa mamlaka na miungu ya kuwasaidia wanadamu, lakini yeye akaiba moto na kuwapa wanadamu. Kitendo cha Prometheus kuiba moto na kuwapa binadamu, kimekuwa ndiyo chanzo cha mapinduzi makubwa sana kwa namna ambavyo binadamu tumeishi hapa duniani. Moto ndiyo msingi mkuu wa ustaarabu ambao umejengeka duniani. Baada ya Prometheus kufanya kitendo hiki, miungu ilikuwa na hasira naye sana kwa kuwa amewapa binadamu uwezo wa kiungu, na hivyo alifungwa kwenye jiwe na mwewe kuwa wanaudonoa mwili wake kama adhabu ya kitendo alichofanya.

Sasa hivi tunaishi kwenye mapinduzi mengine makubwa sana, makubwa kuliko mapinduzi ya moto. Mapinduzi tunayopitia sasa ni mapinduzi ya kiutambuzi. Zipo hali za juu sana za utambuzi ambazo watu wengi wamekuwa hawazifikii, ni watu wachache pekee ambao wamebahatika kufikia hali hizi na zikawa na manufaa sana kwao. Sasa hali hizi za utambuzi wa hali ya juu zimekuwa zinafichwa kama siri, hasa na dini na mataifa, kwa hofu kwamba kila mtu akijua utambuzi huu wa juu na kuutumia, atakuwa huru na kutokutegemea taasisi hizo kubwa mbili zinazoshikilia uhuru wa wengi, yaani dini na taifa.

Waandishi wanatuambia kwenye zama zetu, tunao watu kama Prometheus, ambao wanatushirikisha siri hizi za mapinduzi ya kiutambuzi licha ya kuzuiwa na dini na hata mataifa kufanya hivyo. Anasema watu hawa wanaiba moto na kuushirikisha kwa kila mtu kuweza kuutumia kufikia utambuzi wa hali ya juu na kuweza kufanya makubwa.

Karibu kwenye uchambuzi niliokuandalia kwenye kitabu hiki cha STEALING FIRE, uweze kuyaelewa mapinduzi yanayoendelea kwenye utambuzi na jinsi unavyoweza kuyatumia kufanya makubwa na kuwa na uhuru mkubwa kwenye maisha yako.

MOJA; HUO MOTO NI NINI.

Moto ambao waandishi wanauzungumzia kwenye kitabu chao ni hali ya utambuzi wa hali ya juu sana, ambao siyo wa kawaida. Wanamnukuu Plato akisema utambuzi wa hali ya juu ni pale utambuzi wa kawaida unapopotea na nafasi yake kuchukuliwa na utambuzi ambao unatuunganisha na nguvu kubwa inayoendesha dunia.

Kikwazo cha kwanza kwetu kufikia hali hii ya utambuzi mkubwa ni akili yetu ya kawaida, akili tunayotumia kufikiri. Akili yetu imegawanyika katika sehemu kuu mbili, akili inayofikiri (conscious mind) na akili isiyofikiri (subconscious mind). Sasa akili inayofikiri ina ukomo, inaweza kuchakata kiasi fulani cha taarifa kwa wakati mmoja. Ndiyo maana huwezi kusoma kitu, huku unaongea na mtu na wakati huo huo kusikiliza redio. Kuna ambacho hutaelewa kabisa. lakini akili yetu ya ndani isiyofikiri haina ukomo, inaweza kuchakata taarifa nyingi sana kwa wakati mmoja. Akili hii huwa inafanya kazi muda wote, haipumziki na wala haichoki. Hii ndiyo akili inayotuletea ndoto hata tunapokuwa tumelala.

Katika kufikia utambuzi wa hali ya juu, lazima tuweze kuituliza akili inayofikiri, ili tuweze kuifikia akili isiyofikiri.

Tangu enzi na enzi zimekuwepo njia za kutuliza akili inayofikiri ili kuifikia na kuitumia isiyofikiri. Baadhi ya njia ni halali na baadhi ni haramu kwenye jamii nyingi.

Kwenye kitabu hiki, waandishi wamegawa njia hizi kwenye makundi manne, saikolojia, biolojia, famasia na teknolojia. Tutajifunza kwa kina kuhusu kila kundi na kila njia inayopatikana kwenye makundi hayo.

Katika hali ya utambuzi wa hali ya juu, mtazamo wetu juu yetu na mazingira yanayotuzunguka unabadilika kabisa, hisia zetu na hata tabia zetu zinabadilika. Katika hali hii tunakuwa kwenye uwezo wa juu sana wa kufikiri na hata kuja na jawabu la mambo mbalimbali tunayopitia. Pia ni hali ambayo inaweza kutusaidia kuondokana na msongo, kupata uponyaji na hata kufanya miujiza mikubwa.

MBILI; KWA NINI MOTO HUU NI MUHIMU.

Hali hii ya kuweza kufikia utambuzi wa hali ya juu sana ni muhimu sana kwenye maisha yetu kwa sababu inatuwezesha kufikia na kutumia uwezo mkubwa sana uliopo ndani yetu. Unatuwezesha kuona yale yaliyotuzunguka ambayo kwa hali ya kawaida tumekuwa hatuyaoni, kwa kuwa akili yetu ya kawaida ina ukomo.

Pia tunapokuwa kwenye utambuzi wa hali ya juu, tunapitia hali nne ambazo zinakuwa na manufaa makubwa kwetu.

Hali ya kwanza ni kukosa nafsi, hapa unaacha kujiona wewe kama wewe na kujiangalia kama mtu mwingine, kitu kinachokufanya uweze kujiona zaidi ya unavyojiona.

Hali ya pili ni kuondoka kwa ukomo wa muda, unapokuwa kwenye utambuzi wa hali ya juu, muda pekee unaokuwa nao ni muda uliopo, hupotezi muda kwenye jana wala kesho yako, hivyo muda unakuwa hauna ukomo kwako.

Hali ya tatu ni kutokuhitaji nguvu, katika hali hii, huhitaji kutumia nguvu kubwa kupata majibu au kuona kile sahihi kufanya, kila kitu kinafunguka kwako.

Hali ya nne ni utajiri wa maarifa, katika utambuzi wa hali ya juu, unaweza kuyafikia na kuyatumia maarifa yote yaliyopo ulimwenguni. Unakuwa hauna kikomo chochote katika maarifa au taarifa.

Hali hizi nne nimezielezea kwa kina zaidi kwenye makala ya juma, isome kuelewa zaidi hali hizi.

TATU; KINACHOTUZUIA KUFIKIA UTAMBUZI WA HALI YA JUU.

Kama ambavyo tumeona, kufikia utambuzi wa hali ya juu kunatupa sisi uwezo mkubwa sana, tunaweza kusema uwezo wa kiungu na pia kunaleta uhuru mkubwa sana kwetu. Kuna vikwazo vikubwa vitatu ambavyo vimekuwa vinawazuia wengi kufikia utambuzi mkubwa, ni vyema kuvijua na jinsi ya kuvivuka ili visikuzuie wewe kufikia utambuzi mkubwa na kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Kikwazo cha kwanza ni dini. Dini imekuwa kikwazo kikubwa kwa wengi kuweza kufikia utambuzi mkubwa. Hii ni kwa sababu dini inapenda kuweka ukomo kwa waumini wake, kwenye vitu gani wanapaswa kuamini na vipi hawapaswi kuamini. Pia dini inaweza nguvu kubwa za kiroho kwa viongozi wa dini na kuwaacha wafuasi wa dini hizo kuwa tegemezi kwa viongozi wao pale wanapohitaji msaada wa kiroho. Ambacho watu wengi hawaambiwi ni kwamba, nguvu za kutenda miujiza, nguvu za kupokea uponyaji, nguvu za kupata chochote wanachotaka, tayari zipo ndani yao, ni wao kuzifikia na kuzitumia ili kunufaika nazo.

Ili kuvuka kikwazo hiki cha dini, tunapaswa kuwa tayari kufikiri na kujaribu vitu zaidi ya ukomo wa dini tulizonazo. Kujifunza zaidi kwa mifano kupitia waanzilishi wa dini hizo, kwa mfano kwenye Ukristo, Yesu ambaye ndiye dini hii imejengwa kwa misingi ya mafundisho na falsafa zake, alikuwa akisimamia vitu kwa namna ambayo ni tofauti na Ukristo unavyosimamia sasa. Hivyo ukichagua kujifunza na kuishi kama Yesu, utaweza kuvuka kikwazo cha dini. Kadhalika kwenye Uislamu na mtume Muhamad.

Kikwazo cha pili ni mwili. Miili yetu ni kikwazo kikubwa kwetu kuweza kufikia utambuzi wa hali ya juu, kama ambavyo tumeona kwenye akili inayofikiri, ambayo ina ukomo, kadhalika mwili nao umekuwa kikwazo. Miili yetu ni mizito kufikia hali ya utambuzi wa hali ya juu bila ya msaada wa madawa au teknolojia. Lakini wengi wamekuwa wakitegemea mwili na kuona kutumia dawa au teknolojia siyo njia sahihi ya kufikia utambuzi wa hali ya juu. Lakini kwa zama tunazoishi sasa, kutegemea mwili pekee ukufikishe kwenye utambuzi wa hali ya juu ni kujichelewesha, ni sawa na kukataa kupanda gari kwa safari ndefu na kuamua kutembea kwa miguu, utafika, lakini kwa kuchelewa na ukiwa umechoka.

Suluhisho la kikwazo hiki cha mwili ni kuwa tayari kuusaidia mwili kwa njia ambazo ni salama ili kufika haraka kwenye utambuzi wa hali ya juu. Tutajifunza njia mbalimbali kwenye teknolojia, baiolojia na hata famasia, yaani upande wa madawa mbalimbali. Kuna njia ambazo ni hatari na njia ambazo ni salama. Muhimu ni kujua kiwango cha hatari na usalama kabla ya kutumia.

Kikwazo cha tatu ni Nchi. Nchi au taifa imekuwa kikwazo kikubwa kwa wengi kuweza kufikia utambuzi wa hali ya juu. Kama tulivyojifunza hapo juu, kuna njia za kurahisisha mtu kufikia utambuzi wa hali ya juu. Mfano matumizi ya teknolojia na hata baadhi ya madawa au mimea. Mfano mzuri ni mmea wa bangi, mmea huu ndani yake una kemikali ambayo inaweza kumwezesha mtu kufikia utambuzi wa hali ya juu sana, japo kwa muda mfupi. Lakini kutumia mmea huu ni kinyume na sheria kwa nchi nyingi, baadhi ya nchi sasa hivi zinahalalisha mmea huu kwa matumizi ya matibabu na nchi nyingine zinahalalisha kwa matumizi ya burudani. Zipo teknolojia nyingi pia za kuwawezesha watu kufikia utambuzi mkubwa, lakini kwa kuwa zina hatari, nchi nyingi zinapiga marufuku. Katika kupiga huko marufuku inakuwa kikwazo hata kwa wale ambao wangeweza kutumia kwa umakini.

Kuvuka changamoto hii ya nchi ni kuangalia njia mbadala zinazokubalika kisheria za kukuwezesha kufikia utambuzi wa hali ya juu. Njia kama tahajudi, na kemikali zinazokubalika kisheria kama kahawa, teknolojia kama muziki na sanaa kama za michoro vinaweza kukufikisha kwenye utambuzi wa hali ya juu ukiweza kuzitumia vizuri.

NGUVU KUU NNE ZINAZOTUWEZESHA KUFIKIA UTAMBUZI WA HALI YA JUU.

Waandishi wametushirikisha nguvu kuu nne zinazotuwezesha kufikia utambuzi wa hali ya juu. Nguvu hizo ni saikolojia, biolojia, famasia na teknolojia.

Hapa tunakwenda kujifunza nguvu hizi na jinsi ya kuzitumia kufikia utambuzi wa hali ya juu.

NGUVU YA KWANZA; SAIKOLOJIA.

Saikolojia ndiyo nguvu ya kwanza ya kutufikisha kwenye utambuzi wa juu. Maendeleo kwenye eneo la saikolojia, hasa kwa kujitambua sisi binadamu na uwezo mkubwa uliopo ndani yetu, tunaweza kutoka nje ya miili yetu na kujiangalia kama wengine wanavyotuona.

Njia za kisaikolojia tunazoweza kutumia kufikia utambuzi mkubwa ni tahajudi, hapa unatuliza akili yako na kuweka umakini wako kwenye kitu kimoja. Njia nyingine ni ufanyaji wa mapenzi, zipo njia za tofauti za ufanyaji wa mapenzi ambazo zinasisimua maeneo mbalimbali ya mwili na kuchochea akili kwenda kwenye utambuzi wa juu.

Kujitambua wewe mwenyewe, ni hitaji muhimu sana katika kutumia saikolojia yako kufikia utambuzi mkubwa. Njia za kisaikolojia za kufikia utambuzi mkubwa ndiyo njia salama zaidi, ambazo zina hatari kidogo, lakini pia zinahitaji muda mrefu. Kwa mfano inakuhitaji muda wa angalau wiki 12 za kufanya tahajudi ya kina mpaka uweze kufikia hatua ya kuona manufaa yake, hasa katika utambuzi. Wakati kwa njia nyingine tutakazoziona, ndani ya muda mfupi unapata matokeo unayotaka.

NGUVU YA PILI; BAIOLOJIA.

Baiolojia ya ubongo na mishipa yetu ya fahamu ni nguvu nyingine kubwa inayotuwezesha kufikia utambuzi wa hali ya juu. Kupitia baiolojia tunayaelewa maeneo ya ubongo wetu na kazi zake tofauti, pia tunajua mchango wa homoni mbalimbali zinazozalishwa kwenye ubongo na jinsi tunavyoweza kuzifikia na tukaweza kufikia utambuzi wa juu.

Tumefundishwa na kuzoea kwamba akili inatawala mwili, lakini ukweli ni kwamba akili na mwili vinashirikiana, akili inashawishi mwili na pia mwili unashawishi akili. Kuna muunganiko mkubwa wa mishipa ya fahamu kati ya akili na moyo na kati ya akili na utumbo. Hii ina maana kwamba chochote kinachotokea kwenye moyo, kina athari kwenye akili, na chochote kinachotokea kwenye utumbo kinaathiri akili pia.

Njia za kibaiolojia tunazoweza kutumia kuchochea kufikia utambuzi wa hali ya juu ni kuupa mwili mazoezi ambayo yanapeleka mrejesho kwenye akili. Jinsi tunavyoiweka miili yetu kunachangia namna akili zetu zinavyokuwa.

Mazoezi kama ya yoga yana mchango mkubwa kwenye kufikia utambuzi mkubwa. Na pia kuuweka mwili kwa namna ambayo umeshapata kile unachotaka, kwa namna ya kujiamini, kunachochea akili kujiona kwa namna hiyo na hili kupelekea utambuzi mkubwa pia. Tunapaswa kufundisha miili yetu njia bora za kuchochea akili zetu kutupeleka kwenye utambuzi wa hali ya juu.

Michezo mbalimbali kama kuogelea, kuruka angani, kupanda milima na michezo yote inayohusisha nguvu na akili, imekuwa inatumiwa na wengi kufikia hali ya utambuzi wa juu. Na kadiri mchezo unavyokuwa hatari, ndivyo mtu anaweza kufikia utambuzi wa juu zaidi. Kitu kinachofanya wengi kuwa tegemezi kwenye michezo hii licha ya michezo hiyo kuwa na hatari.

NGUVU YA TATU; FAMASIA.

Famasia ni nguvu nyingine tunayoweza kuitumia kufikia utambuzi wa hali ya juu. Kupitia famasia tunaweza kutengeneza dawa zinazoendana na kemikali zinazochangamsha ubongo na kurahisisha kukifia utambuzi wa hali ya juu.

Karibu kila jamii ina mimea ambayo imekuwa inatumika kutengeneza vilevi, kabla hata ya kuja mapinduzi ya viwanda. Wanaoishi eneo lenye minazi wamekuwa wanatengeneza pombe kwa mnazi, wanaoishi kwenye ndizi pombe zinatokana na ndizi kadhalika wanaoishi kwenye mahindi na mazao mengine. Lakini pia ipo mimea ambayo matumizi yake yamekuwa yanaleta hali ya kubadilika kwa utambuzi, mimea kama tumbaku, bangi, mirungi na hata aina za uyoga.

Kumekuwa na madawa mengi kwa sasa ambayo yanazalishwa na mimea ambayo ina kemikali zinazoweza kutupeleka kwenye utambuzi wa hali ya juu. Kemikali hizi hujulikana kama pyschedelic. Pia tunaona mataifa mbalimbali sasa yakiruhusu matumizi ya bangi kwa matibabu au burudani, bangi ina kemikali ambayo inawezesha mtu kufikia utambuzi wa hali ya juu haraka. Ndiyo maana watumiaji wa bangi huwa wanapata hali fulani ambayo siyo ya kawaida, hali ambayo hawawezi kuielezea.

Kutumia famasia kufikia utambuzi wa hali ya juu nashauri sana mtu kujifunza madhara ya kemikali na mimea mbalimbali kabla ya kuitumia. Kwa sababu baadhi ina nguvu kubwa ambayo inaweza kuharibu kabisa maisha ya mtu.

NGUVU YA NNE; TEKNOLOJIA.

Maendeleo ya teknolojia yamefanya iwe rahisi kwa watu kuweza kufikia utambuzi wa hali ya juu kwa hali ya usalama zaidi. Michezo mbalimbali ambayo zamani ilikuwa hatari sana na pia inaleta uwezo wa kufikia utambuzi mkubwa kwa sasa inaweza kufanywa kwa usalama zaidi. Pia teknolojia za sauti na picha zinaweza kuchochea ubongo wetu kuzalisha kemikali zinazoweza kutufikisha kwenye utambuzi wa juu.

Muziki ni moja ya eneo ambalo limeboreshwa sana kiteknolojia, ambapo namna sauti zinavyopangiliwa, inaweza kuchochea akili ya mtu kwenda kwenye utambuzi wa hali ya juu. Kadhalika picha na michoro mbalimbali, mwanga unapotumiwa vizuri. Maeneo ya starehe, huwa yanawekwa mwanga na muziki ambao unaweza kuwakusanya watu pamoja na kuwafanya wawe kwenye utambuzi wa hali ya juu sana.

Pia teknolojia imekua kiasi cha kuwepo kwa vifaa ambavyo mtu anaweza kuvaa mwilini na vikachochea kwenda kwenye utambuzi wa hali ya juu.

Kutumia teknolojia kufikia utambuzi wa hali ya juu, chagua teknolojia unayoweza kuitumia, kama ni muziki, picha au hata vifaa vya kuvaa. Lakini unapaswa kuwa makini kwa sababu teknolojia hizi zinaweza kuwa na utegemezi.

Mfano utegemezi mkubwa wa wengi kwenye mitandao ya kijamii ni kwa sababu mitandao hii imetengenezwa kwa namna ambayo inachochea akili kuzalisha kemikali inayoleta raha, kwa kiwango kidogo kidogo. Hivyo ili mtu aendelee kupata raha hiyo, lazima aendelee kutumia mitandao hiyo.

HATARI YA KUFIKIA UTAMBUZI WA HALI YA JUU.   

Hakuna kitu kizuri ambacho hakina madhara, hata chakula, japo ni kitabu na muhimu kwa afya, ukila sana kinageuka kuwa sumu.

Kadhalika kwenye kufikia utambuzi wa hali ya juu, japo kuna faida kwenye ukuaji wetu binafsi na kutatua changamoto mbalimbali tunazopitia, kuna hatari kubwa sana ya utambuzi huu wa hali ya juu.

Hatari kubwa kwenye utambuzi wa hali ya juu inaanzia kwenye njia zinazotumiwa na wengi kufikia. Njia ambazo wengi wamekuwa wanatumia, hasa zile za madawa na teknolojia, zina uwezo wa kumpeleka mtu kwenye kiwango cha juu sana cha utambuzi, kitu ambacho kikampelekea kufa au kupata ugonjwa wa akili.

Hivyo tunapaswa kujua hatari hizi kubwa kabla hatujaingia kwenye mazoezi hayo, ili tujue wapi pa kuishia na wakati gani wa kurudi kabla mambo hayajawa hatari zaidi.

Kuna hatari kubwa nne kwenye kufikia utambuzi wa juu;

Hatari ya kwanza ni mtu mwenyewe kujidhuru katika kufikia utambuzi wa juu. Baadhi ya njia ambazo zinatumika kufikia utambuzi huu wa juu huwa zina madhara, hasa kwa upande wa dawa na teknolojia. Kama mtu hatajiwekea ukomo na kuweza kujidhibiti ni rahisi kujidhuru. Madhara makubwa yapo kwenye kupata ugonjwa wa akili na hata kifo.

Hatari ya pili ni serikali kuweza kutumia nguvu zinazoleta utambuzi wa hali ya juu katika kuwadhibiti na kuwatawala watu. Njia nyingi zinazoleta utambuzi wa hali ya juu pia zina uteja na utegemezi, iwapo serikali ya kidikteta utaweza kutumia njia hizi, itawatawala watu bila ya wao wenyewe kujua.

Hatari ya tatu ni jeshi kutumia nguvu hii katika vita, hasa upande wa propaganda. Nguvu hizi zina uwezo wa kutumiwa vibaya kivita na zikaleta madhara makubwa. Mfano baadhi ya madawa yanayoleta utambuzi wa hali ya juu kwa kiwango fulani yanaweza kuleta fujo na taharuki kwa watu.

Hatari ya nne ni makampuni makubwa kutumia nguvu hizi kuwafanya wateja washawishike kununua bidhaa wanazouza, hata kama hazina manufaa kwao. Hili tumeshaanza kuliona kwenye makampuni makubwa ya teknolojia, yanawafanya wateja kuwa tegemezi kwao kwa ajili ya furaha.

Hatari hizi nne tunapaswa kuziangalia kwa umakini ili kutafuta kwetu utambuzi wa hali ya juu kusigeuke kuwa madhara kwetu. Kwenye makinikia nitakushirikisha tahadhari za kuchukua ili hatari hizi zisikudhuru.

HITIMISHO; UWEZO WA UTAMBUZI MKUBWA UNAO, ILA UTUMIE KWA MAKINI.

Uwezo wa kufikia utambuzi mkubwa unao na uwezo huu unaweza kuutumia kujifunza zaidi, kujiponya na kuweza kuzalisha kazi bora sana kwenye kile unachofanya.

Lakini unapaswa kuwa na tahadhari na kutumia umakini mkubwa kwa njia unazotumia kufikia uwezo mkubwa wa utambuzi wa hali ya juu ulionao.

Kwa ushauri wangu kwako kama kocha wako, nashauri sana utumie njia za asili za kufikia utambuzi wa hali ya juu, japo itakuchukua muda na kazi kuweza kufikia uwezo huo mkubwa, madhara yake yanakuwa machache kuliko kutumia njia ambazo siyo za asili kama madawa au teknolojia.

Kufanya tahajudi kwa kina kila siku, kwa angalau saa moja, ukiwa na utulivu mkubwa na umakini wa hali ya juu, ni njia nzuri kwako kuweza kufikia akili ya ndani na kuweza kupata utambuzi mkubwa. Pia kuchagua muziki unaopenda kusikiliza na kuweka umakini wako na hisia zako kwenye mziki huo kutakusaidia kufikia utambuzi wa hali ya juu. Kadhalika jinsi unavyouweka mwili wako kuna mchango mkubwa kwenye kuchangamsha akili yako na kufikia utambuzi wa hali ya juu.

Hapa umeshajifunza jinsi watu wanavyotumia mapinduzi ya sasa kupiga hatua zaidi, umeshaelewa jinsi watu wanavyoiba moto na kuutuma kwa manufaa yao. Nenda na wewe ukaibe moto kwa kufikia utambuzi mkubwa ndani yako, lakini kuwa makini moto huo usikuunguze.

#3 MAKALA YA JUMA; HALI NNE UNAZOZIPATA WAKATI UKIWA KWENYE UTAMBUZI WA HALI YA JUU.

Rafiki, kama tulivyojifunza kwenye kitabu cha juma, kila mmoja wetu anaweza kufikia hali ya juu kabisa ya utambuzi, pale akili yake ya kawaida inayofikiri inapozimwa kwa muda na akili isiyofikiri inaposhika hatamu. Akili isiyofikiri ina nguvu kubwa na ina taarifa nyingi kuliko akili inayofikiri.

Unapokuwa kwenye utambuzi wa hali ya juu, kuna hali nne ambazo unazipitia, hali hizi ndizo zinazofanya utambuzi wa hali ya juu kuwa na manufaa sana kwako. Kwani ni kwenye hali hizi ndiyo unapata utulivu, unapata majibu ya changamoto mbalimbali na pia unapata mtazamo wa kipekee ambao hukuwa nao hapo awali.

Katika makala ya juma hili, nimekushirikisha hali hizo nne unazopitia unapokuwa kwenye utambuzi wa hali ya juu. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, isome sasa hapa; Hali Nne Unazozipata Pale Akili Yako Inapovuka Hali Ya Kawaida Na Kwenda Kwenye Hali Ya Kufanya Miujiza.

Ukizijua hali hizo nne na kuweza kuzitumia vizuri, utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako na kujijengea uhuru kamili. Soma makala hiyo na ufanyie kazi.

#4 TUONGEE PESA; UTAMBUZI WA HALI YA JUU KWENYE FEDHA.

Moja ya changamoto kubwa sana ambayo wengi wanapitia kwenye fedha na inayokuwa kikwazo kwao ni kufikiri katika uhaba.

Watu wengi wamekuwa wakiamini kwamba kinachofanya matajiri waendelee kuwa matajiri na masikini kuendelea kuwa masikini ni kwamba matajiri wanawaibia masikini.

Wengine wamekuwa wakienda mbali zaidi na kusema kama fedha zote zitakusanywa na kila mtu agawiwe kwa usawa, basi dunia itakuwa na usawa. Na wengine wanasema kama matajiri watatozwa kodi zaidi na masikini wakapewa kipato cha kuendesha maisha yao hata kama hawana kazi basi dunia itakuwa sehemu bora ya kuishi.

Waandishi wa kitabu cha STEALING FIRE wanasema matatizo magumu yanapotatuliwa kwa njia rahisi yamekuwa yanatengeneza matatizo zaidi. Na wametoa mfano wa juhudi za kupambana na umasikini, ambapo mataifa yaliyoendelea yamekuwa yanatoa misaada kwa mataifa masikini, kitu ambacho kimezalisha tatizo kubwa la rushwa katika nchi masikini.

Hivyo inapokuja kwenye fedha, tunapaswa kuelewa kwamba matatizo magumu hayahitaji majibu rahisi, bali yanahitaji majibu ya uhakika. Na majibu ya uhakika yanapatikana pale mtu anapoweza kutumia utambuzi wa hali ya juu kupata jawabu la matatizo hayo magumu.

Inapokuja upande wa fedha binafsi, unapaswa kutumia uwezo wako wa kufikia utambuzi wa hali ya juu kuweza kujijengea fikra za utele kwenye eneo la fedha. Uache kuona uhaba na uanze kuona utele. Uache kuona hakuna fedha na uanze kuona changamoto za watu unazoweza kuzitatua na ukalipwa zaidi. Uache kuona kazi au biashara unayofanya sasa haikulipi na uanze kuona fursa zaidi zinazopatikana kwenye kazi au biashara unayofanya.

Yote hayo yatawezekana kama utaweza kuzama ndani kwenye akili yako isiyofikiri, akili ambayo ina majibu ya kila kitu, lakini imekuwa haipati nafasi ya kukupa majibu hayo, kwa sababu kila wakati akili inayofikiri inakuwa imetingwa na mawazo ambayo hayana manufaa kwako.

Mara kwa mara ingia kwenye hali ya utambuzi wa hali ya juu, kwa njia zilizo salama kwako, huku ukiwa na swali unawezaje kuongeza kipato chako zaidi. Ukizima akili inayofikiri, ile ambayo inahukumu na kukukatisha tamaa kwenye mengi, na ukaruhusu akili isiyofikiri ishike hatamu, utapata majibu mengi sana ya namna unavyoweza kuongeza kipato, kwa kuanzia hapo ulipo sasa. Ukiwa kwenye hali hii ni kama vile pazia linalokuzuia wewe usizione fursa zinazokuzunguka linakuwa limeondolewa, na hapo unajionea mwenyewe kila aina ya fursa.

Ninachokuambua hapa rafiki yangu ni hiki, hapo ulipo sasa umezungukwa na fursa nyingi sana za kukuwezesha kukuza kipato chako zaidi. Lakini huzioni au hujui utazitumiaje kwa sababu akili yako inayofikiri ndiyo kikwazo kwako. Ukiweza kuipumzisha akili hii kwa muda, na kuzama ndani kwenye akili isiyofikiri, utaweza kuona fursa hizi na jinsi ya kuzitumia. Hebu tumia sasa akili yako ya ndani na uwezo wako wa juu wa utambuzi kuweza kuona na kutumia fursa zinazokuzunguka hapo ulipo sasa.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; SIYO KILA TATIZO NI MSUMARI KWA NYUNDO YAKO.

“Abraham Maslow once famously said, “When all you’ve got is a hammer, every problem looks like a nail.” What he meant was, when it comes to problem-solving, we tend to get locked into using familiar tools in expected ways.” ― Steven Kotler

Kama ambavyo mwandishi Steven Kotler ametushirikisha kauli ya mwanasaikolojia Abraham Maslow, huwa tuna kawaida ya kuona kila tatizo bali linatatulika kwa suluhisho tulilonalo. Huwa ni vigumu kwetu kukubali kwamba tatizo tunalopitia linahitaji utambuzi tofauti katika kulitatua. Tunakazana kutumia njia tuliyozoea, hata kama haileti matatizo. Na hiki ndiyo chanzo cha wengi kukwama.

Kama unataka kutoka pale ulipokwama sasa, iwe ni kwenye kazi au biashara, lazima kwanza ukubali kwamba njia uliyozoea kutumia haifanyi kazi tena. Kama umekuwa kwenye biashara au kazi kwa muda mrefu lakini hujaweza kupiga hatua kubwa, lazima ukubali kwamba namna ambavyo umekuwa unafanya kazi au biashara hiyo siyo sahihi. Na kwa kukubali hivi ni hatua ya kwanza ya kujifunza zaidi, ili kuja na njia tofauti za kufanya ambazo zitakupa matokeo tofauti.

Mwanasayansi Albert Eisntein amewahi kunukuliwa akisema ujinga ni kufanya kitu kile kile, kwa njia ile ile na kutegemea kupata matokeo ya tofauti. Hii haina tofauti na kutumia suluhisho moja kwa kila tatizo halafu utegemee matokeo ya tofauti.

Kataa mazoea kwenye maisha yako, acha kabisa kutumia njia ile ile ambayo imeshindwa kuleta matokeo bora kwenye maisha yako. Kila wakati kaa chini na fikiria njia bora ya kufanya kile unachofanya, kila unapokutana na tatizo jipya, usikimbilie kulitatua kwanza, badala yake kaa chini na fikiria ipi njia bora ya kulitatua.

Na pale unapotuliza akili yako na kufikia utambuzi wa hali ya juu, utaweza kuona njia bora za kukabiliana na chochote unachokutana nacho. Una uwezo mkubwa sana ndani yako wa kuweza kukabiliana na kila unachokutana nacho, unachohitaji ni kufikia utambuzi wa hali ya juu ili kuweza kutumia uwezo huo.

Rafiki, hizi ndiyo tano za juma kutoka kwenye kitabu cha STEALING FIRE, ambacho kimetuonesha mapinduzi makubwa ya kiutambuzi yanayoendelea duniani.

Kuna tahadhari kubwa sana ambayo waandishi wameitoa katika zile hali nne unazopitia unapokuwa kwenye utambuzi wa hali ya juu. Tahadhari hizi unapaswa kuzielewa kabla hujaanza kujaribu kufikia utambuzi wa juu, kwa sababu hakuna kizuri kisichokuwa na kasoro yake.

Katika mafunzo ya ziada (#MAKINIKIA) ya kitabu hiki, ambayo nakushirikisha kupitia channel ya TANO ZA JUMA, nitakupa tahadhari hizo nne muhimu na jinsi ya kupima hatari na faida ya kuingia kwenye utambuzi wa hali ya juu. Kama bado hujajiunga na channel hii, jiunge sasa (maelekezo yako hapo chini) ili usikose tahadhari hizi muhimu kwenye kutumia uwezo wako mkubwa, kwa kuwa wengi wanaochukua hatua bila ya tahadhari, wameishia kuharibu maisha yao.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu