“If a person gave away your body to some passerby, you’d be furious. Yet you hand over your mind to anyone who comes along, so they may abuse you, leaving it disturbed and troubled—have you no shame in that?”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 28
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIGAWE HOVYO UHURU WAKO…
Tunalinda na kujali sana miili yetu, tunaisafisha na kuivalisha vizuri.
Na kama mtu yeyote atagusa miili yetu tofauti na matakwa yetu, tunakuwa wakali mno.
Mtu akaja na maji machafu akakumwagia mwilini hutamwelewa kabisa, utagombana naye kwa jambo hilo baya alilofanya.
Lakini inapokuja kwenye akili zetu, wala hatujali sana. Tunaruhusu wengine wazitumie kama wanavyotaka wenyewe.
Mtu akija na uchafu wake na kuumwaga kwenye akili zetu wala hatulalamiki.
Na mbaya zaidi, sisi wenyewe ndiyo tunaotafuta uchafu wa kujaza kwenye akili zetu.
Tunatembelea mitandao ya kijamii ambayo tunajua hakuna kikubwa tunajifunza zaidi ya kufuatilia maisha ya wengine na umbeya.
Tunaangalia tv ambapo hakuna kikubwa tunajifunza zaidi ya habari hasi na maigizo yenye nia ya kuharibu fikra zetu.
Tunatumia vibaya akili zetu kwa kufuatilia maisha ya wengine kitu ambacho hakina manufaa yoyote kwetu.
Hivi ndivyo tunavyogawa uhuru wetu bure, ndivyo tunavyowapa wengine nafasi ya kututawala, kwa kuruhusu akili zetu zitumiwe hovyo na yeyote anayeweza kufanya hivyo.
Tunapaswa kuwa wakali sana na akili zetu, tunapaswa kuwa na msimamo mkali na kulinda uhuru wetu wa kufikiri usiingiliwe na yeyote.
Tunapaswa kusafisha akili zetu na kuzivalisha vizuri kwa kupata maarifa sahihi.
Na kuepuka sana uchafu wa mitandao ya kijamii, habari na hata umbeya.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kulinda sana uhuru wako kwa kutoruhusu akili yako itumiwe hovyo na wengine.
#LindaUhuruWako, #LishaFikraZako, #SafishaAkiliYako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha