Uhuru kamili kwenye maisha unakuja pale unapoweza kuachilia, lakini ni vigumu kuachilia, ndiyo maana wengi hawapo huru, wengi wanazama na yale wanayoshikilia.
Chukulia maisha kama mfano wa kuogelea kwenye maji, unapokuwa kwenye maji, ili uweze kuogelea huyashikilii maji, badala yake unayaachia na kujiachilia kwenye maji, na hilo ndiyo linakuwezesha kuelea na kuogelea.
Kama utakazana kuyashikilia maji, utazama.
Kwenye maisha watu wanashikilia vitu vingi sana, na mzigo mkubwa wa watu wanaoshikilia ni hisia hasi kama za chuki, hasira, wivu na hata vinyongo. Hisia hizi zinawafanya watu wakose uhuru.
Kwa mfano kama mtu amekukosea sana, na hilo likakupa hasira na ukawa na kinyongo naye, anayeumia zaidi ni wewe kwenye hasira na kinyongo kuliko yule uliyemwekea kinyongo. Kufanya hivi ni sawa na kunywa sumu wewe mwenyewe halafu utegemee mtu mwingine adhurike.
Msingi mkuu wa maisha ni kuachilia, uhuru kamili unakuja pale unapoweza kuachilia na kutojishikiza na chochote.
Hata upande wa mali, fedha na utajiri, wapo watu wanaopata fedha kidogo na kuzishikilia hizo zisipotee, kinachotokea hawapati fedha zaidi. Lakini mtu unapokuwa tayari kuachilia, unakuwa huru kujaribu vitu bora zaidi na hivyo vinakuwezesha kupata zaidi.
Hata dunia inajua nani anaachilia na nani anashikilia na ina tabia ya kuwapa zaidi wale wanaoachilia.
Kumbuka hili kila siku, chochote unachoshikilia kinakuzamisha, kuwa mtu wa kuachilia na utakuwa na uhuru mkubwa kwenye maisha yako utakaokufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,