Katika zama tunazoishi sasa, mambo yanaenda kasi sana kiasi kwamba watu wamesahau kabisa nini kinahitajika kwenye kazi zao.
Tunaishi kwenye zama za taarifa, ambapo watu hawawezi kutofautisha kati ya taarifa, maarifa na kelele. Kila mtu anapiga kelele akiamini kelele zaidi zitamfanya ajulikane na wengi.
Na hapo ndipo unapoangalia mitandao ya kijamii na jinsi watu wanaitumia kutangaza kazi au biashara wanazofanya. Wanatumia muda na nguvu nyingi katika kutangaza, kuliko muda na nguvu wanazotumia katika kufanya kazi au biashara zao.
Watu wanaweza nguvu nyingi kwenye kutangaza (kwa usahihi; kupiga kelele) lakini watu wanapojaribu kupata huduma kwenye biashara au kazi hizo, hawapati huduma bora na hivyo hawasukumwi kurudi tena kupata huduma pale.
Kutangaza ni muhimu sana, lakini usisahau kitu muhimu zaidi ambacho ni kufanya kazi iliyo bora sana, kutoa huduma ambayo ni bora sana, ambayo mteja kwa kuijaribu, anatamani kurudi tena na hawezi kutulia bali kumwambia kila mtu kuhusu huduma yako.
Kazi yako inapaswa kukutangaza wewe kuliko wewe unavyoitangaza kazi yako. Na njia pekee ya kazi yako kukutangaza ni kuweka ubora wa hali ya juu sana kwenye kile unachofanya, kutoa thamani kubwa sana ambayo watu hawawezi kuipata sehemu nyingine yoyote.
Kuwa bora sana kwenye kile unachofanya, kuwa bora kiasi kwamba mtu anaposikia kuhusu wewe, haanzi kuuliza kama unachofanya ni kizuri, bali anakuwa balozi mzuri wa kile unachofanya.
Na utaweza kufikia hili kama utaweka vipaumbele vyako kwa usahihi, kama utaacha kupiga kelele na kuweka thamani kubwa kwenye kile unachofanya.
Unachopaswa kujua ni kwamba, kuweka thamani kunahitaji muda mpaka watu waanze kukuelewa na kusambaza kazi zako, lakini kunadumu kwa muda mrefu. Lakini kupiga kelele kunaweza kukuletea watu wengi kwa wakati mmoja, lakini hawatadumu, kwa sababu watu hawafuati kelele pekee, wanataka thamani kubwa pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,