Kila mtu anapenda faida kubwa, anapenda matokeo mazuri na makubwa na anapenda kupata zaidi ya alivyozoea kupata.
Lakini wengi wamekuwa wanatumia muda na nguvu zao kufikiria ile faida wanayopata pekee. Na hivyo mtu anapokuja kwao na mpango wa kupata faida zaidi, au wa kupata manufaa makubwa, huwa wanakimbilia kufanyia kazi mpango huo kabla hawajauelewa vizuri. Kinachotokea ni kupata hasara kubwa kwa kuwa hawakujua vyema.
Faida kubwa huwa haitembei yenyewe, bali huwa inaambatana na vitu viwili vya karibu sana, ambavyo ni gharama na hatari.
Kadiri unavyotegemea kupata faida kubwa, ndivyo gharama za kupata faida hiyo zinavyokuwa kubwa pia. Hivyo huwezi kupata faida kubwa kama haupo tayari kuingia gharama kubwa pia. Huwezi kupata faida kubwa kwenye biashara yako kama haupo tayari kufanya uwekezaji mkubwa pia. Na huwezi kupata faida kubwa kwenye taaluma na ujuzi wako kama hutawekeza gharama kubwa kwenye kukuza ujuzi wako na kupata maarifa bora kila wakati. Faida inaambatana na gharama, lazima ulipe gharama kupata faida.
Kitu cha pili kinachoambatana na faida kubwa ni hatari, kadiri faida unayotegemea kupata inavyokuwa kubwa, ndivyo pia hatari ya kupoteza inavyokuwa kubwa. Hatua unazochukua ili upate faida kubwa, zinaposhindwa zinakuletea hasara kubwa pia. Hivyo lazima uelewe kila hatari unayoweza kuingia pale unapofikiria kupata faida kubwa kuliko unayopata sasa. Unachopaswa kujua ni kwamba hatari inaambatana na faida kubwa, hivyo swali siyo kuna hatari au hakuna, bali swali ni hatari ni ipi na unaivukaje.
Wengi wamekuwa wakitaka faida kubwa, kwa gharama ndogo na bila ya hatari yoyote, kitu ambacho ni kujidanganya. Unachopaswa kuangalia wewe ni kuwekeza gharama ambazo unaweza, na kuwa na mbadala wa kukuepusha na hatari inayojitokeza, kisha kuweka juhudi na umakini wako kwenye kile unachofanya. Hata unapopoteza, chukulia kama somo ili wakati mwingine ufanye kwa ubora zaidi.
Unaweza kupata faida kubwa zaidi ya unayopata sasa, kama utakuwa tayari kuweka gharama zinazohitajika, na kuwa tayari kubeba hatari inayotokana na faida hiyo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,