Tatizo kubwa la watu wa kawaida, ambao ndiyo sehemu kubwa ya watu katika zama hizi, hawapo kwenye chochote wanachofanya.

Watu hawa wanaangalia lakini hawaoni,

Wanasikiliza lakini hawasikii,

Wanakula lakini hawaipati ladha,

Wanagusa lakini hawapati hisia,

Wanavuta pumzi bila ya kusikia harufu,

Wanatembea bila ya kuwa na uelewa wa hatua mwili unachukua

Na wanaongea bila ya kufikiri.

Kwa kifupi watu wanafanya kitu kimoja, huku fikra zao zipo kwenye kitu kingine tofauti kabisa. Kwa njia hii watu hawaridhishwi wala kufurahishwa na chochote wanachofanya. Kila ambacho mtu anafanya kinakuwa kama adhabu, kama kitu ambacho kinampotezea mtu muda, huku akiwahi kwenye kitu kingine ambacho pia anakifanya kwa njia ile ile.

Kataa kuwa mtu wa kawaida na kataa kufanya chochote kama kinakupotezea muda. Weka fikra zako na umakini wako kwenye chochote unachofanya. hii ndiyo njia pekee ya kunufaika na hicho unachofanya. Hata kama ni kitu kidogo kiasi gani, unapoweka umakini wako wote, unakifanya kwa ubora zaidi na unapata kuridhika zaidi ndani yako.

Acha kuishi maisha ya kawaida, maisha ya mazoea na maisha ya kukimbizana na kila unachofanya kama vile kunapoteza muda wako. Chagua kufanya vile ambavyo ni muhimu na vifanye kwa umakini wako wote. Hakuna chochote kitakachoonekana kidogo kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha